Rais wa sasa wa Mtandao wa Ufuatiliaji na Urejeshaji wa Mali – Afrika Mashariki (Asset Recovery Inter-Agency Network for Eastern Africa – ARINEA) Bi. Lilian William Kafiti, ameshiriki Mjadala kati ya Mtandao wa Ufuatiliaji na Urejeshaji wa Mali wa Mamlaka za Kupambana na Rushwa (Asset Recovery Inter Agency Networks – ARINs) na Kikosi Kazi cha Kupambana na Fedha Haramu, Ugaidi na Silaha za Maangamizi (Financial Action Task Force – FATF).
Mjadala huo ulifanyika Mei 5, 2023 wakati wa Mkutano Mkuu wa 19 wa Camdem Assets Inter – Agency Network – CARIN, uliofanyika Brussels, Belgium na ajenda iliyojadiliwa ilihusu namna ya kukuza ushirikiano kati ya FATF na ARINs.
CARIN ni Mtandao wa Ufuatiliaji na Urejeshaji Mali ukijumuisha nchi za Umoja wa Ulaya, Marekani na Jumuiya za Kimataifa, ambapo TAKUKURU ni waangalizi (Observer) wa mtandao huo kupitia ARIN-EA.
Akichangia katika mjadala huo, Bi. Lilian ambaye pia ni Afisa Uchunguzi na Mwanasheria kutoka Kurugenzi ya Huduma za Sheria TAKUKURU alisema pamoja na mambo mengine, wakati sasa umefika kwa FATF kuingiza mitandao hii kwenye Mpango Mkakati wa FATF ili kila nchi mwanachama iweze kupimwa ni kwa kiwango gani mitandao hii imetumika na kusaidia katika ufuatiliaji na urejeshaji mali kwa nchi husika. ARINEA ilianzishwa Mwaka 2013 katika Mkutano wa Mwaka wa Shirikisho la Mamlaka za Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki – Eastern Africa Association of Anti-Corruption Authorities EAAACA, lengo likiwa ni kutengeneza mtandao wa watalaam watakaowezesha urahisi wa urejeshwaji wa mali zilizotokana na njia ya uhalifu ikiwemo rushwa na kurejeshwa nchi husika. Bi.Lilian ni Rais wa ARINEA kwa kipindi cha Mwaka 2020 hadi 2024.