WALIMU WALEZI SKAUTI KITETO WAPATIWA MAFUNZO
Ndugu Wanahabari,
Heri ya Mwaka Mpya wa 2022.
Mtakumbuka katika taarifa yetu tuliyotoa kwa umma Oktoba, 2021 tuliwaeleza kuwa tulipanga kuanza utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kutoa elimu kwa vijana wa Skauti kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ili wawe washiriki wa kuzuia na kupambana na rushwa hatimaye waje kuwa msaada kwa Taifa letu kuanzia ngazi yao binafsi, familia na jamii inayowazunguka.
Ushirikiano wa TAKUKURU na SKAUTI:
Katika mwezi Oktoba-Desemba, 2021, tuliendelea na utekelezaji wa uzinduzi wa mwongozo wa kufundishia vijana Skauti ambao ngazi ya Mkoa ulizinduliwa na Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na kisha uzinduzi uliendelea katika ngazi za Wilaya. Aidha katika Wilaya ya Kiteto ushirikiano wa Mhe. Alhaji Mubarak Batenga, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Bw. John Nchimbi, ulituwezesha pia kutoa Semina kwa Walimu Walezi wa Skauti katika shule zote (112) za Msingi na Sekondari zilizoko wilayani Kiteto.
Kila mwalimu aliyewezeshwa kupitia uelimishaji huu, atakuwa mwezeshaji kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa kwa Skauti shuleni kwake, mafundisho ya uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na utaifa yatasisitizwa ili kuwafanya vijana hao wawe mfano wa uadilifu na msaada wa mapambano dhidi ya rushwa kuanzia kwa kijana mwenyewe, familia yake, jamii inayomzunguka na Taifa kwa ujumla. Tunatarajia zoezi la kuwezesha walimu katika Mkoa wa Manyara litakamilika katika wilaya zote za Mkoa huu ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari, 2022.
Ndugu Wanahabari,
Uzuiaji Rushwa:
Kupitia Dawati la Uzuiaji Rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Manyara tulifuatilia jumla ya miradi ya maendeleo (82) yenye thamani ya shilingi bilioni moja, mia sita arobaini milioni, (shilingi 1,640,000,000), mingi ikitumia njia ya manunuzi kupitia force account. Kwa mujibu wa ufuatiliaji huo,imebainika kwambaMiradi mingi iliyotembelewa inaakisi thamani ya fedha.
Aidha katika ufuatiliaji huo tulibaini kuwepo kwa baadhi ya Wakandarasi wanaoomba ujenzi wa miradi hiyo kama ‘Local fundi’, ambapo wanaomba kazi kwa bei inayowawezesha kuwashinda washindani wao katika tathmini ya nyaraka walizowasilisha lakini wakishapata zabuni hizo, huanza madai ya Variation kama ifanyikavyo kwenye miradi mikubwa kwa nia ya kujipatia mapato ya ziada bila kustahili. Ni Rai yetu kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa macho na watu wa aina hiyo ikizingatiwa kwamba utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa utaratibu wa force account bado unaendelea kufanyika.
Ndugu Wanahabari,
Uelimishaji Umma:
Kwa upande wa elimu kwa umma, jumla ya Semina 8 ziliendeshwa kwa makundi tofauti ili kuelimisha jamii katika Mapambano dhidi ya Rushwa.
Jumla ya Mikutano 7 ya hadhara ilifanyika ikiwa na madhumuni ya kuelezea athari za Rushwa na jinsi ya Kupambana nayo. Jumla ya Klabu 10 za wapinga Rushwa katika Shule za Sekondari zilitembelewa kwa lengo la kuziimarisha na kupatiwa mafunzo.
Ndugu Wanahabari,
Uchunguzi na Mashtaka:
Kwa upande wa uchunguzi na Mashtaka, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Manyara tulipokea jumla ya malalamiko (57) kwa mchanganuo ufuatao;
- Idara ya Elimu katika Halmashauri zote yalikuwa Malalamiko Matano (05)
- Idara ya Afya ni malalamiko Manne (04)
- Watu Binafsi pamoja na Mashirika binafsi yalikuwa ni Manne (04)
- Malalamiko dhidi ya Wenyeviti na watendaji wa Vijiji na Kamati mbalimbali za Vijiji yalikuwa ni Thelathini na tatu (33)
- Malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi yalikuwa ni Matatu (03)
- Idara ya Maliasili Malalamiko matatu (03)
- Malalamiko dhidi ya vyama vya Ushirika yalikuwa ni lalamiko Moja (01)
- Mahakama malalamiko matatu (3)
- Mshirika ya Dini lalamiko moja (1)
- Huduma za Barabara ( TARURA) lalamiko moja (1)
- Malalamiko dhidi ya Mabaraza ya Ardhi ni Matatu (03)
Kati ya malalamiko hayo, Malalamiko (19) hayakuhusiana na vitendo vya Rushwa na hivyo wahusika walishauriwa ipasavyo na yale yanayohusiana na rushwa yapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi. Vilevile, katika kipindi hiki cha Oktoba hadi Desemba 2021, kesi (8) zilifunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea Mahakamani kuwa (33).
Ndugu Wanahabari,
Mikakati ya Januari – Machi 2022:
Katika kipindi cha Januari-Machi, 2022, tutaendelea na mafunzo ya walimu watakaowafundisha vijana wa Skauti kuhusu elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na kuendelea na jukumu la kudhibiti vitendo vya rushwa kwa kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika mkoa wetu.
RAI yetu kwa Wanamanyara ni kuwaomba kuendelea kutoa taarifa za rushwa na wanaojihusisha na vitendo hivyo, kupitia namba yetu ya dharura 113 au kwa kufika katika ofisi zetu zilizo karibu nao, kama sehemu ya kuunga mkono kauli mbiu isemayo : “KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LANGU”
Imetolewa na:
HOLLE J. MAKUNGU
MKUU WA TAKUKURU (M)
MANYARA
SIMU: 0738150124