Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2021, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa imeendelea kutekeleza Majukumu yake ya Msingi kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 kupitia madawati ya Uchunguzi na Mashtaka, Uzuiaji Rushwa pamoja na Elimu kwa Umma.
UCHUNGUZI NA MASHTAKA
- Taarifa zilizopokelewa (Kisekta).
Katika kipindi hiki, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa imepokea jumla ya taarifa 58; kati ya hizo, taarifa 44 zilihusu rushwa ambapo ofisi imezifanyia kazi kwa kuanzisha majalada ya uchunguzi na taarifa 14 hazikuhusu rushwa hivyo ofisi imetoa ushauri kwa watoa taarifa na kuwaelekeza mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko hayo. Hakukuwa na taarifa iliyohamishiwa idara nyingine.
Taarifa hizi zimepokelewa kisekta kwa mchanganuo ufuatao:-
IDARA/SEKTA | SUMBAWANGA | KALAMBO | NKASI | JUMLA | |
Serikali za Mitaa | 7 | 5 | 3 | 15 | |
SACCOS | 1 | 0 | 1 | 2 | |
Fedha | 2 | 1 | 1 | 4 | |
Ardhi | 2 | 0 | 1 | 3 | |
Binafsi | 6 | 2 | 1 | 9 | |
Elimu | 3 | 4 | 0 | 7 | |
Afya | 1 | 2 | 4 | 7 | |
Miundombinu | 0 | 2 | 0 | 2 | |
POLISI | 2 | 0 | 0 | 2 | |
PSSSF | 1 | 0 | 0 | 1 | |
TFS | 0 | 0 | 1 | 1 | |
Mahakama | 2 | 1 | 0 | 3 | |
SIASA | 1 | 1 | 0 | 2 | |
Jumla Kuu | 28 | 18 | 12 | 58 |
- Kesi zilizoendelea Mahakamani.
Katika kipindi husika, tulifanikiwa kufungua kesi mpya moja (01) na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani mpaka sasa kuwa kesi nane (8); Kesi hizo zipo wilaya ya Kalambo – kesi mbili (2), wilaya ya Nkasi kuna kesi mbili (2) na wilaya ya Sumbawanga kuna kesi nne (4).
UZUIAJI RUSHWA
Ndugu Wanahabari,
Ili kuboresha mifumo mbalimbali ya utoaji wa huduma kwa wananchi, katika kipindi hiki TAKUKURU Mkoa wa Rukwa iliendelea kufanya chambuzi mbalimbali za mifumo ikiwemo vihatarishi vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu, mfumo na tathmini ya utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Manunuzi Serikalini (GPSA) pamoja na Ununuzi na Ugavi wa Madawa katika vituo vya afya, zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa.
Aidha katika Dawati la Udhibiti, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa katika kipindi hiki, imefanya ufuatiliaji wa miradi 262 yenye jumla ya thamani ya Tshs. 6,539914763.50; ikiwemo miradi ya UVIKO – 19 ya sekta ya elimu yenye jumla ya ujenzi wa vyumba 259 vya madarasa vyenye thamani ya Tshs. 3,090,000,000/= katika shule 87 za sekondari na shule 2 za msingi katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa, ambapo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga miradi yote imekamilika na kwa Halmashauri za Wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi hatua za umaliziaji kwa baadhi ya miradi inaendelea kukamilishwa, miradi 2 ya utoaji wa chanjo ya UVICO – 19 yenye thamani ya Tshs. 89,703,763.51, ujenzi wa Kituo cha Rasilimali Kilimo Kijiji cha Katumba Azimio wenye thamani ya Tshs. 230,211,000/=, ujenzi wa Kituo cha Rasilimali Kilimo Kijiji cha Mpui wenye thamani ya Tshs. 130,000,000/= pamoja na ujenzi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga wenye thamani ya Tshs. 3,000,000,000/=.
Katika ufuatiliaji huu hakukuwa na mianya iliyobainishwa ambayo ingeweza kusababisha mianya ya rushwa.
Ufuatiliaji wa wadaiwa (Defaulters) wa ukusanyaji mapato (POS) unaendelea katika Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ili kuhakikisha fedha wanazodaiwa zinarejeshwa.
