- UTANGULIZI
Ndugu wanahabari,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke tumeendelea kutekeleza majukumu yetu kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11 ya Mwaka 2007. Katika utekelezaji wa majukumu yetu tumeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya Rushwa wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla. Aidha majukumu haya yametekelezwa Mkoani pamoja na wilaya iliyoko chini ya Mkoa wa Temeke ambayo ni Kigamboni.
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu yaani kuanzia tarehe 1/10/2021 hadi 31/12/2021, TAKUKURU Mkoa wa Temeke tumeweza kufanya kazi mbalimbali kama ifuatavyo;
- UZUIAJI RUSHWA
Ndugu wanahabari,
Mojawapo ya majukumu ya TAKUKURU ni kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo (PETS). Lengo kuu la ufuatiliaji huu ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha inapatikana kwa kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wa rasilimali katika utekelezaji wake.
Pia ufuatiliaji huu huweza kubainisha mapema mianya ya rushwa, ucheleweshaji, uchepushaji au uvujaji, ushirikishwaji wa wananchi au wadau na hatimaye kupelekea hatua za haraka kuchukuliwa kwa miradi itakayobainika kuwa na mapungufu mbalimbali kama vile kuanzisha uchunguzi, kutoa elimu kwa umma na kufanya chambuzi za mifumo. Kwa kufanya haya, inasaidia miradi inayotekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa au kutumika katika mradi husika.
Ufuatiliaji huu hufanyika kwa kufuatilia mtiririko wa fedha kutoka chanzo (Hazina, Wafadhili au Vyanzo vya ndani) mpaka kwenye mradi husika, ili kubaini yaliyotajwa hapo juu. Aidha katika kutekeleza jukumu hili tumekuwa tukifanya ufuatiliaji na uchambuzi wa mifumo na kasha kushauri namna bora ya kufanya ili kuondoa mianya ya rushwa mahali pa kazi.
Ndugu wanahabari,
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu, katika jukumu la Uzuiaji Rushwa tumeweza kufanya uchambuzi wa mifumo mitatu (3) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Temeke ambayo ni uchambuzi wa mfumo wa utendaji kazi wa wakala wa Huduma ya ununuzi Serikalini, uchambuzi wa mfumo wa vihatarishi vya rushwa ya Ngono katika Sekta ya Elimu, Halmashauri ya Temeke, na Halmashauri ya Kigamboni.
Aidha tumefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo minne (4) ya utekelezaji wa miradi katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni nne milioni mia moja ishirini na nne mia tisa arobaini na tano elfu mia moja themanini na saba na senti Sabini na tatu (Shs 4,124,945,187.73)
Miradi tuliyofuatilia ni miradi ya ujenzi wa madarasa (157) katika Halmashauri ya Temeke na ujenzi wa madarasa (38) na Bweni moja (1) katika Halmashauri ya Kigamboni. Aidha uchambuzi huu na ufuatiliaji ulilenga katika kuthibitisha thamani ya fedha (Value for Money) katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kubaini mianya ya rushwa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kushauri namna ya kuziba mianya hiyo. Hata hivyo TAKUKURU tumefanya kikao cha pamoja (warsha) na wadau kujadili namna bora ya kuziba mianya ya rushwa katika usimamizi wa mitihani katika vyuo vya kati na kuweka maazimio ya namna ya utekelezaji katika Halmashauri ya Kigamboni.
Kazi hii ya uzuiaji rushwa kama ilivyo kwa kazi zingine imefanyika wilayani Kigamboni na Mkoani Temeke. Aidha katika miradi iliyofanyiwa ufuatiliaji, miradi iliyobainika kuwa na mapungufu imeanza kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna ubadhilifu wa fedha na kisha hatua za kisheria zitachukuliwa.
Ndugu wana habari,
2.2. USHIRIKIANO NA WADAU
2.2.1 Skauti
Mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu na hivyo katika kuhakikisha kuwa jamii nzima na makundi mbalimbali ya watanzania yanashiriki kikamilifu katika mapambano haya, TAKUKURU Mkoa wa Temeke tumeimarisha ushirikiano baina yetu na Chama cha Skauti Tanzania
Kama mnavyofahamu, Chama cha Skauti Tanzania ni chama cha hiari cha kielimu chenye wajibu wa kumlea na kumkuza kijana kiimani, kiakili, kijamii na kimwili kwa kutumia shughuli za Skauti ili kujenga dunia iliyobora zaidi – hivyo ushirikiano na chama hiki utatusaidia sana katika kujenga jamii yenye watu waadilifu.
