UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU MKOA WA TANGA KWA KIPINDI CHA OKTOBA HADI DISEMBA 2021
Ndugu wanahabari,
Ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninawakaribisheni tena katika ofisi ya TAKUKURU (M) Tanga. Kwa kutambua umuhimu wenu, tumewaita leo ili kupitia kwenu tuweze kuuhabarisha umma kuhusu utendaji kazi wa ofisi yetu. Karibuni sana.
Ndugu wanahabari,
Kama ulivyo utaratibu wetu, tumemaliza robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 hivyo nimewaita ili nizungumze na wananchi wa Mkoa wa Tanga na Watanzania kwa ujumla, kwa lengo la kuuhabarisha umma juu ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha Oktoba – Disemba 2021.
Ndugu wanahabari,
Kwa mujibu wa ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake, ikisomwa, pamoja na kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007, TAKUKURU ina wajibu wa kushirikisha raia katika kazi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na pia kuwapa raia taarifa wakati wote, kuhusu shughuli zinazohusu harakati za mapambano dhidi ya Rushwa.
Kwa umuhimu huo, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, tunapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya utekelezaji wa majukumu yetu kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba 2021 hadi Disemba 2021), katika maeneo ya Uchunguzi na Mashitaka, Ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo, udhibiti wa mianya ya rushwa pamoja na Elimu kwa Umma kama ifuatavyo:
Ndugu wanahabari,
UCHUNGUZI:
Katika jukumu la Kuchunguza tuhuma au makosa ya Rushwa pamoja na njama za kutendeka kwa makosa hayo, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imepokea jumla ya taarifa 174 na kati ya taarifa hizo, 95 ni za vitendo vya rushwa na taarifa 79 si taarifa za vitendo vya rushwa. Kati ya taarifa 95 za vitendo vya rushwa, taarifa 80 zinaendelea kuchunguzwa, taarifa 11 zimefungwa kwa kukosekana kwa ushahidi, taarifa 01 imehamishiwa idara nyingine, taarifa 01 imeshuhulikiwa na kukamilika kwa kufanya udhibiti na taarifa 02 watoa taarifa walishauriwa namna watakavyoweza kupata haki zao.
Kati ya taarifa 79 ambazo hazikuwa za vitendo vya rushwa, taarifa 76 watoa taarifa walielimishwa na kushauriwa namna mbadala ya kutatua kero zao na taarifa 03 zimehamishiwa idara zingine kwa hatua zaidi.
Mchanganuo wa taarifa hizo 174 za malalamiko – kisekta ni kama ifuatavyo: Serikali za Mitaa 62, Mahakama 12, Taarifa za watu Binafsi 23, Elimu 14, Afya 11, TAMISEMI 16, Majeshi ya Ulinzi na Usalama 10, Kilimo 03, Nishati na Madini 02, Maji 01, Misitu 01, Mashirika ya Umma 07, Biashara na Viwanda 02, Vyama vya Ushirika 02, Mashirika Binafsi 03 na Usafirishaji 05.
Ndugu wanahabari,
Kifungu cha 7 (e) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, kinaitaka TAKUKURU kuchunguza na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka, kufungua kesi mahakamani chini ya sheria hiyo na makosa mengine yanayohusisha Rushwa. Katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeendesha jumla ya kesi 34 mahakamani. Mashauri 28 yalifunguliwa kabla ya robo ya pili kuanza na mashauri 06 yamefunguliwa ndani ya robo ya pili ya mwaka 2021/2022. Vilevile, katika kipindi husika tulishinda kesi 4 zilizotolewa hukumu mahakamani.
Ndugu wanahabari,
Kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007, TAKUKURU ina wajibu wa kuchukua hatua muhimu katika kuzuia na kupambana na rushwa katika jamii, Taasisi za Umma na katika Sekta Binafsi. Sisi Maafisa wa TAKUKURU tunatakiwa kufuatilia na kuchunguza shughuli na taratibu za jamii, Taasisi za Umma na Binafsi, ili kuwezesha kufanya ugunduzi wa mianya ya vitendo vya rushwa na kushauri namna bora ya kuzuia rushwa kwa kujaribu kupitia upya taratibu za utoaji huduma na au taratibu za kazi ili kuona namna ya kuweka mifumo madhubuti na imara inayoweza kuchangia katika ufanisi na uwazi wa taasisi husika.
Katika utekelezaji wa jukumu hili, TAKUKURU Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2021 tumefanya kazi za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo 29 yenye thamani ya jumla ya sh. 4,363,323,503.16/= kwenye Sekta za Elimu na Afya. Katika ufuatiliaji huo, wilaya zote zilifuatilia fedha za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utoaji chanjo ya UVIKO 19.
Pia ulifanyika ufuatiliaji wa ujenzi wa madarasa na zahanati unaotekelezwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19.Aidha kwa mkoa wa Tanga Serikali ilitoa fedha kiasi cha shs. 9,900,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 495.
Baadhi ya mapungufu tuliyoyabaini tumewafahamisha mamlaka husika na tayari marekebisho yameanza kufanyika.
Pia kuna Ufuatiliaji uliofanyika wa kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika shule za wenye mahitaji maalumu katika wilaya nne za mkoa wa Tanga. Wilaya hizo ni Tanga, Muheza, Lushoto na Korogwe ambapo utekelezaji wa miradi hii bado unaendelea kwani nguvu kubwa ilikuwa imeelekezwa kwenye ujenzi wa madarasa. Kila shule imetengewa kiasi cha shilingi 80,000,000/=.
