TAKUKURU MBEYA YASHIRIKIANA NA SKAUTI KATIKA UZUIAJI RUSHWA
Ndugu Wanahabari.
Leo tumekutana tena katika ofisi yetu ya TAKUKURU mkoa wa Mbeya ili kupitia ninyi tuweze kuuhabarisha umma kuhusu utendaji kazi wa ofisi yetu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi wa Oktoba 2021 hadi Disemba 2021.
Kwa mujibu kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007, TAKUKURU inayo majukumu makuu matatu ambayo ni; Kuelimisha Jamii kuhusu rushwa na madhara yake; Kufanya chambuzi za mifumo kwenye taasisi za umma na sekta binafsi pamoja na kufanya uchunguzi na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kufikisha watuhumiwa mahakamani.
Ndugu Wanahabari
Ushirikiano na SKAUTI
Katika kipindi hiki, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya kupitia ushirikiano wa TAKUKURU NA CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA (TAKUSKA), ilifanya kazi kubwa mbili ambazo ni zifuatazo:
- Kuandaa Mpango wa Kazi wa namna ya kutekeleza Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundisha Vijana wa Skauti kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa na
- Kuendesha Mashindano ya Ligi ya Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete na Mchezo wa Kuvuta Kamba – TAKUSKA SUPPER CUP.
Ndugu Wanahabari
Tarehe 15/11/2021, Mpango wa Kazi wa kutekeleza Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundisha Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa ulizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera. Uzinduzi wa Mpango wa Kazi huo ulienda sambamba na kupewa mafunzo kwa Viongozi wa Skauti kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.
- Mafunzo yalitolewa na Maafisa Uchunguzi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Mbeya ambapo wakuu wa madawati ya Uzuiaji Rushwa, Elimu kwa Umma, Uchunguzi na Intelijensia yaliwasilisha mafunzo hayo.
- Mada zilizowasilishwa ni:
- Madhara ya Rushwa katika jamii pamoja na
- Namna ya kutoa taarifa TAKUKURU kwa kazi za TAKUSKA.
Jumla ya washiriki katika mafunzo haya walikuwa ni 95 ambapo wavulana ni 65 na wanawake 30.
- Mashindano ya TAKUSKA SUPER CUP yalizinduliwa rasmi tarehe 22/12/2021 katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Iyunga, Mgeni Rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Dkt. Mohamed Rashid Chuachua.
- Mashindano haya yameshirikisha jumla ya Tarafa tano za Wilaya ya Mbeya ambazo ni Tarafa ya Iyunga, Sisimba, Usongwe, Tembela na Isangati.
- Michezo iliyoshindanishwa ni Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Kuvuta Kamba, Mashairi, Nyimbo pamoja na Ngonjera.
- Lengo la mashindano ya TAKUSKA SUPER CUP lilikuwa ni kuhamasisha vijana kujiunga na SKAUTI pamoja na Klabu za Wapinga Rushwa ili wapewe mafunzo na elimu ya mapambano dhidi ya rushwa. Tunafanya hivyo tukiamini kuwa vijana hao wakielimika wataweza kuibua taarifa za vitendo vya rushwa katika jamii ikiwemo taarifa zitakazohusu utekelezaji wa Miradi itakayojengwa chini ya kiwango.
- Pili ni kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa washiriki wa michezo na jamii inayofika katika sehemu/viwanja vya michezo kushuhudia michezo hiyo.
- Kupitia mashindano TAKUSKA Super Cup imefanikiwa kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa katika mikutano kumi (10) na vipindi vya redio vitano kwenye tarafa tano ambapo jumla ya vijana 1055 wamejiunga na skauti na jumla ya wananchi 1624 walipata elimu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Ndugu Wanahabari
UCHUNGUZI
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2021, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imeweza kutekeleza majukumu yake ya uchunguzi na kufanikiwa kupokea jumla ya taarifa mpya 109 za tuhuma za rushwa na makosa mengine. Taarifa 69 zilihusu rushwa na taarifa 40 hazikuhusu rushwa.
Taarifa 63 zilizohusu rushwa zimefunguliwa majalada ya uchunguzi.
- Majalada sita (6) yamekamilika
- Majalada matano (5) yamepelekea kufungua majalada ya kesi mahakamani,
- Majalada hamsini na mbili (52) uchunguzi wake unaendelea
Katika taarifa arobaini (40) ambazo hazikuhusu rushwa, taarifa 22 watoa taarifa wake walielimishwa na kushauriwa mamlaka sahihi ya kuwasilisha taarifa zao na taarifa kumi na nane (18) zilihamishiwa idara nyingine.
