TAKUKURU Mkoa wa Tabora kwa kipindi cha Oktoba 2021 hadi Disemba 2021 imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 7.
Utekelezaji wa majukumu hayo umefanyika kwa kuendelea kufanyia kazi malengo tuliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika madawati ya Uchunguzi, Elimu Kwa Umma na Uzuiaji Rushwa.
ELIMU KWA UMMA
Katika upande wa kuelimisha jamii ili ishiriki kivitendo katika mapambano dhidi ya rushwa, elimu ilitolewa kwa makundi mbalimbali ikiwemo klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo, watumishi wa umma na mashirika ya Serikali nayo yalielimishwa kuhusu madhara ya rushwa na namna ambayo wanapaswa kupambana nayo.
Kazi ambazo zimefanyika ni pamoja na:-
- Semina16,
- Uandaaji wa makala 05,
- Mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi 17,
- Utoaji wa habari na vipindi redioni 03.
- Kuimarisha na kufungua klabu za wapinga rushwa 57.
- Onesho 1 lilifanyika
TAKUKURU INAYOTEMBEA
Pia TAKUKURU Mkoa wa TABORA imeendelea kutekeleza utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kupitia mpango wa TAKUKURU INAYOTEMBEA (TAKUKURU MOBILE) wenye lengo la kuwafikia wananchi kwa wingi zaidi, kusikiliza kero zao na kuzitatua. Kwa kipindi cha Oktoba 2021 mpaka Disemba 2021 TAKUKURU Mkoa wa Tabora umezifikia jumla ya kata 3 na kutatua kero mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo kero katika Ardhi, Mahakama, Polisi, Afya, Huduma za kifedha na Ushirika.
Ofisi imeweza kutembelea na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Loya ili kusikiliza kero zao ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa zinahusiana na ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara ya Mabeshi – Loya. Ofisi ilifanikiwa kukutana na mkandarasi anayejenga barabara hiyo na kukubaliana kazi za kukamilisha ili kuondoa kero kwenye barabara hiyo.
USHIRIKIANO WA TAKUKURU NA SKAUTI
Katika kuboresha juhudi za uelimishaji umma ndani ya jamii TAKUKURU imefanya ushirikiano na SKAUTI Tanzania kupitia umoja wa TAKUSKA wenye lengo la kufanya uelimishaji umma kuhusiana na mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwatumia vijana wa SKAUTI ili kuhakikisha elimu hii inafika mbali zaidi ndani ya jamii.
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Tabora iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Mwongozo huu umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa nikuwajenga vijana katika misingi ya Uzalendo, Uwajibikaji na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
SUCCESS STORY
TAKUKURU Mkoa wa Tabora ilishiriki kwenye maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania kwa kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Nzega iliyopo katika Wilaya ya Nzega ambapo watumishi walipeleka mahitaji mbalimbali katika wodi ya mama na mtoto na kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa watumishi wa Hospitali hiyo.
Pia Katika wilaya ya Igunga, TAKUKURU ilifanikiwa kutoa elimu ya Manunuzi kwa Shule za sekondari kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali Wilayani Igunga, miradi ambayo imetekelezwa kwa kutumia fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19. Baadhi ya shule ambazo zilifanikiwa kupewa elimu hiyo na kukamilisha miradi hiyo kama ilivyotakiwa ni Pamoja na Shule za Sekondari Nanga, Nkinga,Simbo,Mbutu na Mwamashimba
UZUIAJI RUSHWA
Dawati la uzuiaji rushwa lina majukumu makuu mawili ambayo ni ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na uchambuzi wa mifumo. Majukumu yote haya mawili yana lengo la kuweza kubaini uwepo wa viashiria au vitendo vya rushwa ili kuweza kuchunguza au kushauri mamlaka husika namna bora ya kuziba mianya ya rushwa.
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba 2021 TAKUKURU Mkoa wa Tabora imeendelea kufanya kazi za uchambuzi, warsha na utekelezaji wa maazimio na kuhakikisha kuwa wadau wanatekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika vikao vya makubaliano. Uchambuzi uliofanyika umehusisha maeneo yafuatayo
- Kubaini viashiria vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu.
- Ufanisi wa vijiji katika kukusanya ushuru wa madini kwenye migodi iliyopo maeneo ya wananchi.
Baadhi ya mapungufu tuliyoyabaini katika uchambuzi huo tumewafahamisha mamlaka husika na tayari marekebisho yameanza kufanyika.
Aidha, katika eneo la ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Tabora imeshiriki katika ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa kwa fedha za UVIKO -19 ambapo miradi yenye thamani shilingi 14,674,000,000 imefuatiliwa miradi hiyo imehusisha ujenzi wa madarasa kwenye shule shikizi uliogarimu shilingi 1,264,000,000 na ujenzi wa madarasa kwenye shule za kawaida msingi na sekondari uliogarimu shilingi 13,410,000,000. Ukaguzi uliofanyika umebaini kukamilika kwa miradi hiyo kwa zaidi ya 80% na baadhi ya madarasa yameshaanza kutumika wakati mengine yakiwa kwenye hatua za mwisho za kukamilika.
UCHUNGUZI NA MASHTAKA
Katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Tabora imepokea jumla ya malalamiko 62 ambayo kati yake 26 yalikua na viashiria vya Rushwa na 36, hayakua na viashiria vya Rushwa. Kati ya Malalamiko yaliyowasilishwa, Malamiko 04 yalitoka sekta ya maji, Elimu 08, Tamisemi 39, Ardhi 05, Polisi 01, Afya 05,
Kati ya malalamiko hayo 36 ambayo hayakuhusu Rushwa, watoa taarifa 21 walipewa ushauri kulingana na malalamiko yao na malalamiko 15 yalihamishiwa kwenye idara zingine kwa ufatiliaji zaidi. Pia katika dawati la uchunguzi kazi zifuatazo zilifanyika:
- Tumekamilisha majalada ya uchunguzi matatu (03)
- Tumefungua kesi mpya saba (7) Mahakamani
- Majalada matatu (03) yalipata kibali cha DPP
- Kesi mbili (2) zimetolewa maamuzi na kushinda
- Jumla ya mashauri kumi na tisa (19) yanaendelea mahakamani
MIKAKATI YA JANUARI – MACHI 2022
TAKUKURU Mkoa wa Tabora itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Rushwa. Tutajikita katika kutoa elimu ya kutosha kwa taasis mbalimbali na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha wananchi sio tu wanaifahamu na kuichukia Rushwa bali kuongeza mwamko wao katika kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa vinavyojitokeza katika mazingira yao.
Pia tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Rushwa kwa kushughulikia taarifa zinazowasilishwa kwa wakati na tutaendelea kufuatilia miradi ya maendeleo na kukagua thamani ya fedha kwenye miradi hiyo.
Natoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Tabora kutokuvumilia uvunjifu wa maadili na vitendo vya Rushwa katika mazingira yao , waendelee kuleta Taarifa za matukio hayo na sisi tunaahidi kuzifanyia kazi kwa usiri na weledi wa hali ya juu.
Pia nichukue fursa hii kuwatahadharisha matapeli wanaotumia jina la TAKUKURU kuwatapeli wananchi kwa lengo la kujipatia manufaa, kuwa wanachofanya ni kosa la jinai na yeyote atakaebainika kuhusika na makosa hayo sheria itachukua mkondo wake.
Imetolewa na:
Mussa Chaulo
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Simu:0738 150 218