KAMPENI YA UWAJIBIKAJI YALETA TIJA MIRADI YA MAENDELEO MKOA WA MTWARA
UTANGULIZI:
Ndugu Waandishi wa Habari,
Nimewaita hapa kwa lengo la kuujulisha umma juu ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021.Utaratibu huu ni wa kawaida ambao TAKUKURU imejiwekea ili kuhakikisha kuwa umma wa Watanzania pamoja na wakazi wa mkoa wa Mtwara wanafahamu jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Ndugu Waandishi wa Habari,
UZUIAJI RUSHWA – Kampeni Maalum:
TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, ilianzisha kampeni tunayoiita “Wajibika, chukua hatua stahiki kuzuia rushwa”. Lengo kuu la kampeni hii ni kubadili tabia ya walengwa kutoka kuwa walalamikaji hadi kufikia hatua ya kuchukua hatua stahiki kwa yale yaliyo katika mamlaka au uwezo wao. Katika kampeni hii tulifanikiwa kuwafikia wadau mbalimbali ikiwemo waheshimiwa madiwani katika Halmashauri zetu, kamati zinazo husika na miradi ya maendeleo na wananchi kiujumla, kupitia semina,vipindi vya redio na uelimishaji maeneo ya miradi.
Katika utekelezaji wa ujenzi wa madarasa haya tulishuhudia ushirikiano wa hali ya juu sana kwanza kwa viongozi ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri. Kamati zilizohusika na miradi pamoja na wananchi na viongozi wa maeneo husika walionesha ushirikiano mkubwa. Kwa ushirikiano huu changamoto nyingi zilizojitokeza zilitatuliwa na ushauri kutoka kwa wataalam na wadau ulitolewa mapema kwa wahusika.
- Kulikuwa na uwazi mkubwa kwa maana wananchi walijua kiasi cha fedha kilichotengwa kwaajili ya shughuli husika.
- Fedha zilifika kwa walengwa kwa wakati na kwa kiwango chote.
- Maamuzi ya kununua baadhi ya vifaa kama saruji, mabati, vigai (tiles) na mbao kwa wingi na kwa pamoja (bulk purchase) kutoka viwandani na kwenye chanzo kimoja, ulileta tija ya ubora wa vifaa, kupunguza gharama na upatikanaji wa vifaa kwa wakati nakufanya kazi zinazoweza kufanyika kwa wakati mmoja kufanyika na hivi kumaliza miradi kwa wakati.
- Kasoro mbalimbali zilizokuwa zinagundulika zilishughulikiwa kwa wakati.
Miradi yote ikifanyika kwa ushirikiano na uwazi wa kiwango hiki na kama kila mmoja wetu atachukua hatua stahiki iliyo ndani ya uwezo wake katika kushiriki ujenzi, kulinda miradi, kufuatilia matumizi ya fedha katika miradi hii na kuhakikisha kuna uwazi na uwajibikaji, Mkoa wa Mtwara utapiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
UENDESHAJI WA MASHTAKA:
Katika kipindi cha Oktoba 2021 hadi Desemba 2021, kesi sita (6) ziliendelea mahakamani na Kesi tatu (3) zilitolewa maamuzi ambapo Jamhuri ilishinda katika kesi mbili (2).
Ndugu Waandishi wa Habari,
UCHUNGUZI:
Katika kipindi cha Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara iliendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kama yalivyotamkwa katika kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 iliyorejewa mwaka 2019.
Katika kipindi tajwa jumla ya malalamiko (77) yalipokelewa TAKUKURU (M) Mtwara. Kati ya malalamiko hayo 77, malalamiko 57 yalihusu rushwa na malalamiko 20 hayakuhusu rushwa. Malalamiko 57 yaliyohusu rushwa yanafanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha makosa ya rushwa na uchunguzi wake bado unaendelea. Kwa Malalamiko 20 ambayo hayakuhusu rushwa, wahusika walishauriwa namna bora ya kupata haki zao. Hakukuwa na taarifa ambayo ilihamishiwa idara nyingine.
Mchanganuo wa Sekta au taasisi zinazolalamikiwa ni kama ifuatavyo:-
Halmashauri malalamiko (49) katika idara zake kwa mchanganuo ufuatao:- afya(21), utawala (8), elimu (6), ardhi (6), Ujenzi (3), biashara(2), Maji (2) na manunuzi (1).
Malalamiko mengine ni vyama vya Ushirika malalamiko (9), Polisi (5), mahakama (3), Magereza (1), Benki (1), viwanda (1) na binafsi (8).
