TAARIFA YA UTENDAJI KAZI KWA KIPINDI CHA
MWEZI OKTOBA-DISEMBA 2021
Ndugu Wanahabari,
Kwa mara nyingine tena nawakaribisha sana katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Katavi.
Ndugu Wanahabari,
Lengo kuu la kukutana kwetu ni kutoa taarifa ya utendaji kazi wa ofisi yetu yaTAKUKURU Mkoa wa Katavi kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo ni kuanzia Oktoba hadi Disemba, 2021.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi hicho cha Oktoba – Disemba, 2021, TAKUKURU Mkoa wa Katavi imetekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 kama ifuatavyo:-
ELIMU KWA UMMA
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2021, katika kutekeleza jukumu lake la kuelemisha na kushirikisha umma katika mapambano dhidi ya rushwa, ofisi yaTAKUKURUmkoa wa Kataviimefanya mikutano 28 ya hadhara katika Wilaya za Mpanda, Mlele na Tanganyika Mkoani Katavi, lengo likiwa ni kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wao wa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya Rushwa. Pia tumefanya vipindi viwili (2) vya Redio, kufungua, kuimarisha klabu (19) za wapinga rushwa katika Shule za Msingi na Sekondari na kufanya maonyesho matatu (3).
Katika maadhimisho ya SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU tarehe 10 Disemba 2021, ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliadhimisha siku hiyo kwa kwenda kutembelea kituo cha Watoto yatima cha Mtakatifu YOHANE PAULO II kilichopo Halmashauri ya Manispaa Mpanda eneo la Nsemlwa na kutoa msaada wa vyakula Mchele kilo 50, unga wa ngano kilo 25, Chumvi, Mafuta ya kula lita 25, nyama kilo 8, biscuits, juisi, miswaki, dawa za meno pamoja na “Pampers”.
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Katavi uliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu umekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa kwakuw ayeye ndiye mlezi wa Skauti katika mkoa husika. Mwongozo huu tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa nikuwajenga vijana katika misiki ya Uzalendo, Uwajibikaji na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
UZUIAJI RUSHWA
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2021, TAKUKURU Mkoa wa Katavi imefanya kazi ya ufuatiliaji wa fedha za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo yenye jumla ya thamani ya shilingi 67,500,000/= ambapo miradi hiyo ni ifuatayo:
- Umaliziaji wa madarasa mawili katika shule ya msingi Shikizi Halmashauri ya Manispaa Mpanda wenye thamani ya shs. 25,000,000/=;
- Umaliziaji wa madarasa mawili katika shule ya msingi Misunkumilo iliyoko Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wenye thamani ya ya sh. 2,500,000/= ;
- Ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Igalula Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika wenye thamani ya sh.40,000,000/=;
Lengo la ufuatiliaji huu ni kuangalia iwapo kuna mianya ya Rushwa kwenye utekelezaji wa miradi na kuongeza uwazi na upatikanaji wa thamani ya fedha kwenye miradi ya Serikali ili kuboresha huduma kwenye shughuli za Serikali. Mapungufu machache yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hii ambayo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa, yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika pamoja na kuwapa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa. Elimu hii pia itasaidia katika kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha (Value for money).
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Katavi, imefuatilia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule za sekondari na vituo shikizi namba. 5441, chini ya Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19, zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Kupitia mpango huu, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele ilipokea jumla ya shs. 680,000,000/=.
Katika kusimamia mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko aliunda timu za ufuatiliaji katika Halmashauri hiyo iliyoongoza na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Bw. Faustine Maijo. Katika ufuatiliaji huo timu hiyo iliweza kufuatilia ujenzi wa vyumba 34 vya madarasa, madawati 360, meza 433 na viti 412, ambapo katika jumla ya kiasi kilichopokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, timu hiyo iliweza kuokoa kiasi cha sh.100,724,838.00 na kupelekea Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Filberto Hassan Sanga kumtunuku Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa cheti cha usimamizi bora.
UCHAMBUZI WA MIFUMO
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU mkoa wa Katavi, imefanya Uchambuzi wa mfumo wa utendaji wa watendaji wa Sekta ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe lengo likiwa ni kupunguza vitendo vya Rushwa ya ngono vinavyotokana na matumizi mabaya ya madaraka.
