Ndugu Wanahabari,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ni chombo chenye dhamana ya kusimamia Mapambano Dhidi ya Rushwa nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019. Tunakutana na ninyi waandishi ili kupitia kwenu, tuuhabarishe umma kuhusu utendaji kazi wetu kama ambavyo imekuwa ikifanyika kila robo ya mwaka. Taarifa inayowasilishwa leo, inahusu utendaji kazi wa ofisi yetu katika maeneo yote matatu yaani Uchunguzi, Elimu kwa Umma na Uzuiaji wa Vitendo vya Rushwa kwa kipindi cha Oktoba – Disemba 2021.
Ndugu Wanahabari,
Katika Dawati la Uchunguzi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Singida imetekeleza majukumu yafuatayo:-
- Jumla ya taarifa au malalamiko 101 yalipokelewa ambapo taarifa 63 zilihusu vitendo vya rushwa na taarifa 38 hazikuhusu vitendo vya rushwa.
Mchanganuo wa malalamiko hayo 101 yaliyopokelewa kisekta ni kama ifuatavyo:
TAMISEMI 44, Afya 14, Ardhi 13, Mahakama 08, Polisi 06, Elimu 04, Binafsi 03, Fedha 03, Kilimo 01, Manunuzi 01, Maliasili 01, Maji 01, Nishati 01 na Mifuko ya hifadhi ya jamii 01.
- Malalamiko 63 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na Malalamiko 38 ambayo yalibainika hayahusiani na rushwa walalamikaji walipewa ushauri na kuhamishiwa idara nyingine kwa hatua zaidi.
- Katika kipindi husika, jumla ya kesi tatu (03) zilifunguliwa Mahakamani na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa kumi na tano (15).
- Katika kipindi hiki cha Oktoba – Desemba 2021, Kesi 6 zilitolewa uamuzi mahakamani na Jamhuri ilishinda katika kesi zote.
Ndugu Wanahabari,
Elimu kwa Umma: Elimu kwa umma inafanyika ili kuielimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Elimu kwa umma pia inafanyika kwa madhumuni ya kuipa jamii uelewa na hivyo kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
TAKUKURU mkoa wa Singida kupitia Dawati la Elimu kwa Umma hutumia mbinu mbalimbali katika kuelimisha kwa kuwashirikisha wanajamii wa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana wa shule za Msingi, Sekondari, Vyuo, Watumishi wa Umma na jamii kwa ujumla.
TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Chama cha SKAUTI Tanzania, imefanikiwa kuanzisha ummoja unaojulikana kwa jina la TAKUKURU – SKAUTI [TAKUSKA]. Walezi wa ummoja huu ni Wakuu wa Mikoa kwa ngazi ya mkoa na Wakuu wa Wilaya kwa ngazi ya wilaya na mwongozo umetolewa wa mashirikiano kati ya TAKUKURU na Skauti.
Mwongozo huo ambao ni MWONGOZO WA MAFUNZO KWA WAWEZESHAJI WA KUFUNDISHIA VIJANA WA SKAUTI KUHUSU KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA, ulizinduliwa kitaifa na baadaye kutambulishwa katika ngazi ya mkoa na wilaya zote za Mkoa wa Singida. Mwongozo huu utatumika katika uelimishaji kwa lengo la kujumuisha vijana wa Skauti katika mapambano dhidi ya Rushwa.
Vilevile, kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2021, jumla ya mikutano ya hadhara 24 imefanyika, semina 32 zimefanyika, klabu za wapinga Rushwa 58 zimeimarishwa na vipindi vya Redio 02 vilirushwa kupitia Standard Radio Fm ya mkoani Singida.
Ndugu Wanahabari,
Pia TAKUKURU INAYOTEMBEA ilitembelea Chuo cha Uuguzi Kiomboi (Kiomboi School of Nursing – KNTC) kilichopo Wilaya ya Iramba kwa lengo la kuwaelimisha na kupokea kero mbalimbali kuhusu Rushwa. Kupitia uelimishaji huo, tulipokea malalamiko kwamba, baadhi ya Wanachuo wanaofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Ufadhili wa Masomo kwa watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu -CAMFED walilalamika kuwa, baada ya kuingiziwa fedha za kujikimu kwenye akaunti zao za benki, Uongozi wa chuo uliwaamuru wanachuo hao kutoa kwa uongozi wa Chuo, fedha kiasi cha Sh. 720,000/= kinyume na utaratibu wa Chuo pamoja na shirika la CAMFED. Baada ya TAKUKURU Mkoa wa Singida kupitia sheria na taratibu za chuo, ilibainika kuwa wanachuo hao hawakutakiwa kufanya hivyo na iliamuliwa kuwa kila mwanachuo aliyetoa fedha Sh. 720,000/= kwa uongozi wa chuo, basi arudishiwe fedha hizo.
Ndugu Wanahabari,
Uzuiaji Vitendo vya Rushwa ni jukumu moja wapo linalotekelezwa na TAKUKURU kwa madhumuni ya kuzuia athari ambazo jamii ingezipata kama vitendo vya rushwa vingeachwa vikatokea. Ili kudhibiti mianya ya rushwa katika Idara mbalim