TAKUKURU imefanya Semina kwa Wabunge Wanachama wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika – Tawi la Tanzania (African Parliamentarian Network Against Corruption – APNAC – Tanzania Chapter). Semina hii imefanyika Septemba 16, 2022 jijini Dodoma kwa lengo la kujengeana uwezo katika mapambano dhidi ya rushwa.
Semina hii ilifunguliwa rasmi na Mhe. Deogratius Ndejembi (MB), Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambapo ujumbe wa Wabunge 37 wa APNAC uliongozwa na Mhe. Cecilia Paresso (MB), Makamu Mwenyekiti wa APNAC.
Akitoa maelezo ya utangulizi CP. Salum Rashid Hamduni, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Tulia Ackson (MB) pamoja na Waheshimiwa Wabunge – Wanachama wa APNAC kwakuwa wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha Wabunge wengine kushiriki kwenye mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini kupitia warsha, makongamano pamoja na semina ambazo zimekuwa zikifanyika.