Mei 29, 2023 Mahakama ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, mbele ya Mh. SASI SORO, imemtia hatiani Mshtakiwa WILSON MSHIMI NGOLANYA, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimana, katika Shauri la Uhujumu Uchumi namba ECC.05/2022.
Katika shauri hili Mshtakiwa alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kuomba Rushwa ya Ngono kutoka kwa binti (jina linahifadhiwa) ili amsaidie kutatua mgogoro wa ardhi uliotokea baada ya wanakijiji wawili kuvamia shamba la marehemu (jambo ambalo ni kosa chini ya kifungu cha 25 cha PCCA).
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hili, upande wa Jamhuri ulipeleka jumla ya mashahidi nane (08) na vielelezo vitano (05), ambavyo vilitosha kumtia mshtakiwa hatiani.
Mwendesha Mashtaka YAHAYA MASAKILIJA aliiomba Mahakama kuzingatia kifungu cha 60(2) cha EOCCA wakati wa kutoa adhabu, huku kwa upande wa mshtakiwa ukiomba shufaa kutoka kwa mahakama.
Mahakama imesema imezingatia shufaa za mshtakiwa na imemhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka miwili (02) jela au kulipa faini ya shilingi laki tano (500,000). TAKUKURU , Manyara. Mei 29, 2023