TAKUKURU PWANI YAONYA WANAOHUJUMU MIRADI YA MAENDELEO NCHINI
Ndugu wanahabari,
Ninawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwakuwa tunakutana kwa mara ya kwanza ndani ya mwaka huu, basi nichukue fursa hii kuwatakieni nyote HERI YA MWAKA MPYA wa 2022.
Nimewaalikeni kuja hapa ili kupitia kwenu, Watanzania wote wafahamu kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba, 2021. Aidha ikumbukwe kuwa ni utaratibu wetu kufanya hivyo ili umma wa Watanzania ufahamu tunafanya nini na wahamasike kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya Rushwa nchini. Kwa msingi huo naomba kuainisha kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi hicho kama ifuatavyo:
UCHUNGUZI NA MASHITAKA
Kwa robo hii ya mwaka, ofisi ilipokea jumla ya malalamiko 132. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 93 yalihusu Rushwa na malalamiko 39 hayakuhusu rushwa. Kati ya malalamiko 93 yaliyohusu Rushwa, malalamiko 92 Uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na lalamiko 1 uchunguzi wake umekamilika.
Kati ya malalamiko 39 ambayo hayakuhusiana na rushwa, walalamikaji 34 walielimishwa na kushauriwa ili kutatua tatizo husika na malalamiko 5 yalihamishiwa idara nyingine.
Mchanganuo wa takwimu za taarifa kiidara ni kama ifuatavyo:
Afya- 30; Ardhi- 13; Mahakama- 8; Elimu- 9; Magereza-2; Fedha- 1; Habari-1; Ulinzi-1; Maendeleo ya Jamii- 1; Maliasili na Misitu- 2; Manunuzi- 1; Mapato- 2; Utawala-3; Nishati- 2;Mifugo-2; Jeshi la Polisi- 11; Tamisemi- 24; Ujenzi- 3; Usafirishaji- 1; Ushirika- 3; Uvuvi-1; Viwanda- 1; Binafsi-11 na Ushirika-1.
Katika kipindi husika, kesi mpya moja (1) ilifunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya mashauri 15 kuendelea mahakamani.
ELIMU KWA UMMA.
Ndugu waandishi wa habari,
Katika kipindi husika, tumeweza kuelimisha jumla ya wananchi 10,012 kupitia Semina 34, Mikutano 54, maonesho 3 na kipindi cha Redio 1. Aidha tuliweza kuandika makala 4 zenye maudhui ya kutokomeza Rushwa katika jamii, pia tuliimarisha klabu 74 za wapinga rushwa mashuleni ili kuwajenga na kuimarisha uadilifu kwa vijana na kuwapa ujasiri wa kukemea vitendo vya Rushwa.
Tuliweza kuwafikia wananchi na kusikiliza kero zao kwa utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA (PCCB MOBILE). Utaratibu huu ulianzishwa ili kumsogezea huduma mwananchi. Ni utaratibu ambao watumishi wa TAKUKURU wanatoka ofisini na kwenda vijijini au katika kata ili kusikiliza kero za wananchi zinazohusiana na vitendo vya Rushwa na kuzitatua kwa wakati na taarifa nyingine kuanzishiwa uchunguzi. Utaratibu huu umekuwa na mafanikio makubwa sana katika vita dhidi ya Rushwa mkoani Pwani kwani wananchi wengi wamekuwa wakijitokeza kuwasilisha kero zao na kuweza kupata ufafanuzi juu ya kero walizonazo ndani ya muda mfupi.
Elimu tuliyotoa kwa kipindi tajwa ilihusu mambo yafuatayo:-
- Makatazo ya Rushwa kwa mujibu wa vitabu vitakatifu vya Mungu; elimu iliyotolewa kupitia vipindi vya redio ambapo inaaminika kwamba viongozi wetu wa dini wakiunganisha nguvu zao katika kukemea vitendo vya Rushwa jamii itabadilika na kuacha vitendo vya Rushwa.