Aidha kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Tanzania, malengo yetu ni kutumia chama hiki katika kutoa elimu kwa vijana kupitia vijana wenzao wa Skauti na kwa bahati nzuri tayari tumeweza kufungua Klabu ya wapinga rushwa ya wanachama wa Skauti hapa mkoani Temeke. Hivyo ni imani yetu kuwa kwa kukuza ushirikiano na chama hiki, tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi walioko mashuleni na walioko mtaani ambao ni rahisi kufikiwa na vijana wenzao wa Skauti.
2.2.2 Wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo
Sanjari na kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Tanzania, pia tumeendelea kuimarisha ushirikiano na kundi la vijana hasa wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo kupitia kufungua na kuimarisha Klabu za wapinga rushwa mashuleni.
Kwa sasa tuna klabu za wapinga rushwa takribani katika shule zote za Msingi, Sekondari na Vyuo vilivyoko katika Mkoa wetu. Klabu hizi zimekuwa zikitusaidia sana kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na uadilifu kwa vijana tukiamini kuwa kundi hili ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya Rushwa na kwamba vijana wakilelewa katika misingi ya uadilifu tutapata viongozi bora wa Taifa la kesho.
Tumelenga sana kushughulika na kundi la vijana kwani tunaamini vijana ni hazina na rasilimali muhimu ya taifa na chachu ya maendeleo.
2.2.3 Wana habari
Kama mnavyofahamu kuwa madhara ya rushwa huikumba jamii nzima hivyo katika kuhakikisha kuwa tunafanikiwa, tumeendelea kukukuza ushirikiano na makundi ya wadau wa mapambano dhidi ya rushwa katika Mkoa wetu. Kundi mojawapo ambalo tumekuwa tukishirikiana nalo kwa ukaribu ni kundi la wanahabari na hii imetusaidia sana katika kufikisha ujumbe wetu wa mapambano dhidi ya rushwa kwa wana Temeke na jamii nzima.
Aidha katika kuhakikisha ushirikano huu unaimarika, tayari tumefungua kundi la Whatsaap la wanahabari ambalo tunalitumia katika kupashana Habari. Hivyo basi ni imani yetu kuwa kupitia kikundi hiki mtatusaidia sana katika kufikisha ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa kwa jamii kwa kutumia taaluma na kalamu zenu.
2.2.4 Idara zingine za Serikali na makundi mengine
Pamoja na kushirikiana na wanahabari vilevile tumekuwa tukishirikiana sana na idara na ofisi mbalimbali za umma na binafsi, ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, pamoja na ofisi za wakuu wa wilaya. Tumekuwa vilevile tukishirikiana na vyama vya siasa pamoja na Idara ya Mahakama. Lengo la kukuza ushirikano huu ni kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwa mapambano haya yanahitaji nguvu ya pamoja na jukumu la kupambana na rushwa na la kila mmoja wetu.
- UCHUNGUZI
Ndugu wanahabari,
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu, tumeweza kupokea jumla ya malalamiko mia moja na hamsini na tano (155). Kati ya malalamiko hayo, malalamiko tisini na sita (96) yalihusu rushwa na malalamiko hamsini na tisa (59) yalikuwa ni malalamiko yasiyohusu rushwa. Kati ya malalamiko hamsini na tisa 59 ambayo hayakuhusu rushwa, malalamiko hamsini na nne (54) watoa taarifa wake walielimishwa na kushauriwa na malalamiko matano (5) yalihamishiwa idara nyingine.
Malalamiko tisini na sita (96) yaliyohusu rushwa, uchunguzi umeanzishwa ambapo kati yake – majalada saba (7) uchunguzi wake umekamilika, majalada kumi na moja (11) yamefungwa kwa kukosa ushahidi na majalada sabini na nane (78), uchunguzi wake bado unaendelea.
