Ukusanyaji wa mapato ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Lengo la Serikali ni kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea
na kupunguza kwa kadri inavyowezekana utegemezi kutoka kwa Wadau wa Maendeleo (DPs) na kuhakikisha kuwa mipango ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini inatekelezwa bila kukwama. Serikali imekuwa ikikusanya mapato kwa kutumia mashine za POS (Point of Sale) tangu mwaka 2016. Hata hivyo, watumiaji wa mfumo huu wanalalamikiwa kwa kuendelea kuipotezea Serikali mapato. Kwa sababu hiyo, TAKUKURU ilifanya uchambuzi wa mfumo wa POS kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa inayosababisha upotevu wa mapato ya Serikali. Uchambuzi huu ulihusisha halmashauri 32 za mikoa 20 ya Tanzania bara ambayo ni Tanga, Tabora, Geita, Arusha, Mbeya, Dodoma, Shinyanga, Lindi, Morogoro, Mwanza, Kagera, Ruvuma, Dar es Salaam, Mara, Pwani, Singida, Manyara, Njombe, Rukwa na Kilimanjaro