SIMIYU, OKT – DES 2021

TAKUKURU SIMIYU YAFUATILIA MIRADI YA MAENDELEO YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI SABA NA MILIONI MIA MOJA TISINI NA SABA.

Ndugu Wanahabari,

Hii ni taarifa ya utendaji kazi zilizotekelezwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Simiyu katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba – Disemba, 2021).

UZUIAJI RUSHWA

TAKUKURU Mkoa wa Simiyu ilijikita katika Kuzuia Rushwa kwenye miradi ya maendeleo 123 inayotekelezwa katika Mkoa mzima wa Simiyu yenye thamani ya Sh. 7,197,164,667/=

Kati ya miradi hiyo mia moja ishirini na tatu (123) mia moja na kumi na tano (115) ni miradi ya ujenzi wa madarasa mia mbili themanini na nne (284) yenye thamani ya Sh. 5,680,000,000/= inayotekelezwa katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu yaani Halmashauri ya wilaya Bariadi, Meatu, Itilima, Busega, na Bariadi mji. Madarasa hayo yanajengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO -19 – miradi iliyopewa fedha za Serikali na ufadhili wa wadau wa maendeleo kwa miradi inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Mradi mmoja (1) ni mradi wa maji wa Mwagila wenye thamani ya Sh. 880,000,000/= unaotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Meatu katika Kata ya Mwanhuzi, mradi mmoja (1) ni ujenzi wa jengo la kituo cha afya cha Mwaunda wenye thamani ya Sh. 450,000,000/= katika halmashauri ya Wilaya ya Itilima na miradi sita (6)nimiradi ya uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19 yenye tamani ya Sh. 187,164,666 kwa halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu.

TAKUKURU Simiyu ilifanya ufuatiliaji ili kuhakikisha fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika ipasavyo na miradi inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na kuhakikisha kuwa hakuna ubadhirifu wala uvujaji wa fedha. Aidha katika miradi hiyo mia moja ishirini na tatu (123) iliyokaguliwa miradi (115) ya ujenzi wa madarasa imekamilika, miradi (06) ya uhamasishaji na utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 bado inaendelea na mradi wa maji wa Mwagila katika Halmashauri ya wilaya ya Meatu unaendelea na utekelezaji.

Katika ufuatiliaji tulibaini baadhi ya miradi hiyo ya ujenzi wa madarasa haikuzingatia vipimo vilivyokuwa katika BOQ na pia tulibaini kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa vifaa jambo lililopelekea baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati kulingana na mwongozo.

Aidha katika miradi ya chanjo ilibanika kuwepo kwa ukiukwaji wa Mwongozo wa Matumizi ya fedha za utekelezaji wa shughuli mbalimbai za chanjo ya UVIKO 19 na pia ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya walengwa kutokana na changamoto za mfumo wa malipo kwa vifungu nje ya bajeti.

Baada ya ufuatiliaji huu, TAKUKURU ilifanya warsha na wadau husika na kwa pamoja tuliweka mikakati ya namna ya kurekebisha mapungufu haya na tayari kazi ya kurekebisha imesha anza.

Sambamba na hilo kwa kipindi husika ofisi imefanya kazi moja (01) ya uchambuzi wa mfumo wa vihatarishi vya Rushwa ya Ngono katika Idara ya Elimu katika wilaya zote tano za mkoa wa Simiyu ili kubaini ukubwa wa tatizo na maeneo hatarishi yanayochochea vitendo vya Rushwa  ya Ngono katika idara ya Elimu.

Aidha Ofisi ilifanya warsha ya usimamizi wa mitihani katika Chuo cha Maafisa Tabibu wilayani Maswa kwa lengo la kujadili matokeo ya uchambuzi wa mfumo huo ambapo ilibainika kulikuwepo na ukiukwaji wa Mwongozo wa Usimamizi wa Mitihani.

Maazimio yaliyowekwa katika warsha hiyo ni kusimamia matumizi ya Mwongozo husika kikamilifu ili kudhibiti kuvuja kwa mitihani.

Ndugu Wanahabari,

Kwa upande Dawati la Uchunguzi, TAKUKURU mkoa wa Simiyu kwa kipindi cha robo ya pili, Oktoba – Disemba cha mwaka wa fedha 2021/2022 tumepokea taarifa 68 ambapo kati ya hizo 42 zilihusu rushwa na 26 hazihusiani na masuala ya rushwa.

Kati ya taarifa 42 ambazo hazikuhusu masuala ya rushwa watoa taarifa walishauriwa na kuelimishwa kuhusu mambo mbalimbali waliyokuwa wakiyalalamikia.

Aidha kati ya taarifa 42 zilizohusu rushwa, 2 uchunguzi umekamilika na  watuhumiwa wameshafikishwa mahakamani. Taarifa 40 zinaendelea na Uchunguzi.

