Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye Juni 20, 2022, amefungua mafunzo kuhusu ‘Cyber Forensic’, yanayofanyika Jijini Dodoma kwa ufadhili wa SADC Anti- Corruption Committee (SACC).
Kupitia mafunzo haya yatakayofanyika kwa wiki moja hadi Juni 24, 2022, watumishi 25 wa TAKUKURU wamepata fursa ya kushiriki ambapo wawezeshaji wa mafunzo ni kutoka TAKUKURU (Bw. Charles Makindi) na kutoka Taasisi ya kuzuia rushwa Botswana – DCEC (Ms. Virginia Sekgwthe).
Akifungua mafunzo haya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu ameshukuru kwa ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na SACC ikiwa ni pamoja na kutoa pongezi kwa utaratibu wa mafunzo uliotumiwa na SADC katika kuyaendesha mafunzo haya. Amesema utaratibu wa kufanya mafunzo haya Tanzania na kuwa moja kati ya nchi 5 zilizochaguliwa kati ya nchi wanachama, umewezesha maafisa wengi wa TAKUKURU kuhudhuria mafunzo haya. Amewataka watumishi wa TAKUKURU waliopata fursa hii waitumie ipasavyo kwa manufaa yao na ya Taasisi kwa ujumla.