- Umuhimu wa wananchi kusimamia miradi ya maendeleo ili miradi hiyo iwe na tija kwa ustawi wa jamii, kwani miradi hiyo ndio msingi wa ujenzi wa Taifa imara katika kutoa huduma bora kwa jamii. Kwani serikali yetu inaelekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo. Hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha miradi hii inasimamiwa vyema na kuleta matokeo chanya katika kutatua changamoto zinazowakabili. Elimu hii inatarajiwa ikawe chachu katika kusimamia miradi inayoendelea kujengwa na serikali kama ambavyo tumefanya katika ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 kupitia mkopo nafuu usio na riba.
- Kupitia kampeni yetu ya Vunja Ukimya: Kataa Rushwa Ya Ngono elimu juu ya madhara ya rushwa ya ngono ilitolewa kwa jamii ikiwa na lengo la kuonyesha nafasi ya wananchi katika ushiriki wa kampeni hii na kuhamasisha umma kuwa jasiri katika kutoa taarifa za rushwa ya ngono.
Aidha, Katika kipindi hiki TAKUKURU mkoa wa Pwani ilishiriki katika shughuli mbalimbali za kitaifa ambapo tarehe 23/10/2021 tulishiriki katika KILELE CHA MAADHIMISHO YA WIKI YA UWT (Umoja wa Wanawake Tanzania) yaliyofanyika wilayani Rufiji kitaifa ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. SAMIA SULUHU HASSAN.
Aidha katika kuadhimisha SIKU YA MAADILI NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA NCHINI ambayo huadhimishwa tarehe 10 Desemba ya kila mwaka, TAKUKURU mkoa wa Pwani iliweza kutoa elimu ya mapambano dhidi ya Rushwa kwa wananchi na kutembelea Gereza la mahabusu kutoa elimu ya Madhara ya Rushwa kwa maafisa magereza pamoja na mahabusu wenyewe pamoja na kutoa vifaa mbalimbali vya usafi wa mwili kwa mahabusu hao.
TAKUKURU mkoa wa Pwani ilishirikiana kwa ukaribu na Kamati za Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wilaya zake zote, wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Idara, katika kuhakikisha MKAKATI WA KUWATUMIA SKAUTI KUTOA ELIMU YA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA mashuleni na vyuoni inafanikiwa. Kamati hizi za ulinzi na usalama wamejitolea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa katika mkoa wetu chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. ABUBAKARI KUNENGE ambapo tayari uzinduzi wa mkakati huo umekwishafanyika na wadau wote ngazi ya mkoa na wilaya walishiriki kikamilifu.
UZUIAJI RUSHWA
Katika eneo la Uzuiaji Rushwa tulifanya chambuzi za mifumo katika sekta za Elimu na Mapato ya Halmashauri.
- Katika elimu tulifanya uchambuzi wa mfumo kuhusu Rushwa ya Ngono katika sekta ya Elimu. Kupitia uchambuzi huu TAKUKURU kwa kushirikiana na wadau wa elimu wa vyuo hivyo tulifanya kikao kazi (Warsha) na kuweka maazimio ya kutekeleza ili kuondoa changamoto au mapungufu yanayoweza kupelekea mianya ya rushwa katika eneo hili la elimu.
- Pia tulifanya uchambuzi wa mfumo katika usimamizi wa fedha za makusanyo vijijini (5%) ambapo yaliyobainika yaliwasilishwa katika kikao kazi cha TAKUKURU Mkoa wa Pwani na wadau wa ukusanyaji mapato vijijini na kuwekeana maazimio ya kutekelezwa na wadau hao ili kuziba mianya ya rushwa.
UFUATILIAJI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
Ndugu waandishi wa habari,
Mtakumbuka kuwa ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika nchi yetu inakuwa na tija na kutoa huduma zilizokusudiwa kwa jamii. Hayo hufanywa sambamba na kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma (PETS) katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Ufuatiliaji huu unalenga kubainisha yafuatayo:
- Mianya ya rushwa katika utekelezaji wa miradi.
- Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi.
- Uvujaji wa fedha na raslimali za miradi.
- Ushirikishwaji wa wananchi/wadau katika utekelezaji wa miradi.
- Mtiririko wa fedha hufuatiliwa kutoka chanzo (Hazina, wafadhili au vyanzo vya ndani) mpaka kwenye mradi husika (utekelezaji wa mradi) ili kubaini mapungufu katika utekelezaji wa miradi husika.
