Katika Mahakama ya Mkoa wa Kagera mnamo Aprili 25, 2023 imetolewa hukumu katika Shauri la Rushwa Na.02/2023 mbele ya Mhe. Yona.
Shauri hili liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Kelvin Murusuri
Shauri hilo lilikuwa dhidi ya Lilian Stanslaus Mwangwa – Afisa wa NIDA Kituo cha ILEMELA, aliyeshitakiwa kwa kupokea Hongo ya Shilingi za Kitanzania 51,000/- kutoka kwa Timothy Nakoko Gerorge, Raia wa Uganda kupitia M-pesa yake.
Alishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya Rushwa chini ya kifungu cha 15 (1) (b) & (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa SURA ya 329 marekebisho ya Mwaka 2022.
Lengo lilikuwa ni kufanikisha kumpatia Bw. Timothy Nakoko George, Kitambulisho cha Taifa ilihali hastahili.
Aliposomewa Mashtaka yake Mshtakiwa alikiri Mashtaka hayo kwamba ni kweli alitenda kosa hilo huku akijua kabisa ni kinyume na sheria.
Baada ya kukiri Mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kufanya kosa hilo na katika kuomba shufaaa aliomba kupewa adhabu ndogo (lenient) kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana mtoto mdogo anayenyonya, hivyo kumtegemea na hajaisumbua Mahakama.
Mwendesha Mashtaka Bw. Murusuri aliieleza Mahakama ni kwa namna gani vitendo hivi ni kero kwa jamii na hivyo kuiomba Mahakama kumpa adhabu Mshtakiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mhe. Yona – Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera, alimtia hatiani Mshtakiwa chini ya kifungu cha 15 (1)(b) & (2) cha PCCA na kumpa adhabu ya kulipa fine ya shilingi za kitanzania laki tano (sh. 500,000)au kwenda jela miaka mitatu.
TAKUKURU KAGERA, Aprili 25, 2023