Kaimu Mkurungezi Mkuu wa TAKUKURU Bibi. Neema Mwakalyelye amefungua mafunzo ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma kwa watumishi wa TAKUKURU kutoka mikoa yote Novemba 25, 2022, jijini Dodoma. Akifungua mafunzo, amewataka wanamafunzo hao kujifunza kwa weledi ili kwenda kusimamia vema miradi iliyopo katika maeneo yao na hatimaye thamani halisi ya fedha iweze kupatikana katika kila mradi. Pia amesisitiza uandaaji bora wa taarifa za miradi “…Tunataka baada ya mafunzo haya taarifa zitakazo andikwa baada ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ziwe zenye tija na zenye kueleza mapungufu yaliyobainika pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa miradi”. Kwa sasa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo Taasisi ina wajibu wa kuhakikisha thamani ya fedha katika miradi hiyo inakuwepo hasa kwa kuzingatia kauli mbiu yetu inayosema: “Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; Tutimize wajibu wetu”.