TAKUKURU SONGWE YADHIBITI IDARA YA AFYA
(PORT HEALTH) MPAKA WA TUNDUMA
Ndugu Wanahabari,
Ninawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nimewaita hapa siku hii ya leo kwa ajili ya kuuhabarisha umma kupitia kwenu Wanahabari, kuhusu Utendaji Kazi wa Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe kwa kipindi cha Oktoba-Disemba, 2021.
Ndugu Wanahabari,
UZUIAJI RUSHWA
Katika kipindi husika, ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe kupitia Kituo Maalumu cha TAKUKURU Tunduma, imefanya udhibiti wa mianya ya rushwa Idara ya Afya Mpaka wa Tunduma (Port Health).
Kwamba, katika Mpaka wa Tunduma, Idara ya Afya hutoa huduma ya chanjo kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia Mpaka huo wa Tunduma.
Chanjo ambazo hutolewa ni pamoja na Chanjo ya Homa ya Manjano (Yellow Fever); Homa ya Ini aina ya B (Hepatitis B); pia hupima UVIKO 19 kwa wasafiri wasio na cheti cha kipimo cha UVIKO 19; pamoja na upulizaji wa dawa ya kuuwa wadudu kwenye vyombo vya usafiri.
Huduma hizi zote ambazo zinazotolewa na Idara ya Afya Mpaka wa Tunduma zina gharama ambazo zinatakiwa kulipwa na msafiri anayeingia nchini ambaye hana cheti husika kulingana na masharti ya kuingia Nchini. Hivyo ili kuweza kupatiwa chanjo husika, msafiri atatakiwa kulipa kupitia mfumo wa GePG (“Government e-Payment Gateway System”), baada ya kuandaliwa namba ya malipo (“Control number”) ndipo aweze kupatiwa chanjo au huduma husika.
Katika udhibiti huu, ilibainika kuwa Idara ya Afya Mpaka wa Tunduma wakati mwingine hupokea fedha taslimu kutoka kwa wasafiri, badala ya kuwaandalia namba ya malipo ili wasafiri wao wenyewe walipe kwa kutumia mfumo wa GePG.
Wakati udhibiti huu ukifanyika, fedha taslimu kiasi cha Shs. 2,220,000.00 pamoja na Dola za Kimarekani 200 zilikutwa zikiwa zimepokelewa na Watumishi wa Mpaka wa Tunduma – Idara ya Afya toka kwa wasafiri ambao walipatiwa huduma mbalimbali katika Mpaka huo.
Baada ya udhibiti huu kufanyika na kukamilika, fedha kiasi cha Shs. 2,220,000.00 pamoja na Dola za Kimarekani 200 zililipwa kwa kutumia mfumo wa GePG.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na kufanya udhibiti wa Idara ya Afya Mpaka wa Tunduma, katika kipindi husika Dawati la Uzuiaji Rushwa ambalo hufanya Chambuzi za Mifumo ya Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali ikiwa na lengo la kuzuia mianya ya Rushwa inayojitokeza kwenye mifumo ya kiutendaji pamoja kutembelea na kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na wadau pamoja na wananchi ambao ndio wanufaika wa miradi husika, lilifanya kazi zifuatazo:
Tuliweza kufanya jumla ya chambuzi za mifumo mitatu katika ofisi zetu za mkoa wa Songwe. Chambuzi zilizofanyika ni pamoja na:
- Uchambuzi wa mfumo katika sekta ya Elimu ambao ulilenga kubaini Viashiria vya Rushwa ya Ngono kwa shule za Msingi na Sekondari.
Uchambuzi huu ulibaini kuwepo kwa mianya mingi ya rushwa katika sekta ya elimu ambayo inachochewa na ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma na maeneo yanayochochea rushwa hiyo ni katika upangaji wa vituo vya kazi, uhamisho wa ndani ya halmashauri pamoja na utoaji wa fursa za mafunzo ya muda mfupi na mrefu pamoja na uteuzi kufanya kazi maalum. Ofisi yetu inatarajia kufanya warsha na wadau wanaohusika na uchambuzi huu ili kujadili namna ya kuziba mianya hiyo.
- Uchambuzi wa mfumo wa mianya ya Rushwa katika mfumo wa Manunuzi ya Umma kupitia GPSA.
Uchambuzi huu umebaini kuwa taasisi nyingi za Serikali hazifanyi manunuzi kupitia Wakala wa Manunuzi ya Umma (GPSA) na kwamba ofisi yetu itafanya warsha na wadau husika ili kujadili namna ya kuziba mianya hiyo.
Vilevile, tuliweza kutembelea na kukagua utekelezaji wa jumla ya miradi ya maendeleo mitatu yenye thamani ya Shs.791,197,546 Miradi hi iimekaguliwa kwa kushirikiana na wadau husika wa miradi pamoja na wananchi ambao ndio wanufaika wa miradi husika. Miradi hiyo ilijumuisha:
- Mradi wa ujenzi barabara ya vwawa mjini kwa kiwango cha lami KM 1 yenye thamani ya Tsh. 449,285,470
- Ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za uhamasishaji wa zoezi la chanjo katika ofisi ya Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Songwe na Halmashauri ya wilaya ya Mbozi wenye thamani ya Tshs. 121,000,000/=
- Ukamilishaji wa zahanati ya Mtunduru, kata ya Magamba Wilaya ya Mbozi wenye thamani ya Shs. 50,000,000/=;
Vilevile, tuliweza kutembelea na kukagua utekelezaji wa jumla ya miradi ya maendeleo 16 iliyotokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 yenye thamani ya Shs. 840,000,000/=.
