TAKUKURU (M) KIGOMA YAFUNGUA KESI TANO NA KUFANYA UFUATILIAJI WA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 11
Ndugu WanaHabari
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuchunguza na kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kuwafikisha washitakiwa Mahakamani, kufanya Utafiti na Udhibiti wenye lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa na kuwahamasisha kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
MASHTAKA:
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021 TAKUKURU (M) Kigoma imefanikiwa kufungua mashauri mapya matano (5) ya makosa ya rushwa na Uhujumu Uchumi na kufanya idadi ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa kumi na tatu (13). Aidha katika kipindi hicho jumla ya mashauri matatu (3) yalitolewa maamuzi ambapo Jamhuri ilishinda.
Katika kipindi tajwa TAKUKURU (M) Kigoma imepokea jumla ya malalamiko 79. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 57 yalikuwa ni ya vitendo vya rushwa na malalamiko 22 hayakuhusu rushwa.
Katika malalamiko 57 yaliyohusu rushwa, malalamiko 40 yanaendelea kufanyiwa kazi katika hatua mbalimbali, malalamiko 17 uchunguzi wake umekamilika ikiwa ni pamoja na majalada matatu 3 ambayowatuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Malalamiko 22 ambayo hayakuhusu rushwa, watoa taarifa walishauriwa na kuelekezwa sehemu stahiki za kupata utatuzi wa kero zao.
Mchanganuo wa kisekta kwa malalamiko 79 yaliyopokelewa ni kama ifuatavyo: TAMISEMI (52), Ardhi (4), Sekta binafsi (4), Elimu (3), Ujenzi (3), Utawala (3), Ushirika (3), Mahakama (2), Afya (2), Jeshi la Polisi(2) na NSSF (1).
Ndugu WanaHabari
UZUIAJI RUSHWA:
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 TAKUKURU (M) Kigoma imefanikiwa kufanya kazi za ufuatiliaji wa rasilimali za umma kwenye miradi 97 yenye thamani ya shilingi 11,178,362,763.9 ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na thamani ya fedha kupatikana. Kazi hizo zilifanyika katika sekta za Elimu, Afya Maji. Barabara na Kilimo.
Kati ya miradi hiyo, miradi 88 yenye thamani ya Shillingi 7,748,512,606.47 ni miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko- 19
Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hiyo ambayo ni ya kuto kuzingatia taratibu za manunuzi ya umma, yameweza kufanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika na kuwashauri kuboresha eneo hilo. Pia elimu ilitolewa kwa wadau husika kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa na kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha (Value for money).
Aidha katika kipindi hiki TAKUKURU Mkoa wa Kigoma ilifanya ufuatiliaji na uchambuzi wa mifumo 3 katika utendaji wa Wakala wa Huduma za Ununuzi wa Umma Serikalini (GPSA), uchambuzi wa mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na uchambuzi wa mfumo wa vihatarishi vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu.
Kutokana na uchambuzi huo, TAKUKURU Mkoa wa Kigoma ilibaini kasoro za kiutendaji za kutozingatia miongozo iliyopo. Ili kutatua tatizo hilo, TAKUKURU (M) Kigoma ilifanya vikao 3 vya wadau na kujadili mapungufu yaliyobainika hasa katika Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) pamoja na mfumo wa usimamizi wa mitihani katika vyuo vya kati na mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Ndugu WanaHabari
UELIMISHAJI UMMA:
Kwa upande wa uelimishaji umma, TAKUKURU Mkoa wa Kigoma imeendelea na jukumu la kuongeza uelewa wa elimu ya rushwa na maadili kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, sambamba na kuendelea kuwahamasisha ili waweze kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021 TAKUKURU (M) Kigoma imeweza kuwafikia wananchi kwa kufanya semina 43, mikutano ya hadhara 40, uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa 72, ufunguzi wa klabu za wapinga rushwa2, maonesho 6 na vipindi vya redio 2. Jumla ya wananchi 22,564 walinufaika na elimu hiyo wanaume wakiwa 12,673 na wanawake 9,891.
Aidha TAKUKURU (M) Kigoma kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la TACARE, iliweza kutoa elimu ya rushwa na maadili katika utunzaji wa mazingira, kwa wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Kasuku kilichopo katika Kata ya Simbo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma. Lengo lilikuwa ni kuwajengea uwezo na uelewa wa vitendo vya rushwa ili kuhakikisha wanashiriki katika kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyosababisha uharibifu wa mazingira.
Elimu hiyo ilitolewa katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kasuku ikiwashirikisha wananfunzi wa shule ya msingi Bondo, Kusuku, walimu wa shule hizo na wananchi wa Kijiji cha Kasuku.
Pamoja na elimu iliyotolewa, wanufaika wa elimu husika, walishiriki katika zoezi la kupanda miti 180 ya matunda na mbao katika shule ya Msingi Kasuku, Bondo na shule mpya ya Sekondari ya Kasima ambapo kila shule ilipandwa miti 60. Miti hiyo ilitokana na kitalu kilichoanzishwa na kutunzwa na wanachama wa Klabu ya wapinga rushwa shule ya msingi Kasuku.
