TAKUKURU LINDI YAFANYA UFUATILIAJI WA MIRADI YENYE THAMANI YA Tsh. 12,277,340,040/= PAMOJA NA KUSHIRIKISHA WAKUU WA WILAYA KATIKA WARSHA NA MAJADILIANO YA KUFANIKISHA MAFUNZO KWA WAWEZESHAJI WA KUFUNDISHA VIJANA (SKAUTI) KUHUSU KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA.
Ndugu wanahabari,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi inajumuisha ofisi za TAKUKURU Lindi Mkoani pamoja na zilizoko katika wilaya za Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa.
Tumeendelea kutekeleza majukumu yetu katika robo ya pili (2) ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoanzia Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021, kama yanavyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 Marejeo 2019. Majukumu yetu yalitekelezwa kupitia madawati mbalimbali ikiwemo Dawati la Uchunguzi, Huduma za Sheria na Mashtaka, Uzuiaji Rushwa pamoja na Elimu kwa Umma.
Ndugu wanahabari,
Dawati la Uchunguzi, kwa kipindi cha Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Lindi imepokea jumla ya taarifa za malalamiko 65. Kati ya taarifa hizo, 34 zilihusu tuhuma za Rushwa na taarifa 31 hazikuhusu Rushwa. Kati ya taarifa hizo 34 zilizohusu Rushwa majalada 15 yamefunguliwa majalada ya uchunguzi na 19 zipo katika uchunguzi wa awali. Aidha katika kipindi tajwa majalada 5 yamekamilika. Taarifa 31 zisizohusu rushwa zimehamishiwa katika idara nyingine kwa hatua zaidi.
Malalamiko hayo 65 kwa ujumla wake yalihusu sekta mbalimbali zikiwemo: Elimu (4), Ardhi (9), Kilimo/Ushirika (7), Afya (19), Fedha (4), Sheria (1), Tamisemi (2), Binafsi (3), Ujenzi (5), Utawala (6), Maji (1), Biashara (1), Habari (1) na Barabara (2).
Ndugu wanahabari,
Kwa upande wa mashtaka katika kipindi cha Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021, TAKUKURU (M) Lindi ilifanikiwa kufungua mashauri 3 katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi na Kilwa kwa tuhuma za makosa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 marejeo ya mwaka 2019, pamoja na sheria nyinginezo. Aidha hadi sasa jumla ya mashauri kumi (12) yanaendelea kusikilizwa mahakamani na yapo katika hatua mbalimbali.
Ndugu wanahabari,
Jukumu lingine la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ufuatiliaji huu unalenga kubainisha yafuatayo: Mianya ya rushwa; Ucheleweshaji wa utekelezaji; Uvujaji; na Ushirikishwaji wa wananchi/wadau.
Mtiririko wa fedha hufuatiliwa kutoka chanzo (Hazina, wafadhili au vyanzo vya ndani) mpaka kwenye mradi husika (utekelezaji wa mradi) ili kubaini yaliyotajwa hapo juu. Aidha, TAKUKURU huchukua hatua zifaazo kulingana na kinachobainika katika ufuatiliaji, zikiwemo: Kushauri au kujadiliana na wadau kuhusu namna ya kuondoa upungufu uliobainika ili thamani ya fedha ifikiwe; Kuelimisha wananachi/wadau; Kufanya uchambuzi wa mifumo; na Kuanzisha uchunguzi.
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu (3) Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021, TAKUKURU Mkoa wa Lindi kupitia Dawati la Uzuiaji Rushwa ilifuatilia matumizi ya fedha za Miradi kumi na tisa (19) ya Maendeleo yenye jumla ya thamani ya Shilingi 12,277,340,040/= kama ifuatavyo:
A: MIRADI ILIYOKAGULIWA KISEKTA
- SEKTA YA KILIMO
Jumla ya miradi 8 ilikaguliwa kwa kipindi hiki.
- Ujenzi wa vituo 8 vya Rasilimali za Kilimo halmashauri ya wilaya ya Ruangwa yenye thamani ya milioni 148,087,587/=
- SEKTA YA AFYA
Jumla ya miradi 2 ilikaguliwa kwa kipindi hiki katika Sekta ya Afya.
- Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Liwale yenye thamani ya Tsh. 894,752,090/=.
- Ujenzi wa Kituo cha Afya Ngongowele halmashauri ya wilaya ya Liwale yenye thamani ya Tsh. 250,000,000/=.
- SEKTA YA UJENZI
Jumla ya mradi 1 ulikaguliwa kwa kipindi hiki katika Sekta ya Ujenzi.
- Ujenzi wa Barabara ya Ujenzi (0.47 km) kwa Kiwango cha Lami halmashauri ya wilaya ya Liwale yenye thamani ya Tsh. 250,000,000/=
- SEKTA YA ELIMU
Jumla ya miradi 8 ilikaguliwa kwa kipindi hiki katika Sekta ya Elimu.
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 58 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya wilaya ya Mtama vyenye thamani ya Tsh. 1,160,000,000/=
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 56 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya manispaa ya Lindi vyenye thamani ya Tsh. 1,120,000,000/=
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 98 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya wilaya ya Kilwa vyenye thamani ya Tsh. 2,560,000,000/=.
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 34 na bweni 1 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya wilaya ya Ruangwa vyenye thamani ya Tsh. 1,100,000,000/=.
- Ujenzi wa Majengo ya Chuo cha Ufundi VETA halmashauri ya wilaya ya Ruangwa yenye thamani ya Tsh. 2,114,500,363/=.
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 69 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya wilaya ya Nachingwea vyenye thamani ya Tsh. 1,380,000,000/=.
- Ujenzi wa vyumba vya madarasa 64 kwa fedha za UVIKO halmashauri ya wilaya ya Liwale vyenye thamani ya Tsh. 1,300,000,000/=.
Yaliyobainika:
Mapungufu yaliyobainika katika Ukaguzi wa miradi hiyo ni ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi; thamani ya fedha kwa baadhi ya miradi kutolingana na hali halisi; ukiukwaji wa taratibu za manunuzi pamoja na ushirikishwaji mdogo wa wadau.
Mapungufu haya ambayo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa, yameweza kufanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika pamoja na kutoa elimu, kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa iliyopo na kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha (Value for money).
B: UIMARISHAJI WA MIFUMO
Uimarishaji wa mifumo hufanyika kwa kufanya uchambuzi wa mifumo, kuweka mikakati ya kudhibiti mianya ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa mikakati. Uimarishaji wa mifumo uliofanyiwa kazi kwa kipindi hiki ni uchambuzi wa mfumo katikaUdhibiti wa mianya ya Rushwa katika Mfumo wa utoaji huduma wa Shirika la Umeme (TANESCO) Wilaya ya Ruangwa.
Kupitia uchambuzi huu, ipo mianya ya rushwa iliyobainishwa ambayo kupitia warsha tulikaa na wadau kujadili matokeo ya uchambuzi wetu na kuwekeana maazimio ya namna bora ya kuondokana na mianya hiyo ya rushwa.
Ndugu wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba, 2021 hadi Desemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Lindi imeendelea kutekeleza malengo yake ya Dawati la Elimu kwa Umma kwa kuwaelimisha wananchi wa makundi mbalimbali na wadau wengine kuhusu rushwa na madhara yake kwa mtu mmoja mmoja, jamii, taasisi na taifa kwa ujumla.
TAKUKURU Mkoa wa Lindi imeendesha semina 16, imefanya mikutano ya hadhara 36. Pia TAKUKURU (M) Lindi imefanya uimarishaji wa klabu za wanafunzi za wapinga rushwa 44, na Utoaji wa makala au uandishi wa habari 6.
Ushirikiano na SKAUTI:
Katika kipindi hiki, kwa kutambua umuhimu wa kundi la vijana hasa waliopo shuleni na vyuoni katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa nchini, TAKUKURU mkoa wa Lindi imefanya utambulisho wa mwongozo wa mafunzo kwa wawezeshaji wa kufundisha vijana kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa ngazi ya wilaya kwa kushirikisha wakuu wa wilaya kwa lengo la kuwafikia vijana wengi zaidi ili kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Aidha wakati wa utambulisho huu ilifanyika warsha na majadiliano ya namna ya kufanikisha mafunzo ya wawezeshaji na wadau wengine ambapo washiriki kwa kila wilaya walikuwa Mkuu wa wilaya, Katibu Tawala wa wilaya, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Mkuu wa TAKUKURU(W), Kamishina wa skauti wilaya, Maafisa elimu msingi na sekondari, maafisa wa
TAKUKURU wilaya na Skauti rika wilaya.
