TAKUKURU MKOA WA MOROGORO YAENDELEA NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Ndugu WanaHabari,
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Nichukue fursa hii kuwatakieni Heri ya Mwaka Mpya wa 2022 kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutukutanisha tena tukiwa na afya njema.
Vile vile niwashukuru sana kwa kuitikia wito wetu ili muweze kuujulisha umma kazi zilizotekelezwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kuanzia mwezi Oktoba 2021 hadi Desemba 2021.
Ndugu WanaHabari,
Tarehe 29 mwezi Oktoba mwaka 2021 nilikupokutana nanyi hapa kwa ajili ya kuuhabarisha umma juu ya utendaji kazi wa TAKUKURU kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Septemba 2021 nilieleza kwamba miongoni mwa vipaumbele vitakavyoshughulikiwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2021 hadi Desemba 2021 ni pamoja na:- Kufuatilia fedha kiasi cha shilingi Bilioni Kumi na Nne na Milioni Mia Moja na Arobaini (Tsh 14,140,000,000) zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Mia Saba na Saba (707) kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022; kuendeleakufuatilia fedha zilizotolewa na Serikali kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro zinazohusiana na ugonjwa wa UVIKO 19 ili ziweze kutumika kama zilivyokusudiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UVIKO 19; Kuendelea kutoa elimu ya vitendo vya rushwa kwa wananchi na watumishi wa umma kupitia mikutano ya hadhara, semina nk ili waweze kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutokomeza vitendo vya rushwa. Kuendelea na uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na tuhuma za ununuzi na usambaji wa madawa na vifaa tiba katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali. Aidha tutaendelea kufuatilia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ndugu WanaHabari
Uchunguzi na Mashtaka
Katika kipindi cha Mwezi Oktoba 2021 hadi Disemba 2021, tulipokea jumla ya taarifa 111 na kati ya hizo, taarifa 60 zinahusiana na vitendo vya rushwa na uchunguzi wake uko katika hatua mbalimbali ambapo taarifa 51 hazikuhusiana na vitendo vya rushwa. Kati ya taarifa 51 zisizohusu rushwa, taarifa moja ilihamishiwa idara nyingine na taarifa 50 watoa taarifa walishauriwa jinsi ya kufuatilia malalamiko yao pamoja na kuwatatulia kero zao kwa kuwapeleka kwenye mamlaka husika.
Katika taarifa hizo jumla ya Sekta 15 zililalamikiwa huku sekta iliyoongoza katika kulalamikiwa ikiwa ni Watendaji wa Vijiji/Mitaa & Kata kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini:-
NA | SEKTA LALAMIKIWA | IDADI |
1 | WATENDAJI WA VIJIJI, MITAA & KATA | 30 |
2 | SEKTA BINAFSI | 17 |
3 | MABARAZA YA ARDHI WILAYA & KATA | 9 |
4 | ELIMU | 9 |
5 | TAMISEMI – UTAWALA | 7 |
6 | MAHAKAMA | 5 |
7 | ARDHI | 4 |
8 | AFYA | 8 |
9 | POLISI | 6 |
10 | AMCOS/USHIRIKA | 5 |
11 | TAASISI ZA FEDHA | 4 |
12 | MAJI | 3 |
13 | MASHIRIKA YA UMMA | 2 |
14 | VYAMA VYA WAFANYAKAZI | 1 |
15 | MAENDELEO YA JAMII | 1 |
JUMLA | 111 |
Katika kipindi tajwa, kesi mpya Tatu (03) zimefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya kesi 24 zinazoendelea Mahakamani. Pia katika kipindi hicho Jamhuri ilishinda kesi nne (4) mahakamani.
Ndugu WanaHabari,
Elimu kwa Umma
Katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2021 hadi Desemba 2021, kupitia Dawati la Elimu kwa Umma, tumeweza kufanya jumla ya Mikutano ya Hadhara pamoja ya Mijadala ya Wazi Thelathini na Nne (34), tumefanya semina kwa wananchi na watumishi wa umma Arobaini (40), tumeimarisha klabu za wapinga rushwa wa shule za msingi, sekondari na vyuo Arobaini na Saba (47), tumeandaa na kurusha vipindi vya Redio na TV Vitatu (03), Tumeshiriki katika maonesho Mawili (02), Uandishi wa Makala Mbili (02) pamoja nautoaji wa habari kwa umma kupitia vyombo vya habari Moja (01).
