TAKUKURU MWANZA YAFUATILIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 9
Ndugu Waandishi wa Habari,
TAKUKURU mkoa wa Mwanza katika kipindi cha mwezi Oktoba – Disemba, 2021, imefanya ukaguzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi 17 ya maendeleo yenye thamani ya Sh 9,845,486,066.85/=.
Kati ya miradi hiyo 17 iliyokaguliwa, mradi 1 unahusu ujenzi wa miundombinu ya maji katika Kijiji cha Mwabilanda wilaya ya Kwimba wenye thamani ya Sh.333,000,000/=, mradi 1 wa ujenzi wa Kituo cha Afya Bulale katika Wilaya ya Nyamagana wenye thamani ya Sh. 250,000,000/=, mradi 1 wa ujenzi wa jengo la OPD Kituo cha Afya Sahwa wenye thamani ya Sh. 50,000,000/=, mradi 1 wa ukarabati wa ukumbi wa mikutano wa Gandhi- Hall wenye thamani ya Sh. 200,000,000/=, miradi ya ujenzi wa vyoo katika shule za msingi na maeneo ya umma yenye thamani ya Sh.3,684,268,652.99/=, miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara yenye thamani ya Sh. 3,088,632,863/=, miradi katika shule mbalimbali ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika sekta ya elimu kutokana na fedha za UVICO 19 yenye thamani ya Sh. 2,239,584,550.86/=.
Aidha, miradi hii ilikaguliwa na maelekezo mbalimbali yalitolewa kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo na kwa sasa miradi hiyo inaendelea kutekelezwa na iko katika hatua za ukamilishwaji.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pamoja na miradi hiyo iliyokaguliwa, TAKUKURU Mkoa wa Mwanza kupitia jukumu lake la Udhibiti na Uzuiaji Rushwa imefanya uchambuzi wa Mfumo wa Usimamizi wa mitihani katika Vyuo vya kati (Vyuo vya ngazi ya Certificate na Diploma) kwa lengo la kukagua endapo taratibu za utungaji, ufanyaji na usahihishaji wa mitihani zilizowekwa na Wizara zinazingatiwa .
Pia TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mfumo wa Elimu ili kubaini vyanzo vya Rushwa ya ngono katika idara ya elimu.Katika uchambuzi huu wadau mbalimbali walihusishwa wakiwemo Waalimu Wakuu,Wakuu wa shule, Maafisa Elimu, Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari ,Wenyeviti wa Bodi za Shule na Kamati za Shule na Maafisa Elimu Kata.
Vilevile Katika kipindi hicho,TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mfumo wa Utoaji huduma kwa Wakala wa Manunuzi nchini (GPSA) kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wake na huduma zinazotolewa na Wakala kwa Taasisi nunuzi.
Kazi hizi zote zimefanyika Tanzania nzima hivyo matokeo ya kazi hizi yametumwa Makao Makuu ambapo itaandaliwa taarifa ya Kitaifa na itakapokamilika itawasilishwa kwa wadau.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa upande wa Elimu kwa Umma katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Mwanza ilitoa elimu na kuyafikia makundi
mbalimbali kwa kufanya Semina 32, mikutano ya hadhara 10, vipindi 5 vya redio, habari 2, na kuimarisha klabu 16 za wapinga rushwa, kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo. Pia onesho moja lilifanyika siku ya jamii katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustino.
Katika kipindi hicho mkazo zaidi wa elimu umetolewa kwa Taasisi na Mashirika katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu – NACSAP III, na kuhakikisha watumishi na wananchi wanapata mafunzo ya maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu pamoja na makatazo ya rushwa. Taasisi zilizopatiwa elimu ni pamoja na Watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Watumishi wa TANROADS, pamoja na Wasimamizi wa Mitihani ya Taifa. Wengine ni wasimamizi na mafundi wa ujenzi katika miradi ya madarasa na zahanati zilizotokana na fedha za UVICO 19.