Aidha, TAKUKURU huchukua hatua zifaazo kulingana na kinachobainika katika ufuatiliaji, zikiwemo, kushauri au kujadiliana na wadau kuhusu namna ya kuondoa mapungufu yaliyobainika ili thamani ya fedha ifikiwe, kuelimisha wananchi/wadau au kuanzisha uchunguzi pale inapobidi.
Katika robo hii ya mwaka, tumekagua jumla ya miradi ya maendeleo Hamsini na Sita (56) katika Sekta za Afya, Elimu na Maji. Miradi hiyo ina thamani ya Shilingi Bilioni kumi na moja,milioni mia Tisa na arobaini, laki moja sabini na sita elfu, mia saba na hamsini na tano na senti tisini na tisa (11,940,176,755.99).
Mapungufu yaliyobainika katika miradi iliyofuatiliwa hususani katika ujenzi wa madarasa ni pamoja na vipimo vya kitaalamu vilivyotumiwa katika ujenzi kutofautiana na matakwa ya Bill of Quantity – BOQ. Ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa, TAKUKURU Mkoa wa Pwani iliandaa warsha ya majadiliano na wataalamu husika kuhusiana na mapungufu yaliyobainishwa ambapo maboresho yalifanyika na kazi za ujenzi wa madarasa husika unaendelea.
MIKAKATI YETU KWA KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI, 2022
- Kuendelea kuelimisha umma wa watanzania juu ya madhara ya rushwa ili wafahamu nafasi yao katika mapambano dhidi ya rushwa kwani vita hii si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya watanzania wote, elimu ambayo tutaitoa kupitia vijana wetu wa SKAUTI na Klabu za wapinga Rushwa mashuleni na vyuoni.
- Kuendelea kufanya ufuatiliaji wa mifumo kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa itakayobainika.
- Kuendelea kukagua utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo katika mkoa wetu ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na kwa ubora unaostahili na kuleta tija kwa jamii.
- Kukamilisha chunguzi zote zinazoendelea kwa kasi na kwa weledi mkubwa.
WITO WA TAKUKURU KWA WANANCHI
Ndugu waandishi na wananchi,
Naomba kutumia fursa hii kuwasihi wananchi wa mkoa wa Pwani na watanzania kwa ujumla kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuepuka vitendo vya Rushwa kwani Rushwa ni adui namba moja kwa maendeleo ya nchi yetu, na kwakuwa dhamira ya Serikali yetu ni kuleta maendeleo basi hatuna budi kuepukana na vitendo vya Rushwa. Hivyo basi kila mmoja kwa nafasi yake aweze kujiepusha na vitendo vya Rushwa na Ufisadi.
Na kila mmoja awe mtoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa TAKUKURU pindi anapobaini uwepo wa vitendo hivyo.
Aidha, niwaombe sana wanaPwani kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu na kutoa taarifa pindi mnapobaini au kuwa na shaka juu ya utekelezaji wa miradi hiyo kwani serikali imeleta fedha nyingi katika Halmashauri zetu kwa ajili miradi hiyo kwa mfano mmeshuhudia miradi ya ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 na zahanati na vituo vya afya ili kumsaidia mtanzania kutatua changamoto za huduma za kijamii zinazomkabili. Ni tarajio letu kwamba miradi hiyo italeta tija kwa jamii endapo itafanywa kwa usimamizi wa karibu wa wananchi.
Aidha, katika usimamizi wa miradi hiyo tutangulize uzalendo, tuwe waaminifu na waadilifu ili kujenga Tanzania imara kadiri ya maelekezo ya serikali yetu pendwa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu SAMIA SULUHU HASSANI.
Ndugu WanaHabari,
Mwisho, nitoe ONYO kwa wote wenye nia mbaya ya kuihujumu Serikali kwenye miradi ya maendeleo. Nadhani mmeshuhudia maafisa wa TAKUKURU wakipita kukagua miradi hiyo kila wakati. Tutakuwa wakali sana kwa watu wanaojihusisha na Rushwa au ufisadi kwenye miradi hiyo ya maendeleo. Tuungane pamoja kuijenga Tanzania yenye maendeleo ya kweli kupitia miradi hii iliyoanzishwa na serikali yetu.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa Na:
SUZANA RAYMOND
Mkuu wa TAKUKURU (M),
PWANI.0738 150176