TAKUKURU SHINYANGA YAFUATILIA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 4.1
Hii ni taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba-Disemba, 2021). Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga ilijikita katika Kuzuia Rushwa kwenye miradi ya maendeleo sitini na mbili (62) inayotekelezwa mkoa mzima wa Shinyanga.
TAKUKURU Shinyanga ilifuatilia jumla ya miradi Sitini na mbili (62) yenye thamani ya Sh. 4,127,494,475/= Kati ya miradi hiyo sitini na mbili (62) miradi sitini (60) ni miradi ya ujenzi wa madarasa yenye thamani ya Sh. 4,085,996,434/= inayotekelezwa katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga yaani Halmashauri ya wilaya Msalala, Ushetu, Kishapu, Shinyanga, Kahama Manispaa na Shinyanga Manispaa. Mingine – miradi miwili (2) ni ya rasilimali kilimo yenye thamani ya Sh. 41,498,041/= inayotekelezwa Manispaa ya Shinyanga katika Kata ya Mwamalili na Pandagichiza. Miradi hii sitini (60) ni ya ujenzi wa madarasayanayojengwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko -19.
TAKUKURU mkoa wa Shinyanga ilifanya ufuatiliaji huo ili kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika ipasavyo na miradi inakuwa na thamani halisi ikilinganishwa na fedha iliyotolewa.
Lengo lingine ni kuhakikisha kuwa hakuna ubadhirifu wala ufujaji wa fedha. Aidha katika miradi hiyo 62 iliyokaguliwa miradi 60 ya ujenzi wa madarasa imekamilika na miradi miwili ya vituo vya rasilimali kilimo inaendelea kutekelezwa.
Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hii ambavyo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa. yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau ambao ni wasimamizi na watekelezaji wa miradi husika pamoja na kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa.
Sambamba na hilo kwa kipindi husika, ofisi imefanya kazi sita (06) za uchambuzi wa mfumo katika halmashauri tatu ili kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa katika uombaji na utoaji wa leseni za uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo, usimamizi wa mitihani katika vyuo vya kati, ukusanyaji wa ada za maegesho ya vyombo vya usafiri pamoja na faini. Katika kuboresha kazi hizi, ofisi ilifanya vikao vya warsha na kujadiliana na wadau namna ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika katika Taaasisi hizo hivyo utelekezaji wa maazimio ya vikao vya warsha yanaendelea.
Kwa upande Dawati la Uchunguzi, TAKUKURU mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha robo ya pili, Oktoba – Disemba cha mwaka wa fedha 2021/2022 tumepokea taarifa/malalamiko 42 ambapo taarifa zinazohusu rushwa zilikuwa 20 na zisizohusu rushwa zilikuwa 22.
Kati ya taarifa 20 zilizohusu rushwa, taarifa 9 uchunguzi wake unaendelea na taarifa 11 uchunguzi wake umefungwa kwa kukosa ushahidi. Kutokana na taarifa 22 ambazo hazikuhusu rushwa, taarifa 2 zilihamishiwa idara nyingine na taarifa 20 watoa taarifa wake walishauriwa.
Kwa mujibu wa taarifa 42 tulizopokea, idara zilizolalamikiwa ni kama ifuatavyo: Serikali za Mitaa (16), Ardhi (9), Biashara (6), Elimu (2), Maji (2), Uhamiaji (2), Polisi (2), Madini (1), Vyama vya Ushirika (1) na Sekta binafsi (1).
Kesi zinazoendelea mahakamani ni 23 ambapo kati ya hizo, kesi mpya ni mbili (2) ambazo zilifunguliwa katika kipindi cha Oktoba – Desemba, 2021.
Kwa upande wa Dawati la Elimu kwa Umma, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imeendelea na jukumu lake la kuelimisha umma huku ikitoa kipaumbele kuhamasisha wananchi wote kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.
Katika kipindi hiki TAKUKURU iliweza kutoa elimu ya mapambano dhidi ya Rushwa kwa vijana wa Skauti 200 wa Wilaya ya Kahama kupitia kampeni maalum ya TAKUSKA ambapo TAKUKURU na SKAUTI wameungana ili kutoa elimu kwa vijana wa skauti na kuwajenga wakue katika misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji – kwao na kwa Taifa lao.
Katika kipindi hiki ofisi ya TAKUKURU – (M) Shinyanga iliweza kufanya kazi nyingine za uelimishaji zifuatazo;
NA | KAZI ZILIZOFANYIKA | IDADI |
1. | Semina. | 20 |
2. | Mikutano ya hadhara. | 19 |
3. | Uimarishaji wa klabu. | 19 |
5. | Mikutano na vyombo vya habari. | 1 |
Jumla ya wananchi 3,057 walielimishwa. |
MIKAKATI YA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU MKOA WA SHINYANGA KWA KIPINDI CHA MWEZI JANUARI HADI MACHI 2022.
Mkakati mkubwa kwa kipindi hiki ni kuendelea kutoa elimu kwa vijana wa Skauti ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwajenga kwenye misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji kwao na kwa Taifa lao pia washiriki katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki katika usimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
TAKUKURU mkoa wa Shinyanga itaendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha zote za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu na afya zilizotumika na zinazotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo Mkoani Shinyanga ikiwa ni pamoja kukagua miradi yote inayotekelezwa kuhakikisha kuwa miradi inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali ya awamu ya sita.
Mwisho napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na wadau wote mkiwemo waandishi wa habari kwa kushiriki kwenu katika mapambano dhidi ya rushwa, kwani wadau wote tukishirikiana kwa pamoja tutashinda vita hii ya Kupambana na rushwa.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
Hussein Mussa
Mkuu wa TAKUKURU (M) Shinyanga.
0738150196.