Ndugu wanahabari,
Katika kuhakikisha kuwa tunakidhi matakwa ya Kifungu cha 7 (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, TAKUKURU pia tumefanya uchambuzi wa mifumo ili kupata tija ya mifumo imara isiyokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Katika utekelezaji wa jukumu hili, chambuzi 10 za mifumo zimefanywa na TAKUKURU Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2021, katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa uwepo wa rushwa ya ngono katika Sekta ya Elimu. Kazi hii imefanyika katika wilaya zote za mkoani Tanga, kwa sababu hii ni kazi ya kitaifa.Aidha zimefanyika warsha 05 kwa kipindi tajwa.
Ndugu waandishi wa Habari,
TAKUKURU (M) Tanga hatuishii tu katika kufanya uchambuzi wa mifumo, kufanya warsha na kuweka maazimio peke yake, bali tunafanya pia ufuatiliaji ili kujiridhisha iwapo maazimio tuliyoyaweka yanatekelezwa ipasavyo.
Ndugu wanahabari,
Kifungu cha 7 (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, kinaitaka TAKUKURU kuhimiza na kuendeleza uungaji mkono wa jamii katika kupambana na vitendo vya Rushwa. Sisi tunatekeleza jukumu hili kwa kuelimisha na kushirikisha wadau na umma kwa ujumla katika mapambano dhidi ya rushwa.
Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imefanya jumla ya semina 53 kwa makundi ya watumishi wa umma pamoja na wadau wengine. Pia tumefanya mikutano ya hadhara 36 kwa wananchi katika vijiji na mitaa mbalimbali, vipindi vya redio 15 na maonesho 05. Lakini pia tumeandika Habari na Makala 06 kwa ajili ya Jarida la TAKUKURU, sambamba na kutoa taarifa 1 kwa umma kupitia ninyi waandishi wa habari. Kwa upande wa elimu na hamasa kwa wanafunzi na vijana, tumeimarisha jumla ya klabu 86 katika shule na vyuo mbalimbali hapa mkoani Tanga.
Kupitia utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeweza kuwafikia wananchi katika kata ya USAGARA ili kufahamu kero zao na maoni yao juu ya utendaji kazi wa TAKUKURU katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru. Vile vile TAKUKURU INAYOTEMBEA iliwafikia wananchi katika kata ya MNYANJANI na kata ya MZINGANI. Kupitia utaratibu huu tumeweza kutatua changamoto nyingi pamoja na kuwapa elimu wananchi wetu.
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Tanga iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa nikuwajenga vijana katika misiki ya Uzalendo, Uwajibikaji na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
Ndugu wanahabari,
SUCCESS STORY (JAMBO LA MAFANIKIO).
Kutokana na uwepo wa tatizo kubwa katika maswala ya Ardhi katika Mkoa wa Tanga, TAKUKURU INAYOTEMBEA ilishirikiana na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Tanga ambapo kwa pamoja tulikutana na wananchi na kuwapatia elimu ya masuala ya Ardhi pamoja na madhara ya na Elimu ya Rushwa. Suala hili lilifanikiwa sana kwani wananchi walielewa kuwa kumbe sio kila mgogoro wa Ardhi unasababishwa na uwepo wa Rushwa lakini pia walifahamu njia bora za kutatua migogoro ya ardhi na kwamba ni mgogoro upi una viashiria vya Rushwa hivyo uwasilishwe TAKUKURU.
Ndugu wanahabari,
MIKAKATI YA KIPINDI CHA JANUARI – MACHI 2022, ni kama ifauatavyo:
Mkakati wetu kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022 ni kufanya kazi kwa juhudi, weledi na utashi wa hali ya juu, huku tukijielekeza zaidi katika KUZUIA RUSHWA. Hii ni pamoja na Ufuatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Udhibiti wa mianya ya Rushwa pamoja na uelimishaji wa jamii hususan kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU na Chama cha Skauti nchini – TAKUSKA.
Ndugu wanahabari,
HITIMISHO:
Niwaombe sana wakazi wa Mkoa wa Tanga na wadau wote kwa ujumla kupitia ninyi waandishi wa habari, kuendelea kutupa ushirikiano wakati wote katika mapambano dhidi ya Rushwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu tulilopewa wote kwa mujibu wa Kifungu cha 39 (1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007. Kifungu hiki kinatamka wazi kwamba kila mtu ambaye ana taarifa juu ya mtu kutenda kosa au kusudio la mtu kutenda kosa chini ya sheria hii, awe anafahamu kabla au baada ya kosa kutendwa, anatakiwa kutoa taarifa TAKUKURU. Hivyo basi Kwa yeyote mwenye taarifa inayohusu vitendo vya rushwa asisite kufika katika ofisi yetu ya mkoa iliyopo BOMBO AREA karibu na HARBOURS CLUB na kwa wale waishio wilayani wasisite kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo katika Wilaya husika.
Pia mnaweza kupiga simu ya dharura namba 113 au ukatuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kupiga *113# na kufuata maelekezo. Huduma hii ni BURE.
Ninaomba niwakumbushe kuwa hii vita ni yetu sote na kwa pamoja tunaweza kuishinda.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Zainabu Bakari
MKUU WA TAKUKURU (M) TANGASimu 0738150225