Kwa mujibu wa taarifa 68 tulizopokea idara zilizolalamikiwa ni kama ifuatavyo: Serikali za Mitaa (7), Ardhi (11), Elimu (9), Uhamiaji (1), Polisi (1), Madini (1), Vyama vya Ushirika (13), Sekta binafsi (5), Afya (5), Ulinzi (1),Fedha (1), Utawala (6),Mahakama (2), Ujenzi (1), Kilimo (2), Tarura (1) na TANESCO (1).

Kesi zinazoendelea mahakamani ni 13 kati ya hizo kesi mpya ni mbili (2) na katika kipindi hicho cha Oktoba – Disemba, 2021 kesi nne (4) ziliamuliwa mahakamani na Jamhuri kushinda kesi zote.

Katka kipindi hiki pia, Uchunguzi umeweza kubaini ubadhilifu wa fedha za ununuzi wa pamba uliofanywa na baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) katika mkoa wa Simiyu ambapo walinunua pamba toka kwa wakulima kwa bei ya chini ikilinganishwa na bei ambayo makampuni ya ununuzi wa pamba yalilipa kwa vyama hivyo katika msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2021/2022.

AMCOS zilizobainika kufanya ubadhilifu ni 21, kati ya hizo 2 ni kutoka Wilaya ya Bariadi, 7 kutoka Meatu, 9 kutoka Maswa na 3 kutoka wilaya ya Itilima. Kiasi cha fedha kilichobainika kufanyiwa ubadhilifu hadi sasa ni Sh. 27,544,775/. Uchunguzi wa AMCOS husika unaendelea na pindi utakaokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Ndugu Wanahabari,

Kwa upande wa Dawati la Elimu kwa Umma, Taasisi imeendelea na jukumu lake la kuelimisha umma huku ikitoa kipaumbele kuelimisha wananchi wote kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

Ushirikiano na SKAUTI:

Katika kipindi hiki TAKUKURU iliweza kutoa elimu ya mapambano dhidi ya Rushwa kwa vijana wa Skauti 200 wa wilaya ya Kahama kupitia kampeni maalum ya TAKUSKA ambapo TAKUKURU na SKAUTI wameungana ili kutoa elimu kwa vijana wa skauti na kuwajenga wakue katika misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji kwao na kwa Taifa lao. 

Katika kipindi hiki Ofisi ya TAKUKURU – (M) Simiyu iliweza kufanya kazi nyingine za uelimishaji zifuatazo;

NAKAZI ZILIZOFANYIKAIDADI
1.Semina.42
2.Mikutano ya hadhara.11
3.Uimarishaji wa klabu.44
4.Mikutano na vyombo vya habari.02
5.0nyesho01
Jumla ya wananchi 11,662 walielimishwa.

TAKUKURU INAYOTEMBEA

Ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Simiyu imeweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi siku moja kila mwezi kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ambapo katika kipindi cha Oktoba – Desemba, 2021 TAKUKURU (M) wa Simiyu ilitembelea na kusikiliza kero katika Kata 3 ambazo ni Mwaubingi, Gamboshi na Ibulyu. Katika ziara hizo, wananchi walipatiwa elimu ya kutosha juu ya madhara ya rushwa, wajibu wao katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na namna ya kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwenye ofisi za TAKUKURU.

Utaratibu huu wa kusikiliza Kero za wananchi kwa kuwafuata walipo utaendelea kwa kila mwezi katika wilaya zote zilizopo Mkoa wa Simiyu hivyo kwa wananchi wasioweza kufika katika ofisi zetu watumie nafasi hiyo kuwasilisha kero zao pindi tutakapofika kwenye maeneo yao.

MIKAKATI YA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU MKOA WA SIMIYU KWA KIPINDI CHA MWEZI JANUARI HADI MACHI, 2022.

Ndugu Wanahabari,

Mkakati mkubwa kwa kipindi hiki ni kutoa elimu kwa vijana wa Skauti ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwajenga kwenye misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji kwao binafsi  na kwa Taifa lao pia washiriki katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki katika kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao. 

TAKUKURU Simiyu itaendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha zote za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu na afya zilizotumika na zinazotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoani Simiyu ikiwa ni pamoja kukagua miradi yote inayotekelezwa kuhakikisha kuwa miradi inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali ya awamu ya sita. 

Ndugu Wanahabari,

Mwisho napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wote mkiwemo waandishi wa habari kwa kushiriki kwenu katika mapambano dhidi ya rushwa, kwani wadau wote tukishirikiana kwa pamoja tutashinda vita hii ya Kupambana na rushwa.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

IMETOLEWA NA:

OREST P. MUSHI

KAIMU MKUU WA TAKUKURU (M) SIMIYU

SIMU: 0738150

Taarifa kwa Umma