Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imefanya tathmini ya maeneo hatarishi yanayochochea vitendo vya rushwa ya ngono katika sekta ya Elimu ya msingi na sekondari. Matokeo ya tathmini hiyo yamejadiliwa katika Warsha ya Wadau iliyofanyika Agosti 11, 2022, katika Ukumbi wa ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Walimu, jijini Dodoma.
Warsha hiyo ilifunguliwa rasmi na Bi. Paulina Mkwana – Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu. Akifungua warsha hiyo, Katibu huyo aliipongeza TAKUKURU kwa kazi nzuri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini na kuwakumbusha washiriki kuwa, mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mdau kama ilivyo ainishwa katika Mkakati wa Kitaifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP).
Bi. Mkwana alisema tatizo la rushwa ya ngono lipo na ni changamoto kubwa kwenye sekta ya elimu nchini, hivyo, alipendekeza kwamba baada ya wasilisho la tathmini hiyo, majadiliano yaambatane na kuweka mikakati mahususi ya kushughulikia tatizo la rushwa ya ngono. Alishauri pia kuwepo na Sekretariat itakayo jumuisha wadau muhimu kwa ajili ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikakati.
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa TAKUKURU Bi. Sabina Seja alisema Rushwa ya ngono ni kosa chini ya Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007. Alisema, kifungu cha saba cha sheria hiyo kinaipa TAKUKURU mamlaka ya kufanya Kufanya uchambuzi na utafiti wa mifumo ya utendaji ili kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna bora ya kuiziba na kwamba jukumu hilo ndilo lililoiwezesha TAKUKURU kufanya tathmini ya maeneo hatarishi yanayochochea rushwa ya ngono katika Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari ambayo taarifa yake imeletwa kwa wadau husika kwa lengo la kujadiliana na kuiwekea mikakati ya kuiziba mianya iliyobainishwa.
Wadau waliohudhuria warsha hii ni pamoja na washiriki kutoka TAKUKURU; Wizara ya Elimu; Tume ya Utumishi ya Walimu; Ofisi ya Rais TAMISEMI; Chama cha Walimu; Mdhibiti Ubora; Maafisa Elimu wa Msingi, Sekondari na Halmashauri ya Jiji pamoja na Walimu.
Wakati wa majadiliano, pamoja na mambo mengine, Wadau hawa walipendekeza yafuatayo kama sehemu ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainishwa:-
- Matumizi ya TEHAMA,
- Kuangalia maeneo ambayo yanapelekea uwepo wa mianya ya rushwa ya ngono na kuiziba mianya hiyo,
- Kuendelea kutoa elimu na kujenga ujasiri kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Warsha hii ya siku moja ilihitimishwa na Bw. Oscar Msalila – Kamishna wa Elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI.