- UTANGULIZI
Ndugu wanahabari,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera tumeendelea kutekeleza majukumu yetu kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, namba 11 ya Mwaka 2007. Katika utekelezaji wa majukumu yetu tumeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya Rushwa wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla. Aidha majukumu haya yametekelezwa katika wilaya zote zilizopo chini ya Mkoa wa Kagera ambazo ni Bukoba, Misenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba.
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu yaani kuanzia tarehe 01/10/2021 hadi 31/12/2021, TAKUKURU Mkoa wa Kagera tumeweza kufanya kazi mbalimbali kama ifuatavyo;-
- UZUIAJI RUSHWA
Ndugu wanahabari,
Mojawapo ya majukumu ya TAKUKURU ni kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo (PETS). Lengo kuu la ufuatiliaji huu ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha inapatikana kwa kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wa rasilimali katika utekelezaji wake.
Pia ufuatiliaji huu huwezesha kubainisha mapema mianya ya rushwa, ucheleweshaji, uchepushaji au uvujaji wa fedha, ushirikishwaji wa wananchi au wadau na hatimaye kupelekea hatua za haraka kuchukuliwa kwa miradi itakayobainika kuwa na mapungufu mbalimbali kama vile kuanzisha uchunguzi, kutoa elimu kwa umma na kufanya chambuzi za mifumo inayohusu utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa kufanya haya inasaidia miradi inayotekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa au kutumika katika mradi husika.
Ufuatiliaji huu hufanyika kwa kufuatilia mtiririko wa fedha kutoka chanzo (Hazina, Wafadhili au Vyanzo vya ndani) mpaka kwenye mradi husika, ili kubaini yaliyotajwa hapo juu. Aidha katika kutekeleza jukumu hili tumekuwa tukifanya ufuatiliaji na uchambuzi wa mifumo na kisha kushauri namna bora ya kuzuia mianya ya rushwa katika utekelezaji wa miradi
Ndugu wanahabari,
Kwa kipindi hiki cha miezi mitatu, katika jukumu la Uzuiaji Rushwa tumeweza kufanya tafiti nane (8) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera na kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo hamsini na tano (55) yenye thamani ya jumla ya shilingi Bilioni kumi na nne, millioni mia tano tisini na mbili mia mbili hamsini na tano elfu mia tatu sabini na moja (Shs 14.592, 255,371)
Miradi tuliyofuatilia ni miradi ya ukarabati wa miradi ya maji, ujenzi wa Hospitali, vituo vya afya, zahanati pamoja na ujenzi wa madarasa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa wa Mapambano Dhidi ya Uviko 19. Aidha tafiti hizo na ufuatiliaji ulilenga kuthibitisha thamani ya fedha (Value for Money) katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kubaini mianya ya rushwa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kushauri namna ya kuziba mianya hiyo.
Kazi hii ya uzuiaji rushwa kama ilivyo kwa kazi zingine imefanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Kagera. Aidha katika miradi iliyofanyiwa ufuatiliaji, ipo miradi iliyobainika kuwa na mapungufu ikiwemo ya kutumia vifaa vyenye ubora tofauti na ilivyoelekezwa na BOQ. Kuna miradi ilibainika kutumia kioo cha 4mm badala ya 5mm; Kulikuwa na uwekaji mbaya wa vigae (Tiles) kutokana na usimamizi hafifu wa kihandisi; Viti kutengenezwa pungufu na ilivyokadiriwa kwa maelezo kuwa fedha hizo hazikutosha; pia kulibainika mapungufu ya kutoweka kumbukumbu za utoaji wa vifaa kutoka stoo na vifaa vya umeme kuuzwa kwa bei kubwa kuliko bei ya soko.
Baada ya ufuatiliaji huu, imetolewa elimu kwa wahusika wa miradi hii ili kuboresha kasoro hizo zilizojitokeza na tayari maboresho yanafanyika.
- UCHUNGUZI
- Utangulizi
Ndugu wanahabari,
Katika kipindi hiki cha miezi mitatu, tumeweza kupokea jumla ya malalamiko mia moja sabini na tatu (173). Kati ya malalamiko hayo, malalamiko mia moja na orobani na tisa (149) yalikuwa ni malalamiko yasiyohusu rushwa, hivyo walalamikaji walielimishwa na kupewa ushauri na hakukuwa na taarifa iliyohamishiwa idara nyingine.
Aidha malalamiko (24) yalihusu rushwa na kufunguliwa majalada ya uchunguzi. Kati ya majalada hayo 24, uchunguzi wa majalada 6 umekamilika na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa. Majalada 18 uchunguzi wake unaendelea.
Aidha idara zinazolalamikiwa kutokana na taarifa 173 zilizopokelewa ni kama ifuatavyo:- Taarifa 91 ni kutoka Halmashauri za Mkoa wa Kagera ambapo maeneo yanayolalamikiwa kupitia taarifa hizi yanahusu Sekta ya ardhi 33, sekta ya afya 10, sekta ya fedha 12, Idara ya Elimu 6,maendeleo ya jamii 9, ugavi 18, na watendaji wa kata na vijiji 4. Taarifa zingine 82 zilihusu watu binafsi 28, taasisi za kifedha 11, mashirika binafsi (NG”O) 5, Polisi 13, Uhamiaji 8, Mahakama 3, TANESCO 9 na Mabaraza ya Ardhi 5.
Vilevile katika kipindi hiki tumeweza kufungua mashauri mapya Saba (7) mahakamani na kufanya jumla ya mashauri arobaini na nane (48) yanayoendelea kusikilizwa mahakamani mkoani Kagera.
- Mapambano Dhidi ya Matapeli Wanaojifanya Maafisa wa TAKUKURU
Ndugu wanahabari
Katika miaka ya hivi karibuni vimejitokeza vitendo vya baadhi ya watu wanaojipatia fedha kutoka kwa wananchi kwa njia za udanganyifu. Kwamba watu hao wamekuwa wakiwapigia simu wananchi na kujitambulisha kuwa wao ni mafisa wa TAKUKURU na kwamba ili waweze kutochunguza tuhuma zinazowakabili watoe fedha. Baadhi ya wananchi wameingia kwenye mtego na wametoa fedha kwa matapeli hao.
Ndugu wanahabari
Hapa nitaeleza mfano mmoja:
Mnamo tarehe 9/11/2021 tapeli anayejitambulisha kwa jina la BRUNO SELLA, alikutana na wakazi wawili wa Wilaya ya Karagwe nakujitambulisha kuwa yeye ni Afisa wa TAKUKURU mkoa wa Kagera anayechunguza tuhuma zinazowakabili.
Tapeli huyo aliwaeleza wakazi hao, ambao pia ni viongozi wa Chama cha Ushirika cha Nguvumali kilichopo Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera, kwamba ili aache kuchunguza tuhuma zinazowakabili ndani ya TAKUKURU Mkoa wa Kagera, inabidi wampatie fedha kiasi cha sh. 2,000,000/=.
TAKUKURU Mkoa wa Kagera ilifanya uchunguzi dhidi ya suala hili ambapo tarehe 16/12/2021 TAPELI BRUNO SELLA alikamatwa na Maafisa wa TAKUKURU mkoa wa Kagera, akipokea fedha hizo.
Mtuhumiwa BRUNO SELLA amefikishwa mahakamani kwa makosa ya kujifanya Afisa wa TAKUKURU na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Tunatoa shukrani kwa watoa taarifa wetu ambao tulishirikiana na kumkamata tapeli huyo na tunawasisitiza WanaKagera kuwa makini na kutokubali kutapeliwa.
