Mei 3, 2023, katika Mahakama ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera mbele ya Mhe. KAVALO, Shauri la Rushwa na Uhujumu Uchumi Namba 8/2022 limetolewa maamuzi kwa mshitakiwa Wisman Ngyanabo Geshaza kutiwa hatiani baada ya kusikiliza mashahidi watano na vielelezo vinne huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wawili.
Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashtaka wa TAKUKURU Bw. Kelvin Murusuri (Wakili Kiongozi), akisaidiana na Bw. Leodger Siriwa(Wakili wa Jamhuri – Ngara).
Ilithibitika mahakamani kuwa mshitakiwa ambaye alikuwa ni Mkusanya Mapato, alifanya ubadhirifu wa fedha za Halmashauri ya Ngara kupitia POS No. 47 kiasi cha sh. 3,027,356 ambazo ilibainika zilikusanywa na yeye kama Mkusanya Mapato kwa POS hiyo tajwa na hivyo kushtakiwa kwa kosa la ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marekebisho ya Mwaka 2022.
Mhe. Hakimu KAVALO, amemhukumu mshitakiwa kulipa fine ya shilingi za kitanzania laki tano (sh. 500,000), au kutumikia jela kifungo cha miaka miwili. Pia aliamriwa arejeshe fedha zote alizofanyia ubadhirifu kiasi cha sh 3,027,356/- TAKUKURU Kagera, Mei 3, 2023