Huu ni mkakati wa shule hiyo kuimarisha klabu za wapinga kwa shule za sekondari na msingi zilizojirani na shule hiyo ambapo kila shule itapatiwa miti 60 bure kwa masharti ya kwamba lazima shule iwe na klabu ya wapinga rushwa itakayohusika na utunzaji wa miti hiyo. TAKUKURU kwa ufadhili wa shirika la TACARE lililopo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji iliwezakukabidhi viliba vyenye uwezo wa kuotesha miti 9,200 ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanafunzi hao.
Ndugu WanaHabari
TAKUKURU INAYOTEMBEA:
Katika kutatua kero za wananchi, TAKUKURU (M) Kigoma kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA imefanikiwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao kwa lengo la kutoa elimu, kusikiliza kero zao na kutafuta ufumbuzi wa kero zao. Kero nyingi zilizotolewa na wananchi zilihusu tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali za vijiiji kutosoma taarifa ya mapato na matumizi, baadhi ya Wakuu wa Shule za Sekondari kuwatumikisha wanafunzi kufanya kazi za ujenzi ikiwa ni pamoja na kuchimba visiki, kusomba mchanga na matofali ilihali kazi hizo zikiwa zimetengewa fedha.
Fedha zilizotengwa kulipwa kwa walimu ambao huzitumia kwa masilahi binafsi. Kero nyingine iliyowasilishwa ni kuhusu ubadhirifu wa fedha za Serikali katika miradi ya maji na afya, ambayo imetumia fedha nyingi bila matokeo chanya kwa wananchi. Kufuatia malalamiko haya, TAKUKURU (M) Kigoma kupitia ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Uvinza, imeanzisha uchunguzi wa awali katika miradi hiyo ya maji na afya iliyolalamikiwa, aaambayo ipo katika vijiji vya Sunuka, Lulinga na Rukoma wilayani Uvinza.
TAKUKURU Mkoa wa Kigoma imeendelea kutafuta ufumbuzi wa kero hizi za wananchi kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Wakala husika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Maeneo yaliyotembelewa na TAKUKURU INAYOTEMBEA ni pamoja na Kijiji cha Nyarubanda katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma, kijiji cha Sunuka, Mgambazi, Rukoma na Rulinga katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Ndugu WanaHabari
USHIRIKIANO NA WADAU:
Katika kukuza ushirikiano na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa, TAKUKURU kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania (M) Kigoma imefanikiwa kuutambulisha kwa viongozi ngazi ya mkoa na wilaya Mwongozo wa Mafunzo kwa wawezeshaji wa kufundisha vijana wa Skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa.
Lengo la ushirikiano huu ni kupanua wigo wa kupambana na rushwa ili kujenga jamii inayozingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na uzalendo pamoja na kulinda rasilimali za umma ikiwemo miradi ya maendeleo.
MIKAKATI YA TAKUKURU MKOA WA KIGOMA JANUARI – MACHI 2022:
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2022, TAKUKURU (M) Kigoma itaendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inajengwa kwa viwango vinavyotakiwa na pia itaratibu vikao vya wadau ili kujadili utatuzi wa changamoto/ mapungufu yaliyobainika katika uchambuzi wa mfumo kwenye utendaji wa Wakala wa Huduma za Ununuzi wa Umma Serikalini (GPSA) na uchambuzi wa mfumo kuhusu vihatarishi vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu
Ndugu WanaHabari
Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2022 TAKUKURU itashirikiana na Chama cha Skauti Mkoa wa Kigoma kuwaelimisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa ili kupanua wigo wa mapambano dhidi ya rushwa katika jamii.
Aidha kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA, kero za wananchi zitapokelewa, elimu ya madhara ya rushwa katika jamii na katika miradi ya maendeleo itatolewa sambamba na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kuwa na utayari wa kutoa ushahidi mahakamani pale wanapotakiwa kufanya hivyo.
WITO
Ndugu WanaHabari
TAKUKURU (M) Kigoma inatoa wito kwa wananchi kuiona rushwa kama janga la Taifa linalohitaji nguvu ya pamoja kupambana nalo. Hivyo wanaaswa kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa na utayari wa kufika Ofisi za TAKUKURU zilizo karibu ili kutoa taarifa za vitendo vya rushwa. Pia wananchi wanaombwa kuwasiliana na ofisi za TAKUKURU katika Mkoa wa Kigoma kwa Simu ya Bure 113 inayopatikana kupitia mitandao ya TTCL, AIRTEL, VODACOM, TIGO, HALOTEL pindi wanapokuwa na taarifa za vitendo vya rushwa ili hatua za stahiki ziweze kuchukuliwa.
Asanteni kwa kunisikiliza.
STEPHEN P. MAFIPA
MKUU WA TAKUKURU (M) KIGOMA
0738150103