Miradi hii iimekaguliwa kwa kushirikiana na wadau husika wa miradi pamoja na wananchi ambao ndio wanufaika wa miradi husika. Miradi hiyo ilijumuisha:
- Ujenzi wa vyumba 04 vya madarasa shule ya Sekondari Muungano; Majengo; DANIDA na J.K. Nyerere wenye thamani ya Shs. 80,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa bweni shule ya msingi Kitete H/Mji Tunduma wenye Thamani ya Tsh 80,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 02 vya madarasa na Ofisi 01 katika shule za Sekondari Bubigu; Itumba; Luswiswi; Mlale; Steven Kibona; Wilaya ya Ileje wenye thamani ya Shs. 40,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa vyumba 03 vya madarasa na Ofisi 01 katika shule za Sekondari Ikinga; Ileje; Kafule na Nakalulu Wilaya ya Ileje wenye thamani ya Shs. 60,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa vyumba 03 vya madarasa na Ofisi 01 katika shule ya Sekondari Shinji Wilaya ya Ileje wenye thamani ya Shs. 80,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 02 vya madarasa na Ofisi 01 katika vituo shikizi vya Shule za Msingi za Lusungo; Mangwina; Ibandi na Ipesi Wilaya ya Ileje wenye thamani ya Shs. 40,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa vyumba 05 vya madarasa katika shule ya Sekondari Isanga na Ilolo Wilaya ya Mbozi wenye thamani ya Shs. 100,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa vyumba 03 vya madarasa katika shule ya Sekondari Ihanda Wilaya ya Mbozi wenye thamani ya Shs. 60,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 02 vya madarasa katika shule za Sekondari Hasamba na Iyula Wilaya ya Mbozi wenye thamani ya Shs. 40,000,000.00 kila mmoja
- Ujenzi wa bweni shule ya msingi Lutumbi Wilaya ya Mbozi wenye Thamani ya Tsh 80,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 05 vya madarasa katika shule ya Sekondari Sume Wilaya ya Songwe wenye thamani ya Shs. 100,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 03vya madarasa katika shule ya Sekondari Gua Wilaya ya Songwe wenye thamani ya Shs. 60,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 02 vya madarasa katika shule ya Sekondari Kapalala Wilaya ya Songwe wenye thamani ya Shs. 40,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 04 vya madarasa katika shule ya Sekondari Kapele Wilaya ya Momba wenye thamani ya Shs. 80,000,000.00
- Ujenzi wa vyumba 02 vya madarasa katika shule za Shikizi Chipumpu na Iyendwe Wilaya ya Momba wenye thamani ya Shs. 40,000,000.00 kila mmoja
Ufuatiliaji huu umebaini kuwa utekelezaji wa miradi unaendelea vema kwa kadri ilivyokusudiwa.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi husika, ofisi yetu pia iliendelea na majukumu yake mengine kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 kama ifuatavyo:
Katika Uchunguzi, ofisi yetu ilipokea jumla ya taarifa 72 za malalamiko ya uwepo wa vitendo vya rushwa. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 57 yalihusu Rushwa na malalamiko 15 hayakuhusu rushwa ambapo watoa taarifa walishauriwa. Taarifa 57 zilizohusu rushwa zilifunguliwa majalada ya kuanzisha uchunguzi ambapo taarifa 32 uchunguzi wake bado unaendelea na taarifa 22 uchunguzi wake umekamilika na kufungwa kwa kuwa haukuweza kuthibitisha tuhuma. Kuna taarifa 3 zilizohamishiwa idara nyingine.
Mchanganuo wa malalamiko hayo kisekta yaliyopokelewa ni kama ifuatavyo: Malalamiko 17 yalihusu Serikali za Vijiji na Kata; Malalamiko 15 yalihusu Sekta binafsi ; Malalamiko 10 yalihusu Idara ya Afya; malalamiko 05 yalihusu Idara ya Utawala; Malalamiko 5 yalihusu Idara ya Fedha; Malalamiko 4 yalihusu Idara ya Elimu; Malalamiko 3 yalihusu Idara ya Ardhi; Malalamiko 2 yalihusu Jeshi la Polisi; Malalamiko 2 yalihusu Idara ya Kilimo; Malalamiko 2 yalihusu Idara ya Mahakama; Malalamiko 2 yalihusu Idara ya Maji; Malalamiko 2 yalihusu Vyama vya Siasa; Malalamiko 2 yalihusu Idara ya Nishati na Madini; Lalalamiko 1 lilihusu Chama cha Ushirika; Lalalamiko 1 lilihusu Idara ya Maliasili; Lalalamiko 1 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.