Ndugu WanaHabari
Elimu inayotolewa kwa wananchi kwa njia TAKUKURU INAYOTEMBEA inawawezesha kutoa kero zao ambazo zinapatiwa majibu na wahusika. Mfano tarehe 14.11.2021 TAKUKURU INAYOTEMBEA ilikutanana na wananchi wa Kijiji cha Mkambalani kufuatia kuwepo kwa kero ya upatikanani wa maji. Kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA wananchi waliweza kutoa kero zao ambazo zilipatiwa ufumbuzi kutoka kwa viongozi na watendaji wa Kamati ya Maji. Tunashukuru wanahabari ambao mlishiriki katika mkutano huo na kisha kujulisha umma kupitia vyombo vyenu.
Rai ya TAKUKURU Mkoa wa Morogoro ni kuwaomba wananchi washiriki kwa wingi wao pindi mikutano ya hadhara inapoitishwa katika maeneo yao ili waweze kutumia haki yao ya kuelimishwa pamoja na kutoa kero zao katika Mikutano ya hadhara, mijadala ya wazi na TAKUKURU INAYOTEMBEA.
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Morogoro iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa nikuwajenga vijana katika misiki ya Uzalendo, Uwajibikaji na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
Ndugu WanaHabari
Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
Katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, tulifanikiwa kufuatilia jumla ya Miradi ya Maendeleo 14 yenye thamani ya Shilingi Bilioni Tano, Milioni mia Nne Themanini na Moja, Laki Mbili Sabini na Nane Elfu Mia Moja Sitini na Tano na Senti Nne kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NA | JINA LA MRADI | MAHALI ULIPO | THAMANI (SHS.) |
1 | Ufuatiliaji wa matengenezo ya barabara | Manispaa ya Morogoro | 476,298,544.00 |
2 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Mkoa wa Morogoro | 86,023,074.00 |
3 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Manispaa ya Morogoro | 57,106,061.14 |
4 | Ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Uchindile | Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba | 250,000,000.00 |
5 | Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mlimba | Wilaya ya Mlimba | 1,300,000,000.00 |
6 | Ujenzi wa Miradi wa maji Mbingu | Wilaya ya Mlimba | 400,000,000.00 |
7 | Ufuatiliaji wa Mradi wa maji Kata ya Dakawa | Wilaya ya Mvomero | 309,265,537.00 |
8 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Wilaya ya Mvomero | 71,968,6676.00 |
9 | Ujenzi wa shule ya Sekondari Berega. | Wilaya ya Kilosa | 1,000,000,000.00 |
10 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Wilaya ya Kilosa | 66,492,970.00 |
11 | Ukamilishaji wa maabara shule ya Sekondari Rubeho | Wilaya ya Gairo | 26,376,000.00 |
12 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Wilaya ya Gairo | 39,896,727.34 |
13 | Ujenzi wa barabara ya Lugala hadi Misegese na Malinyi hadi Igawa | Wilaya ya Malinyu | 720,405,000.00 |
14 | Ufuatiliaji wa fedha za UVIKO 19 | Wilaya ya Malinyi | 29,727,575.56 |
JUMLA | 5,481,278,165.04 |
Katika ufuatiliaji huo tumebaini uwepo wa mapungufu madogo madogo ambapo wahusika wameshauriwa kuyarekebisha na utekelezaji wa marekekebisho hayo unaendelea.
Ndugu WanaHabari
Ufuatiliaji wa matumizi ya Fedha za Mpango wa Maendedeleo kwa Ustawi wa Taarifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19
Kama mnavyofahamu, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fedha nyingi kwa ajili ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, Mkoa wa Morogogo ulipokea zaidi ya shilingi Bilioni Kumi na Sita kwa ajili ya sekta za Afya na Elimu. Katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, tulifanikiwa kufuatilia Miradi yenye thamani Shilingi Bilioni Kumi na Sita, Milioni mia moja na Kumi (Shs. 16,110,000,000.00). Miradi hiyo inahusisha vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, vyumba vya madarasa katika shule shikizi, bweni na Kituo cha Afya. Jedwali lifuatalo linaonyesha miradi iliyokaguliwa:-
NA | JINA LA MRADI | MAHALI ULIPO | THAMANI (SHS.) |
1 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 86 | Manispaa ya Morogoro | 1,720,000,000.00 |
2 | Ujenzi wa Bweni la watoto wenye mahitaji maalum shule ya msingi Kihonda | Manispaa ya Morogoro | 80,000,000.00 |
3 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 103 | Halmashauri ya Morogoro | 2,060,000.00 |
4 | Ujenzi wa madarasa shule shikizi 11 | Halmashauri ya Morogoro | 220,000,000.00 |
5 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 42 | Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga | 840,000,000.00 |
6 | Ujenzi wa madarasa shule shikizi 24 | Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga | 480,000,000.00 |
7 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 34 | Wilaya Malinyi | 680,000,000.00 |
8 | Ujenzi wa madarasa shule shikizi 44 | Wilaya ya Malinyi | 880,000,000.00 |
9 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 107 | Wilaya ya Mvomero | 2,140,000,000.00 |
10 | Ujenzi wa madarasa shule shikizi 15 | Wilaya ya Mvomero | 300,000,000.00 |
11 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 78 | Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba | 1,560,000,000.00 |
12 | Ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Uchindile | Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba | 250,000,000.00 |
13 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 55 | Wilaya ya Gairo | 1,140,000,000.00 |
14 | Ujenzi wa madarasa shule shikizi 2 | Wilaya ya Gairo | 40,000,000.00 |
15 | Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari 186 | Wilaya ya Kilosa | 3,720,000,000.00 |
JUMLA | 16,110,000,000.00 |
Ndugu Wanahabari,
Baada ya ufuatiliaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU huchukua hatua zifaazo kulingana na kinachobainika katika ufuatiliaji huo ikiwemo; kushauri au kujadiliana na wadau husika kuhusu namna ya kuondoa upungufu uliobainika ili thamani ya fedha ifikiwe.
Katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hii inayotekelezwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 mkoani Morogoro, yapo mapungufu ya kitaalamu yaliyobainishwa ambayo yangeachwa yangeweza kusababisha mianya ya rushwa. TAKUKURU ilifanya warsha na kujadili mapungufu hayo na wadau husika na tayari marekebisho yanaendelea kufanyika.
Ndugu WanaHabari
Uchambuzi wa Mifumo
Katika kipindi cha Oktoba 2021 hadi Desemba 2021 TAKUKURU Mkoa wa Morogoro tumefanya chambuzi za mifumo Kumi na Mbili (12) zinazohusiana na Ukusanyaji wa ushuru wa mazao ya Kilimo; mianya ya rushwa katika asilimia kumi (10%) ya mikopo kwa Akinamama, Vijana na Walemavu; Mianya ya rushwa katika usimamizi wa mtihani katika vyuo vya kati;
Mianya ya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu Msingi na Sekondari; Mianya ya rushwa katika utendaji wa huduma za ununuzi Serikalini GPSA.
Aidha jumla ya Warsha nne (4) zilifanyika katika maeneo yafuatayo:- Rushwa ya ngono katika sekta ya elimu Msingi na sekondari; Mianya ya rushwa katika matumizi ya mafuta GPSA; Mianya ya rushwa katika usimamizi wa mitihani vyuo vya kati na Rushwa katika utendaji wa Wakala wa huduma za ununuzi Serikalini GPSA.
Mapungufu machache yaliyobainika katika uchambuzi huu yalibainishwa na kujadiliwa kwa pamoja na TAKUKURU pamoja na wadau husika na tayari marekebisho yameanza kufanyika.
Ndugu WanaHabari
Mikakati ya vipaumbele kwa kipindi cha januari 2022 – machi 2022
Katika kipindi cha Januari 2022 hadi Machi 2022 tumejiwekea mikakati mbalimbali kama ifuatavyo;
Kwanza, tunaendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa jamii kupitia mpango wa TAKUKURU INAYOTEMBEA kwa kufanya mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi. Mpango huu umesaidia kuwafikia wananchi hususani walioko pembezoni mwa miji ambao hutumia fursa ya kutoa kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao. Nitoe rai kwa wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi zaidi pindi mikutano hiyo inapoitishwa na TAKUKURU. Pia tutaendelea kutoa elimu kupitia Mpango wa Ushirikiano kati ya TAKUKURU na SKAUTI – TAKUSKA.
Pili, tutaendelea na uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na ununuzi na usambaji wa madawa na vifaa tiba katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali ambapo uchunguzi wake uko katika hatua mbalimbali.
Tatu, Serikali yetuinaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Hivyo tutaendelea kwa ukaribu kufuatilia miradi hiyo ili kuhakikisha kwamba kuna thamani ya fedha katika miradi hiyo. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wasimamizi wa miradi ya maendeleo wote kuwa waaminifu na wadilifu katika kutekeleza majukumu yao. TAKUKURU haitasita kuchukua hatua dhidi ya wote watakaofuja fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Ndugu WanaHabari,
Ninatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika katika ofisi zetu ambazo ziko kila wilaya au kwa kupiga simu ya bure 113, ujumbe mfupi wa maandishi *113# au kupiga simu kwa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro namba 0738150143 na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Namba 0738150144. Aidha wananchi waliopo Wilayani wanaweza kuwasiliana na Wakuu wa TAKUKURU Wilaya kwa namba zifuatazo :- Kilombero 0738 150 145, Kilosa 0738 150 146 ; Mvomero 0738 150 147, Ulanga 0738 150 148; Malinyi 0738150149 na Gairo 0767 531 177.
Vile vile niwatake wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano pindi watakapohitajika kwa ajili ya ushahidi Mahakamani.