Ushirikiano wa TAKUKURU na SKAUTI – TAKUSKA
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika kipindi husika, katika kuendeleza ushirikiano katika uelimishaji uliopo kati ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Nchi, TAKUKURU mkoa wa Mwanza ilifanya semina 9 za kuutambulisha Mwongozo wa Mkakati wa TAKUSKA ambao unahusisha TAKUKURU na SKAUTI ukiwa na lengo la kuwaelimisha vijana wa SKAUTI katika mkoa wa Mwanza ili washiriki katika mapambano dhidi ya Rushwa.
Semina hizi zilifanyika kwa viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa na Wilaya wakiwemo; Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa TAKUKURU (M), Mkuu wa Skauti (M), Afisa Elimu(M) Wakuu wa Wilaya wote, Wakuu wa Skauti (W), Wakuu wa TAKUKURU (W), Maafisa Elimu (W), Mkuu wa Zimamoto (M) na (W), Waalimu wakuu Shule za Msingi na Sekondari, Walezi wa Skauti na Watumishi wengine mbalimbali.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika kipindi cha Oktoba –Disemba 2021 ,TAKUKURU (M) Mwanza ilipokea jumla ya Malalamiko 139. Kati ya hayo, malalamiko 70 yanahusu vitendo vya rushwa na malalamiko 69 hayahusiani na rushwa.
Kati ya malalamiko 70 yanayohusu vitendo vya rushwa, malalamiko 62 Uchunguzi wake unaendelea, malalamiko 6 uchunguzi wake umekamilika kwa watuhumiwa kufikishwa Mahakamani na malalamiko 2 majalada yake yamepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupata vibali vya kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani.
Kwa malalamiko 69 yasiyohusu rushwa, taarifa 10 zimehamishiwa kwenye idara nyingine na malalamiko 59 elimu na ushauri umetolewa kwa wahusika.
Katika taarifa hizo 139 zilizopokelewa, Idara ya Elimu inaongoza kwa kulalamikiwa malalamiko 16, ikifuatiwa na ofisi za Serikali za Mitaa (Wenyeviti na Watendaji wa vijiji, Mitaa, Vitongoji na Kata) kwa kuwa na taarifa 14, Ardhi 12, Mahakama 11, Michezo 10, Vyama vya Ushirka 9, TAMISEMI 8, Taasisi binafsi 7, Taasisi za Fedha 6, Idara ya Afya 5, Ujenzi 5, Uvuvi 4, Madini 4, Ustawi wa jamii 4, Uchukuzi 4,Polisi 3, Manunuzi 3, Kilimo 2, TANESCO 2, Biashara 2, Ulinzi 1,Maji 1, Bima 1, Viwanda 1, Idara ya Kazi 1, TRA 1, NAO 1, Posta 1.
Vilevile, katika kipindi husika TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imefungua mashauri mapya 6 mahakamani na hivyo kufanya jumla ya mashauri 13 yanayoendelea mahakamani kwa sasa.
Malengo;
TAKUKURU Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha Januari – Machi 2022 itaendelea kutekeleza majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na rushwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Vilevile, tutaendelea kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na wafadhili kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na zile zinazotolewa kwa ajili ya kupambana na UVICO 19.
Kazi nyingine ya kipaumbele ni kuendelea kuelimisha kundi la vijana na hususan Vijana wanachama wa Skauti, ili kuwafikia vijana wengi katika mkoa wetu.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wito kwa wananchi;
Ninatoa wito kwa wananchi wa mkoa wetu wa Mwanza, kuwa kila mwananchi analo jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo lake. Hivyo pindi mnapobaini utekelezaji mbovu wa miradi, mwananchi analo jukumu la kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU kwani madhara ya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanamgusa kila mwanajamii.
Mwisho, nina watahadharisha wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuepukana na matapeli wanaojifanya kuwa ni maafisa wa TAKUKURU, pindi mwananchi unapopigiwa simu na kuombwa pesa ili ushughulikiwe jambo lako ambalo liko TAKUKURU tafadhali toa taarifa mara moja au fika ofisini.
RUSHWA NI ADUI WA MAENDELEO
“Kwa taarifa za vitendo vya rushwa tafadhali fika ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nawe au piga simu ya dharura namba 113 au tuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au Piga *113# fuata maelekezo” Huduma hii ni ya BURE.
IMETOLEWA NA:
SIGNED
FRANK MKILANYA – 0738 150 162, MKUU WA TAKUKURU (M) MWANZA