- UELIMISHAJI UMMA
- Utangulizi
Ndugu wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Kagera tunaamini kuwa Elimu ni tendo lenye athari katika akili, maarifa au maumbile ya mwanandamu na kwamba ni nyenzo muhimu katika kupitisha maarifa na maadili kutoka katika kundi moja kwenda kundi jingine, au kutoka katika kizazi kimoja kwenda kingine au kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Hivyo, ili kuongeza uelewa wa wana Kagera katika mapambano dhidi ya rushwa msisitizo wetu umekuwa katika kutoa elimu katika makundi mbalimbali yenye kuhamasisha wananchi kutambua madhara ya rushwa, pamoja na namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika maeneo ya kazi na biashara, lengo likiwa ni kuifanya jamii ifahamu maana ya rushwa, vyanzo vyake na madhara yake katika jamii na kushiriki kikamilifu katika mapambano haya.
Katika kuhakikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa inawafikia watu wengi hapa mkoani Kagera, TAKUKURU mkoa wa Kagera imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia-;
- Vyombo vya habari vya Radio zilizoko katika mkoa wetu, ambapo tumeweza kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja.
- Semina: Tumekuwa tukielimisha umma kupitia semina na tumekuwa tukifanya na kushiriki semina katika ofisi za umma na binafsi na hata mashuleni. Katika kipindi cha miezi mitatu tumeweza kufanya semina arobaini na sita (46) katika Mkoa wa Kagera.
- Mikutano ya hadhara: Njia hii imekuwa ikitusaidia katika uelimishaji ikiwa ni pamoja na kutumia utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA ambapo tumekuwa tukiwafuata wananchi na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali kama Masoko, Magulio pamoja na Vituo vya mabasi (Stendi). Kupitia utaratibu huu tumeweza kufanya mikutano ya hadhara (45) katika mkoa mzima.
- Kushiriki maonesho: Katika Mkoa wetu wa Kagera tumeshiriki katika maonyesho ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021 tangu tarehe 02.10.2021 hadi 08.10.2021 na Nanenane pamoja na magulioni na kuweza kufikisha ujumbe wetu ambapo tumeweza kushiriki jumla ya maonyesho nane (8) katika kipindi cha miezi mitatu.
- USHIRIKIANO NA WADAU Skauti
Mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu na hivyo katika kuhakikisha kuwa jamii nzima na makundi mbalimbali ya watanzania yanashiriki kikamilifu katika mapambano haya, TAKUKURU Mkoa wa Kagera tumeimarisha ushirikiano baina yetu na Chama cha Skauti Tanzania
Kama mnavyofahamu, Chama cha Skauti Tanzania ni chama cha hiari cha kielimu chenye wajibu wa kumlea na kumkuza kijana kiimani, kiakili, kijamii na kimwili kwa kutumia shughuli za Skauti ili kujenga dunia iliyo bora zaidi – hivyo ushikiano na chama hiki utatusaidia sana katika kujenga jamii yenye watu waadilifu. Aidha kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Tanzania, malengo yetu ni kutumia chama hiki katika kutoa elimu kwa vijana kupitia vijana wenzao wa Skauti na kwa bahati nzuri tayari tumeweza kufungua Klabu ya wapinga rushwa ya wanachama wa Skauti hapa mkoani Kagera. Hivyo ni imani yetu kuwa kwa kukuza ushikiano na chama hiki, tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi walioko mashuleni na walioko mtaani ambao ni rahisi kufikiwa na vijana wenzao wa Skauti.
- Wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo
Sanjari na kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Tanzania, pia tumeendelea kuimarisha ushirikiano na kundi la vijana hasa wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo kupitia kufungua na kuimarisha Klabu za wapinga rushwa mashuleni.