Aidha Idara zinazolalamikiwa kutokana na taarifa 155 zilizopokelewa ni kama ifuatavyo: – Taarifa 84 ni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke pamoja na Kigamboni. Maeneo yanayolalamikiwa kupitia taarifa hizi 84 yanahusu sekta ya Afya 25, Elimu 8, Ardhi 20, na Watendaji wa Kata 08, Maendeleo ya Jamii 12, Ugavi 6, Tehama 3 na Mipango 2.
Taarifa zingine 71 zilihusu TARURA 1, TAASISI ZA KIFEDHA 4, TANROAD 1, Watu binafsi 35, TFF 2, TAZARA 2, Polisi 9, MSD 2, TANESCO 1, UHAMIHAJI 1, UVUVI 1, RITA 1, BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU 2, MAHAKAMA 4, MAWASILIANO 3, NHIF 1, na Idara ya KAZI 1.
Vilevile katika kipindi hiki tuna jumla ya mashauri ishirini na mbili (22) yanayoendelea kusikilizwa mahakamani mkoani Temeke.
- UELIMISHAJI UMMA
Ndugu wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Temeke tunaamini kuwa elimu ni tendo au uzoefu wenye athari katika akili, maarifa au maumbile ya mwanadamu na kwamba ni nyenzo muhimu katika kupitisha maarifa na maadili kutoka katika kundi moja kwenda kundi jingine, au kutoka katika kizazi kimoja kwenda kingine au kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Hivyo, ili kuongeza uelewa wa wana Temeke katika mapambano dhidi ya rushwa msisitizo wetu umekuwa katika kutoa elimu katika makundi mbalimbali yenye kuhamasisha wananchi kutambua madhara ya rushwa, pamoja na namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika maeneo ya kazi na biashara, lengo likiwa ni kuifanya jamii ifahamu maana ya rushwa, vyanzo vyake na madhara yake katika jamii na kushiriki kikamilifu katika mapambano haya.
Katika kuhakikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa inawafikia watu wengi hapa mkoani Temeke, TAKUKURU mkoa wa Temeke imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia.
- Vyombo vya Habari: Katika mkoa wetu tumeweza kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja kwa kuelimisha kupitia vyombo vya Habari kimoja (1). Aidha sanjari na Radio, TV na Magazeti pia tumekuwa tukielimisha kupitia mitandao ya kijamii.
- Semina: Tumekuwa tukielimisha umma kupitia semina na tumekuwa tukifanya na kushiriki semina katika ofisi za umma na binafsi. Katika kipindi cha miezi mitatu tumeweza kufanya semina kumi na saba (17).
- Mikutano ya hadhara: Njia hii imekuwa ikitusaidia katika uelimishaji ikiwa ni pamoja na kutumia utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA ambapo tumekuwa tukiwafuata wananchi na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali kama Masoko, Magulio, Zahanati na vituo vya afya pamoja na Vituo vya mabasi (Stendi).Kupitia utaratibu huu tumeweza kufanya mikutano ya hadhara thelasini na nne (34).
- Kushiriki maonyesho: Tumekuwa tukishiriki katika maonyesho mbalimbali hasa katika vituo vya afya mwaka 2021, pamoja na ya magulioni na kuweza kufikisha ujumbe wetu ambapo tumeweza kushiriki maonyesho matatu (3) katika kipindi cha miezi mitatu.
- Kuelimisha jamii kupitia uandishi wa makala mbili (2) mbalimbali zenye maudhui ya kukemea vitendo vya Rushwa.
- Kutoa taarifa moja (1) kwa vyombo vya Habari kuhusu kazi mbalimbali zifanywazo na TAKUKURU mkoa wa Temeke.
- Kuimarisha klabu za wapinga rushwa kumi na moja (11) na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao, kuichukia rushwa na kuwa jasiri katika kutoa taarifa zinazohusu vitendo vya rushwa.
5. USHUGHULIKIAJI WA KERO ZA RUSHWA KWA WANANCHI.
Kupitia utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA tumeweza kusikiliza kero za wananchi katika maeneo mbalimbali na kutatua kero hizo na maeneo yaliyoweza kufikiwa ni Zahanati, Vituo vya afya, pamoja na Magulioni. Katika usikilizaji wa kero hizo baadhi ya kero zilizokuwa ni malalamiko ya Rushwa ambapo wanananchi walishauriwa kufika ofisini na kero zingine zilitatuliwa palepale.
