Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi. Neema Mwakalyeye, amewataka wadau wanaohusika na uchimbaji madini kuhakikisha kuwa uchimbaji wa madini unapofanyika unahifadhi mazingira. Amesema uwepo wa nchi na ustawi wa wananchi wake unategemea sana uwepo wa mazingira, hivyo ni jukumu la kila mdau husika, kuhakikisha kuwa uchimbaji unapofanyika na kubadili asili, unafanyika kwa kuhifadhi mazingira. Naibu Mkurugenzi Mkuu ametoa maelekezo hayo Agosti 18, 2022 jijini Dodoma, alipokuwa akifungua Warsha ya siku moja ya kupokea na kujadili Taarifa ya TAKUKURU ya Uchambuzi wa Mfumo wa Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira katika Uchimbaji wa Madini nchini. Warsha hiyo iliwashirikisha wadau kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira; Wizara ya Madini; Wizara ya Maji; Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali; Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira; Wawakilishi kutoka Mgodi wa Mwadui – Shinyanga pamoja na TAKUKURU.