Ifuatayo ni takwimu ya utekelezaji wa miradi ya UVICO – 19 katika sekta ya elimu – Mkoa wa Rukwa:
HALMASHAURI | IDADI YA VYUMBA VYA MADARASA | IDADI YA VYUMBA VYA MADARASAVILIVYOKAMILIKA | HATUA |
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga | 45 | Vyumba 45 vya madarasa vimekamilika maboma na madawati | Vimekamilika |
Halmashauri ya wilaya sumbawanga | 87 | Vyumba 14 vya madarasa vimekamilika maboma na madawati | Vyumba vya madarasa 73 vipo hatua za umaliziaji |
Halmashauri ya wilaya ya Nkasi | 68 | Vyumba 12 vya madarasa vimekamilika maboma na madawati | Vyumba vya madarasa 56 vipo hatua ya umaliziaji |
Halmashauri ya wilaya ya Kalambo | 59 | Vyumba 21 vya madarasa wamekamilisha maboma bado madawati | Vyumba vya madarasa 38 vipo hatua ya umaliziaji |
JUMLA | 259 | 90 | 169 |
ELIMU KWA UMMA
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha kwamba Wananchi wa Rika/Kada mbalimbali katika Mkoa wa Rukwa wanaendelea kupewa elimu na uelewa juu ya vitendo vya Rushwa ili washiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Rushwa ndani ya jamii yetu, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa katika kipindi cha miezi mitatu (3) Oktoba hadi Desemba, 2021, imefanya jumla ya semina ishirini (20) kwa wadau mbalimbali ili kuwakumbusha wajibu wao katika kupambana na rushwa, imeimarisha Klabu za Wapinga Rushwa thelasini na mbili (32) katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo kwa lengo la kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na kuwajenga wanafunzi kimaadili
USHIRIKIANO WA TAKUKURU NA SKAUTI:
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa nikuwajenga vijana katika misiki ya Uzalendo, Uwajibikaji na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
Aidha, katika kipindi hiki TAKUKURU Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo baadhi ya Wakuu wa Idara katika Halmashauri za Wilaya, Maafisa Watendaji wa Kata, Mitaa na vijiji, Maafisa Tarafa, Waheshimiwa Madiwani, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wakuu wa Vituo vya Polisi katika maeneo husika kwa kufanya mikutano ya hadhara kumi na mbili (12) ikiwemo mitatu (3) kupitia “PROGRAMU YA TAKUKURU INAYOTEMBEA (PCCB MOBILE)” kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika maeneo yao, imerusha vipindi vya redio sita (6), imeandika makala sita (6) pamoja na kuongea na Waandishi wa Habari ili kuhakikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa inawafikia wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine ya Tanzania.
MIKAKATI YA MWEZI JANUARI HADI MACHI, 2022:
Aidha kwa mwaka 2022/2023 TAKUKURU Mkoa wa Rukwa kupitia Dawati la Uzuaji Rushwa itaendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ni ile ya UVICO – 19 inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa na kudhibiti upoteaji wa fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kufuatilia Miradi ya Ujenzi wa barabara zilizo chini ya TARURA.
Pia kwa mwaka 2022/2023 TAKUKURU Mkoa wa Rukwa itaendelea kufanya udhibiti na uchunguzi kuhusu ubadhirifu wa fedha za serikali katika ugavi wa dawa na bidhaa za afya (vifaa tiba) ambao umekuwa ukijitokeza katika Vituo vya Afya na Hospitali za Serikali Mkoa wa Rukwa ili wote wanaohusika na ubadhirifu huo wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, kwa upande wa Uelimishaji Umma tutaendelea na uelimishaji huku msisitizo ukiwa katika kuendeleza ushirikiano kupitia TAKUKURU na SKAUTI kwa kuwalenga vijana.
WITO:
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Rukwa bado inaendelea kutoa rai kwa wale wote wanaowatapeli wananchi kwa kujifanya maafisa wa TAKUKURU na wale wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya rushwa waache mara moja, kwani wakikamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
TAKUKURU Mkoa wa Rukwa tunaendelea kutoa shukrani kwa viongozi mbalimbali na wanannchi kwa kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa zinazohusu vitendo vya rushwa.
Aidha, TAKUKURU tunawashukuru sana wana habari wote katika Mkoa wetu wa Rukwa ambao mmekuwa mstari wa mbele kufikisha elimu hii ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na maeneo mengine, maana mapambano dhidi ya rushwa si ya TAKUKURU pekee bali yanamhusu kila mtu/mtanzania.
Imetolewa na:
DANIEL NTERA
MKUU WA TAKUKURU (M) RUKWA
SIMU: 0738150186