UCHUNGUZI
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba, 2021 jumla ya malalamiko 51 yalipokelewa, kati ya hayo malalamiko 39 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 12– hayakuhusisha vitendo vya Rushwa. Kutokana na malalamiko 12 ambayo hayakuhusu rushwa, walalamikaji walihitaji ufafanuzi zaidi na walieleweshwa, kushauriwa na wengine walielekezwa mahali sahihi pa kupeleka malalamiko yao hasa Polisi na Mahakamani.
Mchanganuo wa malalamiko 51 yaliyopokelewa kwa kipindi hicho ni kama ifuatavyo-:
SN | IDARA/SEKTA | IDADI |
2 | AMCOS | 6 |
3 | Binafsi | 9 |
4 | Polisi | 1 |
5 | Elimu | 2 |
6 | Mahakama | 2 |
7 | TAMISEMI | 11 |
8 | TARURA | 1 |
9 | Afya | 3 |
10 | Mazingira | 1 |
11 | Ulinzi | 1 |
12 | Ardhi | 1 |
13 | Maji | 1 |
14 | Taasisi za fedha | 2 |
15 | Makazi ya wakimbizi | 1 |
16 | TANESCO | 1 |
17 | Siasa | 1 |
18 | Serikali za vijiji | 5 |
19 | TRA | 1 |
20 | TFS | 1 |
JUMLA | 51 |
Katika kipindi hicho uchunguzi wa majalada (03) ulikamilika, kesi nne (04) zilifunguliwa mahakamni na kesi moja (01) iliamuliwa Mahakamani na mtuhumiwa alipatikana na hatia.
MIKAKATI KWA KIPINDI CHA JANUARI – MACHI 2022
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Januari – Machi, 2022, TAKUKURU Mkoa wa Katavi tunatarajia kuongeza nguvu katika uchunguzi wa malalamiko yanayopokelewa hasa yanayohusu ubadhirifu wa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Halmashauri zote na kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika Kupambana na Rushwa na kutoa taarifa zinazohusiana na vitendo vya Rushwa kwa TAKUKURU.
Kwa upande wa Uchambuzi wa mifumo, TAKUKURU Mkoa wa Katavi itafanya Uchambuzi wa mfumo juu ya utendaji kazi wa maafisa watendaji wa kata na vijiji, ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na mianya ya rushwa katika miradi ya barabara inayosimamiwa na TARURA.
Vilevile, kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022, TAKUKURU Mkoa wa Katavi itafanya uelimishaji wa jamii hususan kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU na Chama cha Skauti nchini – TAKUSKA unaolenga kuwafikia vijana wengi zaidi katika mkoa wetu.
WITO:
Ndugu Wanahabari,
Mwisho natoa shukurani kwenu Wanahabari kwa ushirikiano wenu mkubwa katika Mapambano dhidi ya Rushwa. Aidha, TAKUKURU Mkoa wa Katavi inatoa wito kwa jamii ya wana-Katavi kwa ujumla kutokujihusisha na vitendo vya kijinai kama kuomba na kupokea rushwa za aina zozote zile.
Hivyo tunatoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kupiga simu ya bure 113 na *113# au kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia namba 113 au kupiga simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa ambayo ni 0738-150096 au kufika katika ofisi za TAKUKURU iliyo karibu nawe.
Pia bado kumeendelea kuwa na wimbi la matapeli wanaojifanya ni maafisa wa TAKUKURU ambao hupiga simu kwa watu mbalimbali wakitoa maelekezo na maagizo kwa watu hao ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuripoti ofisi fulani ya TAKUKURU au kutaka kuonana na wahusika.
Tunatoa wito na rai kwa jamii na watumishi wote ambao ikitokea wamepigiwa simu na matapeli hao basi wajiridhishe na ofisi ya TAKUKURU iliyoko karibu na maeneo yao au kupiga simu ya bure 113 na *113# au kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia namba 113 na simu rasmi za TAKUKURU Mkoa wa Katavi ambazo ni 0738150096, 0738150098 (Mlele) na 0738150099 (Tanganyika). Usikubali kutapeliwa, toa taarifa TAKUKURU ili mhalifu huyo aweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwani ni kosa la kisheria kujifanya wa TAKUKURU.
Kwa pamoja tushirikiane kuitokomeza rushwa
TANZANIA BILA RUSHWA INAWEZEKANA NA KAZI IENDELEE
Imetolewana:
Festo Mdede
MKUU WA TAKUKURU (M)
KATAVI.
0738-150096