Mchanganuo wa kisekta na idadi kwa malalamiko yote 109 iko kama ifuatavyo kwenye jedwali hapo chini
Na | Idara | Idadi |
1 | Halmashauri | 20 |
2 | Mahakama | 12 |
3 | Polisi | 5 |
4 | Afya | 8 |
5 | Sekta binafsi (wafanyabiashara) | 20 |
6 | Ardhi | 12 |
7 | Mashirika ya Umma | 12 |
9 | Vyama vya Ushirika | 4 |
10 | Ujenzi | 2 |
15 | Maliasili | 5 |
16 | Elimu | 7 |
17 | Fedha | 2 |
Jumla | 109 |
Ndugu Wanahabari
MASHTAKA
Kwa upande wa Mashtaka, katika kipindi hiki, tumeweza kufungua kesi mpya kumi na mbili (12) Mahakamani kwa makosa mbalimbali na kufanya tuwe na kesi 57 zilizoendeshwa mahakamani katika kipindi tajwa. Hata hivyo Katika kipindi hicho kesi zilizoamuliwa mahakamani ni 18 ambapo kati ya hizo TAKUKURU imeshinda kesi 12 na kushindwa kesi 6.
Ndugu Wanahabari
UZUIAJI RUSHWA
Katika kipindi cha Oktoba – Desemba 2021, kwa upande wa Uzuiaji Rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imefanikiwa kufanya chambuzi za mfumo sita (6) ambazo zilifanyika katika Sekta ya Elimu katika Shule za Msingi na Sekondari, Usimamizi wa Mitihani katika Vyuo vya Kati na Utawala.
Mapungufu yaliyobainika ni kutokuzingatiwa kwa Mwongozo wa Usimamizi wa Mitihani. Ili kuidhibiti hali hiyo, Kikao kati ya TAKUKURU Mkoa wa Mbeya na wadau husika kilifanyika na kuweka mikakati ya namna ya kurekebisha mapungufu haya.
Ndugu Wanahabari
Vilevile, katika kipindi tajwa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya ilifuatilia utekelezaji wa miradi 44 ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni saba, milioni miatatu na themanini na sita, laki tano ishirini na saba, mia nane themanini na mbili nukta sita tisa (7,386,527,882.69) katika Sekta za Afya, Elimu, Maji na Barabara ikiwemo miradi inayotekelezwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19 (Maarufu Miradi ya UVIKO). Lengo la ufuatiliaji huu lilikuwa ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa, inatekelezwa kwa wakati ikiwa na ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Miradi ya Maendeleo endelevu inategemea rasilimali fedha na bidhaa, nguvu kazi, mawazo na ushiriki wa dhati na adilifu wa kila mwananchi, asasi za kiraia, sekta binafsi, asasi zisizo za Serikali, nchi wahisani na Serikali. Kila mmoja kati ya wadau hawa ana wajibu wa kuzuia na kupambana na rushwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha malengo ya miradi ya maendeleo yanafikiwa. Ikumbukwe kuwa maendeleo ya nchi huletwa na wananchi wenyewe, ambao ni wewe na mimi.
Mapungufu yaliyobainika katika ufuatiliaji wa miradi hiyo yanahusisha maeneo yafuatayo:
- Ujazaji wa vitabu vya kuingiza na kutolea vifaa vya ujenzi;
- Uchelewaji wa kuanza kwa ujenzi jambo ambalo hupelekea ujenzi kuchelewa kumalizwa kwa wakati na kusababisha huduma kuchelewa kutolewa kwa wananchi.
TAKUKURU mkoa wa Mbeya ilitoa ushauri ikiwa ni njia moja wapo ya kufanya uzuiaji wa vitendo vya rushwa kutokea hivyo mapungufu hayo yalifanyiwa kazi. Vilevile, elimu imetolewa kwa wadau husika kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa iliyopo na kuimarisha usimamizi wa miradi hiyo hasa kwa kusisitiza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Manunuzi ya Umma.
Katika hatua nyingine, katika kipindi tajwa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya ilianzisha operation maalumu ambayo imepewa jina la KATA KWA KATA katika Kata za Itezi, Nonde, Ilomba, Nsalaga na Sisimba.
Kata hizo zote ni za Wilaya ya Mbeya.
Katika kata hizo tumefanya yafuatayo:
- Utambuzi wa Miradi ya Serikali Kuu,
- Utambuzi wa Miradi inayoendeshwa na Halmashauri kupitia fedha za ndani,
- Utambuzi wa Miradi inayoendeshwa na wafadhili,
- Tumepokea taarifa za malalamiko ya wananchi dhidi ya Rushwa na
- Tumebainisha vyanzo vya mapato ya fedha katika kata hizo.
