Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mhimili wa Mahakama kushiriki katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 pamoja na maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo 2050 ili kuenda sambamba na mfumo wa sheria na utawala bora.
Makamu wa Rais amesema hayo Aprili 12, 2023 akifungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 uliofanyika mkoani Mwanza.
Kupitia mkutano huo, Makamu wa Rais ametoa wito wa kufanya maboresho yatakayopelekea kupunguza urasimu ili kuharakisha kukamilika kwa mashauri na amewataka kuendelea kuboresha matumizi ya tehama pamoja na kuutumia mkutano huo kufanya tathmini ya mianya na viashiria vya rushwa na kuchukua hatua stahiki.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP. Salum Rashid Hamduni ameshiriki mkutano huu ambapo mada kuhusu TATHMINI YA HALI YA RUSHWA KATIKA MAHAKAMA TANZANIA iliwasilishwa.