TAKUKURU YAWAPIGA MSASA MAAFISA WAKE KWA MAFUNZO YA UFUATILIAJI WA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi. Neema Mwakalyelye, amewataka maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kuimiliki ajenda ya Serikali ambayo ni ‘USTAWI WA JAMII YA WATANZANIA’, kwa kuhakikisha kwamba wanafuatilia kwa makini matumizi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

“Sote tunafahamu kwamba msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo… hivyo sisi kama TAKUKURU ni lazima tuwe na jicho la ziada katika kufuatilia utekelezaji wa miradi hii kwa lengo la kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo na malengo yaliyokusudiwa na Serikali yanatimia”.

Naibu Mkurugenzi Mkuu ameyasema hayo Agosti 8, 2022, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo kwa Maafisa wa TAKUKURU kutoka Mikoa ya Katavi, Lindi na Njombe. Mafunzo hayo yanafanyika jijini Dodoma kwa ushirikiano na Shirika la Ujerumani la Konrad Adenauer Stiftung (KAS), ambapo wawezeshaji ni kutoka TAKUKURU pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa TAKUKURU Bi. Sabina Seja alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo maafisa hao wa TAKUKURU, ambao katika vituo wanavyotoka wanahusika na jukumu la kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma (Public Expenditure Surveys), katika miradi ya maendeleo. Amesema jukumu hili la TAKUKURU la ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma, linawawezesha kubaini mapema ni wapi kuna mianya ya rushwa na hivyo kuchukua hatua za haraka za kuiziba mianya hiyo na hivyo kuokoa fedha za Serikali.

Bi. Sabina ameeleza kuwa maafisa wanaopatiwa elimu, wanatarajiwa wakirudi katika vituo vyao, wakawawezeshe maafisa wanaohusika na usimamizi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri, ili waifuatilie na kuisimamia vyema miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Ameeleza pia kuwa, ndiyo maana wamewashirikisha Wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ili wawapitishe katika utaratibu na mtiririko wa rasilimali, usimamizi wa miradi ya maendeleo unavyofanyika katika ngazi ya Halmashauri pamoja na kufahamu namna ambavyo udhibiti wa ubora katika miradi hiyo kwa ngazi ya halmashauri, unafanyika.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa KAS Bw. Damas Nderumaki amesema KAS kama Shirika lisilo la Kiserikali, inashirikiana na TAKUKURU kwakuwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007, ni wajibu wa kila mdau kushirikiana na Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini. Amesema KAS ina ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1964 na ushirikiano huo upo katika nyanja nyingi ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa.

Taarifa kwa Umma