Baada ya kufanya utambuzi wa miradi hiyo na kuchambua nyaraka mbalimbali, pamoja na mambo mengine, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya ilibaini kuwa fedha za utekelezaji wa Miradi hazina usimamizi mzuri na hivyo kufikia hatua ya kutotumika kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa.
Ili kuziba mwanya huo ambao ungeweza kusababisha uwepo wa rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Mbeya imewaelimisha wahusika wakuu katika usimamizi wa fedha za miradi na pia taarifa ya changamoto hii inaandaliwa ili kuona iwapo kuna haja ya kuanzisha uchunguzi.
Ndugu Wanahabari
ELIMU KWA UMMA
TAKUKURU Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha miezi mitatu imeendelea na jukumu la kuelimisha umma kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii, lengo likiwa ni kuendelea kuwajengea uelewa wa madhara ya rushwa, ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kupitia uelimishaji huo tumeweza kuwafikia wananchi 2,913 ambao walipata elimu kupitia Semina 11 zilizoandaliwa, Mkutano wa hadhara 01, Maonesho 6 na Klabu za wapinga rushwa 07 za shule za msingi na sekondari – zilizoimarishwa.
Ndugu Wanahabari
TAKUKURU INAYOTEMBEA
TAKUKURU Mkoa wa Mbeya iliendelea na zoezi la kutembelea wananchi katika maeneo yao kwa lengo la kusikiliza kero za rushwa. Katika kipindi cha miezi mitatu tumefanikiwa kupokea kero mbalimbali za rushwa na makosa mengine. Kwa zile taarifa ambazo hazihusiani na rushwa tumekuwa tukiziwasilisha kwenye Mamlaka husika ili ziweze kufanyiwa kazi na wananchi kupewa mrejesho. Kwa kipindi tajwa tumefika katika Kata za Itewe, Kambikatoto pamoja na Lupa.
Ndugu Wanahabari
MATARAJIO YETU KWA KIPINDI CHA MIEZI MITATU IJAYO.
Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kuanzia Januari hadi Machi 2022 tumejipanga kufanya mambo yafuatayo: –
- Kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu rushwa na madhara yake katika usimamizi wa miradi ya maendeleo katika Kata, Mitaa na Vijiji, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata uelewa na kuweza kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa karibu na kutoa taarifa TAKUKURU pale wanapoona ubadhirifu.
- Tutaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa TAKUSKA katika mkoa wetu ili tuwafikie vijana wengi zaidi.
- Tutaendelea kufanya kazi za uzuiaji rushwa kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika maeneo mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi na kushauri namna bora ya kuiziba mianya hiyo.
Pia natoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Mbeya, kutoa ushirikiano wa wakati wa kutekeleza miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pindi utakapo hitajika.
- Tutaendelea kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote watakao kutwa na tuhuma za vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.
- Pamoja na Serikali kuweka sheria nyingi na kali bado taaarifa nyingi ambazo zimekuwa zikipokelewa kwenye ofisi za TAKUKURU (M) Mbeya zimekuwa zikiwagusa sana Watendaji wa Kata, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa na viongozi wengine wa ngazi ya Kata.
- Baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia udhaifu wa wananchi kutojua sheria na hivyo kuwakandamiza au kuwanyima haki zao za msingi. Hivyo TAKUKURU Mkoa wa Mbeya itaendesha operation ya KATA KWA KATA ili kubaini yafuatayo:-
- Kuchunguza ufanisi wa matumizi ya sheria na miongozo mbalimbali iliyotolewa kuhusu uongozi kwenye ngazi ya Kata.
- Kubaini mianya ya rushwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya viongozi wa Kata za mkoa wa Mbeya.
- Kubaini changamoto za upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kwenye ngazi ya kata.
- Kubaini thamani ya fedha katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye kata ikilinganishwa na hali halisi ya mradi unavyoonekana.
- Kubaini vitendo na ubadhirifu wa fedha ambavyo vinaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Na. 11/2007
- Kubaini aina ya elimu ya rushwa inayohitajika kuwapatia wananchi wa kata husika.
Ndugu Wanahabari
Baada ya kusema hayo, nipende kuwapongeza wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya kwa jinsi wanavyoendelea kushirikiana na TAKUKURU katika kufichua vitendo vya rushwa. Ninawasihi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, nasi tunaahidi kuzifanyia kazi taarifa tutakazo zipokea kwa wakati.
Imetolewa na:
DENIS MANUMBU
MKUU WA TAKUKURU MKOA WA MBEYA
Nambari ya simu: SIMU BURE 113
MKUU WA TAKUKURU (M) 0738 150137
NAIBU MKUU WA TAKUKURU (M) 0738 150 138