Mei 26, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) nchini Bw. Aretas James Lyimo, wamesaini Mkataba wa Makubaliano ya kikazi (Memorandum of Understanding – MoU) baina ya Taasisi hizi, yenye madhumuni ya kuongeza wigo na nguvu ya kukabiliana na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na tatizo la rushwa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara tu baada ya kusaini MoU hiyo, Mkurugenzi Mkuu amesema, Rushwa ni kati ya vichocheo vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya duniani na pia biashara ya dawa za kulevya ni kati ya vichocheo vya vitendo vya rushwa ambapo wafanyabiashara au watumiaji wa dawa za kulevya hutumia rushwa kuwanyamazisha watendaji wasiokuwa waadilifu wa mamlaka za usimamizi wa sheria ili wasichukuliwe hatua za kisheria.
Pamoja na mambo mengine, Mkataba huu uliosainiwa TAKUKURU Makao Makuu Dodoma na kushuhudiwa na Viongozi wa taasisi zote mbili, umetaja maeneo yafuatayo ya ushirkiano: –
- Kutoa mafunzo kwa watumishi wa DCEA na TAKUKURU;
- Kubadilishana taarifa muhimu zitakazowezesha kukabili biashara ya dawa kulevya, matumizi ya dawa za kulevya, na vitendo vya rushwa katika jamii;
- Kushirikiana kutoa elimu kwa umma kwa kutumia njia na majukwaa mbalimbali zikiwamo klabu za wapinga rushwa shuleni na vyuoni
- Kuhamasisha wanafunzi, vijana na jamii kwa ujumla kutoshiriki vitendo vya rushwa na biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuchukua hatua kukabili makosa haya;