Ndugu Waandishi wa Habari.
UZUIAJI RUSHWA:
katika kipindi tajwa, ili kuzuia Rushwa, tumefuatilia matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa hapa mkoani Mtwara.
Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha inapatikana.
Jumla ya miradi ya maendeleo 114 yenye thamani ya jumla ya shilingi 6,937,500,000/= ilifuatiliwa kama ilivyoainishwa kwenye jedwali hapa chini:-
Miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yatokanayo na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 :-
NA | MRADI | THAMANI (Tsh) |
1. | Ujenzi wa vyumba vya madarasa 109 katika shule 44 tofauti wilaya ya Mtwara. | 2,180,000,000/= |
2. | Ujenzi wa vyumba vya madarasa 82 katika shule 21 tofauti wilaya ya Tandahimba | 1,640,000,000/= |
3. | Ujenzi wa vyumba vya madarasa 80 katika shule 21 tofauti wilaya ya Masasi. | 1,600,000,000/= |
4. | Ujenzi wa madarasa 24 katika shule 5 tofauti wilaya ya Nanyumbu | 480,000,000/= |
JUMLA | 5,900,000,000/= |
Pia , umefanyika ufuatiliaji wa miradi mingine kama ilivyoainishwa kwenye jedwali hapo chini:-
NA | MRADI | THAMANI |
1. | Ujenzi wa OPD na Maabara kituo cha Afya ufukoni wilaya ya Mtwara. | 250,000,000/= |
2. | Ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa shule ya Msingi Mitengo wilaya ya Mtwara. | 37,500,000/= |
3. | Ujenzi wa OPD na Maabara hosipitali ya Mkomaindo wilaya ya Nanyumbu. | 500,000,000/= |
4. | Ujenzi wa kituo cha Afya Mtandi wilaya ya Nanyumbu. | 250,000,000/= |
JUMLA | 1,037,500,000/= |
Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hiyo ni pamoja na utunzaji duni wa nyaraka za miradi; ununuzi wa vifaa tofauti na maelekezo ya BOQ; usimamizi hafifu wa miradi na ushirikshwajii mdogo wa wananchi wa eneo husika – mambo ambayo yangeachwa yangeweza kusababisha mianya ya rushwa.
Mapungufu haya yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika pamoja na kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa iliyopo na kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha (Value for money).
Vilevile TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, inaendelea na uchambuzi mmoja (1) wa Mfumo juu ya vihatarishi vya Rushwa ya ngono katika sekta ya elimu kazi ambayo bado inaendelea kwa wilaya zote za mkoa wa Mtwara. Kupitia uchambuzi huu, baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na vihatarishi ni pamoja na upangaji wa vituo vya kazi; uhamisho ndani ya halmashauri; upandishwaji vyeo; uteuzi wa kufanya kazi maalum kama sensa au usimamizi wa mitihani na usimamizi na upangaji wa majukumu ya kila siku – mambo ambayo yasiposimamiwa vizuri yanaweza kusababisha mianya ya rushwa.
Baada ya mapungufu haya kubainishwa, TAKUKURU na Mamlaka husika imejadili na kuweka mikakati ya kurekebisha mapungufu haya.
Ndugu Waandishi wa Habari,
UELIMISHAJI UMMA:
Katika kuhakikisha kuwa TAKUKURU (M) wa Mtwara inashirikisha umma katika mapambano dhidi ya Rushwa, shughuli za kuelimisha Umma katika kipindi tajwa zilifanyika kwa kuendesha Semina 31, mikutano ya hadhara 18, kuimarisha Klabu 30 za wapinga rushwa katika shule za msingi, Sekondari na vyuo, Uandishi wa makala 5, Kuelimisha kupitia vipindi vya redio 7 na kutoa taarifa 1 kwa umma kupitia vyombo vya habari. Aidha jumla ya machapisho 1,506 yenye elimu dhidi ya rushwa yaligawiwa kwa wananchi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
TAKUKURU INAYOTEMBEA:
Pia kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA, kwa maana ya ofisi kuwafuata wananchi katika mahali walipo,TAKUKURU(M) wa Mtwara ikishirikiana na wadau wengine ikiwemo kamati za usalama za wilaya na mkoa iliwatembelea wananchi katika maeneo ambayo miradi inatekelezwa kwa lengo la kukagua miradi, kutatua kero na kutoa elimu.