Kwa sasa tuna klabu za wapinga rushwa takriban katika shule zote za Msingi, Sekondari na Vyuo vilivyoko katika Mkoa wetu. Klabu hizi zimekuwa zikitusaidia katika kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na uadilifu kwa vijana tukiamini kuwa kundi hili ni muhimu katika mapambano dhidi ya Rushwa, kwamba vijana wakilelewa katika misingi ya uadilifu tutapata viongozi bora wa Taifa la kesho.
Tumelenga kushughulika na kundi la vijana kwani tunaamini vijana ni hazina na rasilimali muhimu ya taifa na chachu ya maendeleo.
- VIPAUMBELE KWA KIPINDI CHA Januari – Machi, 2022
Ndugu Wanahabari
Pamoja na utekezaji wa majukumu yetu ya kawaida pia tumejiwekea malengo ya kutekeleza vipaumbele vifuatavyo:-
I. Kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika Ujenzi wa miradi ya maendeleo ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi.
Pia kama mtakumbuka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano Mkuu maalum wa ALAT Septemba 27, 2021 jijini Dodoma alisema. Ninanukuu
“Bado kuna shida kwenye thamani ya fedha Kwa miradi mnayoitekeleza, fedha nyingi zinakuja kwenu lakini miradi haifanani na fedha zinazotolewa. Pamoja na kwamba tutaendelea kuleta fedha naagiza thamani ya fedha katika miradi tunayoitekeleza ionekane.” Mwisho wa kunukuu.
Kauli hii imetuongezea ari na kasi ya ufuatiliaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Pia tumeweka kipaumbele katika chunguzi za Vyama vya Ushirika kwani katika Vyama vya Ushirika taarifa mbalimbali zinaonyesha kuna kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ufujaji wa mali za ushirika. Vilevile, tumejipanga kuongeza kasi uchunguzi katika ubadhilifu wa fedha za makusanyo ya mapato ya ndani katika Halmashari.
- Kuongeza kasi ya uelimishaji umma kwa kutumia njia mbalimbali mfano kushiriki katika maonyesho kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania, maadhimisho ya wiki ya sheria kuanzia tarehe 23.01.2022 hadi tarehe 01/02/2022 yatakayofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba na katika matamasha ya uelimishaji, semina, mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi pamoja na kuendelea kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa mashuleni. Vilevile kutoa elimu kwa viongozi wa dini ili katika mahubiri yao waendelee kukemia vitendo dhidi ya rushwa.
- Kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi kama maeneo ya utoaji wa huduma kwa wananchi na katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa katika miradi ya Sekta ya Elimu, Ununuzi, Kilimo, Afya, uchukuzi pamoja na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika.
- Tutaendelea kuelimisha jamii na hususani kundi la vijana kupitia ushirikiano uliopo kati ya TAKUKURU na SKAUTI – TAKUSKA.
- HITIMISHO
Ndugu wanahabari,
Mapambano dhidi ya rushwa ni ya kila mwana Kagera, hivyo ili kuufanya Mkoa wa Kagera kuwa sehemu isiyokuwa na rushwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mapambano haya. Hivyo ninawaomba wana Kagera wote tuendeleee kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja na tuwe mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na tuendelee kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Aidha nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wana Kagera wote ambao wamekuwa na wanaendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa kutoa taarifa ambazo zimekuwa zikifanikisha kuwabaini wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na hatimaye hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao. Kila mmoja wetu anahitaji kutanguliza maslahi ya nchi na kuchukua hatua katika kukabiliana na tatizo la rushwa katika Mkoa wetu. Vilevile, tukumbuke kwamba Rushwa ni adui wa haki na inaweza kuathiri mgawanyo wa rasilimali katika jamii na kusababisha wananchi kukata tamaa.
Hivyo ni wajibu wa kila Mwana Kagera kuchukua hatua ya kutoa taarifa TAKUKURU, pale anapoona kuna dalili ya vitendo vya rushwa kufanyika.
Imetolewa na
Signed
EZEKIA SINKALA
KAIMU MKUU WA TAKUKURU (M)
Simu: 0738 15 00 89