Katika kipindi husika pia kesi mpya 2 zilifunguliwa mahakamani, kesi 1 iliamuliwa kwa mshitakiwa kutiwa hatiani na kesi 11 zinaendelea kusikilizwa mahakamani.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi husika Dawati la Elimu kwa Umma tuliweza kuelimisha makundi mengine ya Wanafunzi, Vijana, Watumishi wa Umma na Mamlaka nyingine za Serikali zilizoko katika Mkoa wetu pamoja na wananchi kwa ujumla.
Katika kipindi husika tumeweza kufanya Uimarishaji wa Klabu za Wapinga rushwa 84; Mikutano ya hadhara 44; Semina 32; Uandishi wa Habari 4; Kuelimisha umma kupitia vipindi vya Redio 2.
Katika kipindi husika ofisi yetu ilifanya uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya TAKUKURU na SKAUTI (TAKUSKA) uzinduzi uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na Mkuu wa TAKUKURU (M) Songwe. Katika uzinduzi wa Mpango huo washiriki pia Wajumbe Kamati ya Usalama Mkoa, Kamati ya Usalama za wilaya zote za Mkoa wa Songwe, Maafisa Elimu Mkoa na Wilaya (Msingi na Sekondari).
Pamoja na uzinduzi wa TAKUSKA tumeweza kutoa elimu kwa viongozi wa skauti Wilaya ya Mbozi pamoja na wanaskauti ambao waliweka kambi katika kijiji cha Sasanda. Elimu iliyotolewa ni pamoja na Umuhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo, Rushwa katika mitihani, Rushwa ya ngono pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa.
Katika utekelezaji wa majukumu yetu tumejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na kuhudumiwa. Utaratibu huu unafanyika kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA (TAKUKURU “Mobile Services”) ikiwa ni mbinu mahususi kabisa ili kuweza kufikia wananchi wengi na kusikiliza kero zao zinazohusiana na rushwa kwa ukaribu. Katika utekelezaji wa jukumu hili Ofisi yetu imeweza kufika na kuelimisha Wananchi wa kijiji cha Shiwinga, Kamsamba, Ndalambo, Khanga, Galula na Mbebe kutatua kero zao.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kipindi cha Januari-Machi, 2022, ofisi yetu imejipanga kutoa elimu ya rushwa kupitia vipindi vya Redio na Kuelimisha umma umuhimu wa kusimamia Miradi ya Maendeleo na Makosa ya Rushwa chini ya sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Vile vile, Ofisi yetu kwa kipindi husika imejipanga kuendelea kutekeleza Mwongozo wa TAKUSKA kama ifuatavyo;
- Ofisi ya Mkoa imejipanga kutoa Elimu ya Umuhimu wa kutoa taariza za vitendo vya Rushwa pamoja na Usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa Waratibu wa Skauti; Vijana wa Skauti; pamoja na Vijana wa Klabu za Wapinga.
- Vile vile, Kurusha kipindi kimoja hewani (kwenye radio) kuhusiana na TAKUSKA hususani katika kipengele cha umuhimu wa utoaji wa taarifa za vitendo vya Rushwa
- Ofisi yetu ya Wilaya ya Ileje imejipanga kutoa elimu ya Rushwa ya ngono pamoja na Udanganyifu katika mitihani kwa Viongozi na Waratibu wa Skauti katika wilaya husika
- Ofisi yetu ya wilaya ya Songwe imejipanga kutoa Elimu ya Rushwa ya ngono pamoja na umuhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa Waratibu wa Skauti; Walezi wa Vilabu vya Wapinga Rushwa; Vijana wa Skauti pamoja na Vijana wa Klabu za Wapinga Rushwa katika wilaya husika
- Ofisi yetu ya wilaya ya Momba imejipanga kutoa Elimu ya Rushwa ya ngono; Rushwa katika chaguzi za Kisiasa pamoja na umuhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo kwa Waratibu wa Skauti; Walezi wa Vilabu vya Wapinga Rushwa; Vijana wa Skauti pamoja na Vijana wa Klabu za Wapinga Rushwa katika wilaya husika
- Ofisi yetu ya Kituo Maalum Tunduma imejipanga kutoa elimu ya Rushwa ya ngono pamoja na Udanganyifu katika mitihani kwa Viongozi na Waratibu wa Skauti katika eneo husika.
Ndugu Wanahabari,
Nitoe wito kwa Maafisa Masuhuli wote kukusanya fedha za umma kupitia mfumo wa GePG kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma. Mfumo huu upo kwa Mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 kupitia marekebisho ya mwaka 2017 (Sura 348), na Waraka wa HAZINA Namba 3 ya Mwaka 2017.
Hivyo kwa Maafisa Masuhuli wote ambao watashindwa kukusanya Fedha za Umma kupitia mfumo wa GePG atakuwa anatenda kosa la Rushwa chini ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007. Ofisi yetu imejipanga kuwashughulikia wote ambao watakwamisha uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa kutotumia mfumo huu.
Mapambano dhidi ya Rushwa yatafanikiwa iwapo kila mmoja akitimiza wajibu wake.
Imetolewana:
Edings Mwakambonja,
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe
0738150214