Katika ziara hizi, kero za upatikanaji wa vifaa kwa wakati vilivyoagizwa katika viwanda ndani na nje ya mkoa kwaajili ya miradi hiyo zilitatuliwa vizuri sana na uongozi wa Mkoa na Wilaya zetu. Aidha elimu ya kuzingatia miongozo ya utekelezaji wa miradi, uundaji na ushiriki wa kamati pamoja na utunzaji sahihi wa kumbukumbu za miradi ilitolewa. Aidha katika kijiji cha RUKUMBI kata ya SENGENYA wilaya ya NANYUMBU wananchi walikuwa na kero ya kutosomewa mapato na matumizi kwa muda mrefu na pia vifaa vilivyokuwa vinatumika katika kazi za kujitolea za maendeleo vililalamikiwa kuwa vimekodishwa kisisiri kwa wananchi wachache na kufanya kazi za maendeleo kuwa ngumu.
TAKUKURU inayotembea wilayani Nanyumbu ikafuatilia masuala haya kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji husika Tarehe 29/12/2021 wananchi walisomewa taarifa ya mapato na matumizi na vifaa vilivyoazimishwa bila uwazi kwa wananchi vilirejeshwa. Mpaka kufikia tarehe 29/12/2021 vifaa vilivyopatikana ni karai 17, Torori 2, jembe 8, Sululu 5, Binding wire rola 2, gloves pair 32, misumeno 2, ndoo 2, pima maji 3, chepe 4, vijiko vya kujengea 2, First Aid Kit 1 na Rainboot pair 3. Jambo hili limeongeza hari ya wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
TAKUSKA:
TAKUSKA ni ushirikiano wa TAKUKURU na Chama cha SKAUTI kwa lengo la kushirikisha vijana wa skauti katika mapambano dhidi ya Rushwa kwa kuwapa mafunzo kwani ni kundi muhimu sana. Tunaamini tukishirikiana nao pamoja na klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni tutapiga hatua kubwa zaidi katika kulea vijana wazalendo na wenye hari na uwezo wa kupambana na rushwa.
TAKUKURU (M) Mtwara kwa ushirikiano na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mtwara na Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara, Novemba 21, 2021, waliutambulisha na kuukabidhi Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundisha Vijana wa Skauti kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Gen. Marko Elisha Gaguti.
Katika Wilaya ya Masasi mwongozo wa huo wa mafunzo kwa vijana wa skauti wilaya ya Masasi ulitambulishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi kwa kushirikiana na Mratibu wa Skauti Wilaya ya Masasi .
Hadi sasa uelimishaji skauti umefanyika katika makambi mawili ya skauti wilayani masasi ambapo jumla ya skauti 120 walifikiwa na elimu hii kati ya hao wavulana (87) na wasichana (33).
Ndugu Waandishi wa Habari,
MIKAKATI YA JANUARI – MACHI 2022:
Katika kipindi kilichoanza Januari 2022 hadi Machi 2022, mikakati ya TAKUKURU mkoa wa Mtwara katika kuzuia na kupambana na rushwa ni pamoja na ifuatayo:-
- Kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabaraza ya madiwani kwa lengo la kuwafanya wananchi kuchukua hatua na kushiriki mapambano dhidi ya Rushwa na kuacha kuwa walalamikaji tu.
- Kuendelea kutekeleza Mpango Kazi wa ushirikiano kati ya TAKUKURU na Chama cha SKAUTI – TAKUSKA
- Kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi katika sekta za kimkakati za maji, afya, elimu na ujenzi (barabara).
- Kuendelea kufanya chambuzi za mifumo ili kubaini sababu zinazosababisha kuwepo kwa Rushwa na kutoa ushauri wa namna ya kurekebisha au kuboresha na hatimaye kutoa huduma bora.
SHUKRANI NA WITO:
TAKUKURU (M) wa Mtwara inapenda kuwashukuru wananchi na wadau wote wa mkoa wa Mtwara kwa ushirikiano wanaotupatia katika shughuli zetu na tunaomba tuendelee na moyo huu wa kizalendo.
Pia napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati Ndugu waandishi wa habari, kwa ushirikiano wenu na pia nizidi kuwaomba kutuunga mkono katika kutekeleza majukumu yetu kwa kutupatia fursa katika vyombo vyenu ili kuwaelimisha wananchi kuhusu athari na madhara ya rushwa na namna salama na rahisi ya kukabiliana nayo.
Imetolewa na:
ENOCK P. NGAILO
MKUU WA TAKUKURU (M) MTWARA
0738150156