Uanzishwaji wa TAKUKURU INAYOTEMBEA, lengo lake ni kuwafikia wananchi sehemu walipo kwa lengo la kusikiliza kero walizonazo na kuzitolea majibu. Pamoja na kusikiliza kero utaratibu huu umesaidia zaidi katika kutuweka karibu na wananchi na imekuza ushirikiano baina yetu na wananchi hususan wakazi wa Mkoa wa Temeke.
6 VIPAUMBELE KWA KIPINDI CHA JANUARI – MACHI, 2022
Pamoja na utekezaji wa majukumu yetu ya kawaida pia tumejiwekea malengo ya kutekeleza vipaumbele vifuatavyo: –
- Kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika Ujenzi wa miradi ya maendeleo ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi.
Pia kama mtakumbuka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano Mkuu maalum wa ALAT Septemba 27, 2021 jijini Dodoma alisema.
Ninanukuu“Bado kuna shida kwenye thamani ya fedha Kwa miradi mnayoitekeleza, fedha nyingi zinakuja kwenu lakini miradi haifanani na fedha zinazotolewa. Pamoja na kwamba tutaendelea kuleta fedha naagiza thamani ya fedha katika miradi tunayoitekeleza ionekane.”Mwisho wa kunukuu.
Kauli hii imetuongezea ari na kasi ya ufuatiliaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Pia tumeendelea kuweka kipaumbele katika chunguzi za fedha za ndani za manispaa hususani tumejipanga kuongeza kasi katika kufatilia ubadhilifu katika makusanyo ya fedha za ndani za Halmashari kupitia utaratibu wa POS, pamoja na kufanya chunguzi katika miradi ya Ujenzi wa Madarasa, Afya, Miundo mbinu ya Maji na matumizi 10%, fedha ambazo Serikali hurudisha katika Halmashauri kwa ajili ya kusaidia makundi ya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwani kumekuwepo na malalamiko ya ufujaji wa fedha hizi Pamoja na vya vya Michezo.
- Kuongeza kasi ya uelimishaji umma kwa kutumia njia mbalimbali mfano kushiriki katika maonyesho kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania, Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru na matamasha ya uelimishaji, semina, mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi, kuimarisha klabu za wapinga rushwa mashuleni pamoja na kuendelea kufungua klabu za wapinga rushwa katika shule zitakazopata usajili mpya. Vilevile kutoa elimu kwa viongozi wa dini ili katika mahubiri yao waendelee kukemia vitendo dhidi ya rushwa.
- Kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi kama maeneo ya utoaji wa huduma kwa wananchi na katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa katika miradi ya Sekta ya Elimu, Ujenzi, Ununuzi, Afya, uchukuzi.
- HITIMISHO
Ndugu wanahabari,
Mapambano dhidi ya rushwa ni ya kila mwana Temeke, hivyo ili kuufanya Mkoa wa Temeke kuwa sehemu nzuri ya kuishi isiyokuwa na rushwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mapambano haya. Hivyo ninawaomba wana Temeke wote tuendeleee kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja na tuwe mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na tuendelee kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Aidha nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wana Temeke wote ambao wamekuwa na wanaendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa kutoa taarifa ambazo zimekuwa zikifanikisha kuwabaini wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na hatimaye hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Kila mmoja wetu anahitaji kutanguliza maslahi ya nchi na kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na tatizo la rushwa katika Mkoa wetu.
Vilevile, tukumbuke kwamba Rushwa ni adui wa haki na inaweza kuathiri mgawanyo wa rasilimali katika jamii na kusababisha wananchi kukata tamaa. Hivyo ni wajibu wa kila MwanaTemeke kuchukua hatua ya kutoa taarifa TAKUKURU, pale anapoona kuna dalili ya vitendo vya rushwa kufanyika.
Imetolewa na: –
CHRISTOPHER MYAVA
MKUU WA TAKUKURU (M)Simu: 0738 15023