Mha. Joseph Mwaiswelo Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma – TAKUKURU amezindua Filamu ya TANJEMA ambayo imelenga kuwajenga vijana hususan wanafunzi wa shule za msingi kuwa na Maadili, Wawajibikaji, Wazalendo na Wasioivumilia RUSHWA.
Filamu hiyo iliyozinduliwa Mei 15, 2023, imeandaliwa na vijana wanne wahitimu wa Programu ya Marekani inayojulikana kama ‘Mandela Washington Fellowship’.
Akizindua filamu hiyo, Mha. Mwaiswelo amewataka wanafunzi na walimu kuwajibika katika nafasi walizonazo kwa kuondokana na vitendo vya rushwa kwani hakuna mtu atakayeweza kuijenga Tanzania bali Watanzania wenyewe.
Wito huo umekuja wakati muafaka ambapo Serikali imejikita katika kuzuia vitendo vya Rushwa kabla havijatokea msisitizo ukiwa ni kuwaelimisha vijana tangu wakiwa shuleni.