KIKAO KAZI CHA TAKUKURU NA WAKUZA MITAALA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Agosti 25, 2022 imeshiriki kikao kazi na Wakuza Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Anneth Komba pamoja na Kamati ya Kitaifa ya Uboreshaji Mitaala inayoongozwa na Prof. Makenya Maboko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Lengo la kikao kazi hicho ni kuwasilisha mapendekezo ya kuingiza Maudhui ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwenye Mitaala ya Elimu nchini. Kikao kazi hicho kilichofanyika katika ofisi za TET Dar -Es- Salaam ni mwendelezo wa kikao kilichofanyika Aprili 23, 2022 – Chuo cha Mipango, Dodoma na baada ya kukamilishwa kwa uandishi wa rasimu ya Mitaala mwezi Agosti 2022 ambayo inatarajiwa kupelekwa kwa Wadau kupokea maoni zaidi.

Katika kikao hicho, TAKUKURU imesisitiza umuhimu wa elimu dhidi ya rushwa kuingizwa kwenye mitaala ya elimu katika ngazi zote kuanzia awali, msingi, sekondari hadi vyuoni.

Ujumbe wa TAKUKURU, uliongozwa na Bw. Joseph K. Mwaiswelo – Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma aliyeambatana na Dkt. Omari Mzee, Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti, John Kabale, Mkurugenzi Msaidizi wa Uchapishaji na Huduma za Maktaba pamoja na Sarah Chodota, Afisa kutoka wa Timu wa Vijana na Mitaala – Kurugenzi ya Elimu kwa Umma.