Ndugu wanahabari
TAKUKURU INAYOTEMBEA:
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 katika kufahamu na kuzifanyia kazi kero za wananchi TAKUKURU imeendelea na mpango wa TAKUKURU INAYOTEMBEA. Kwa kutekeleza mpango huu, TAKUKURU Mkoa wa Lindi huambatana na baadhi ya Wakuu wa Idara za Halmashauri ili kuweza kutatua kero za wananchi papo kwa papo na zile ambazo zinakuwa hazina majibu ya mara moja, huchukuliwa na kufanyiwa kazi na majibu kutolewa.
Katika mpango huu, wananchi wengi wamejitokeza na kulalamikia matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi katika maeneo ya Kata na Vijiji, ikiwemo kutopewa taarifa juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao pamoja na kutosomwa kwa mapato na matumizi ya miradi inayosimamiwa na ngazi ya vijiji na kata. Aidha migogoro ya ardhi isiyoisha, tozo mbalimbali za Halmashauri, kuchelewa kupata malipo ya mazao yao baada ya kuuzwa na ubadhirifu wa viongozi ni miongoni mwa kero kubwa.
TAKUKURU mkoa wa Lindi ikishirikiana na idara za Halmashauri na mamlaka zingine inaendelea kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayoibuliwa kufuatia mpango huu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA.
Aidha hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwaagiza viongozi wa ngazi ya vijiji na kata kubandika kwenye mbao za matangazo miradi inayotekelezwa, kusomwa kwa mapato na matumizi ya miradi inayosimamiwa katika maeneo ya vijiji na kata pamoja na Mkurugenzi kuyajengea uwezo Mabaraza ya Ardhi ya Kata kupitia Wanasheria wa Halmashauri ili mabaraza haya yaweze kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria.
Ndugu wanahabari,
MIKAKATI YA JANUARI – MACHI 2022
Katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 inayoanza Januari, 2022 hadi Machi 2022, TAKUKURU Mkoa wa Lindi imejipanga katika kuendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa fedha za Miradi ya Majina na ujenzi wa barabara chini ya TARURA inayotekelezwa katika Halmashauri zote ndani ya mkoa wa Lindi.
Pia Mkoa umejipanga kukamilisha chunguzi zinazotokana na taarifa mbalimbali zikiwemo taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na nyinginezo.
Kwa upande wa uelimishaji umma, sambamba na kuendelea kuelimisha umma kuhusu madhara yatokanayo na vitendo vya rushwa, pia katika kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwafikia vijana wengi zaidi, TAKUKURU mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na wadau wengine ndani ya mkoa, itaendelea na mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundisha Vijana wa Skauti kuhusu kuzuia na kupambana na Rushwa pamoja na kutoa ushauri wa kitalaam kwa lengo la kuwezesha ufundishaji wa vijana wa Skauti ili wawe waadilifu, wawajibikaji na wazalendo kuanzia ngazi yake binafsi, katika familia, shuleni, jamii na Taifa ikiwa ni mkakati uliopo kati ya TAKUKURU na CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA.
Ndugu wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Lindi inaendelea kuwashukuru wananchi, vyombo vya habari, pamoja na taasisi mbalimbali (binafsi na za serikali) katika Mkoa wa Lindi, kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa ofisi zetu ikiwepo kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya rushwa. Aidha, tunawaomba wananchi na wadau wote waendelee kutuunga mkono kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia simu yetu ya dharura namba 113 bure, kwani mapambano dhidi ya rushwa si ya TAKUKURU peke yake bali ni ya jamii nzima kwa ujumla.
Imetolewa na:
Eng. Abnery J. Mganga
Mkuu wa TAKUKURU (M) Lindi
0738 150 118