TAKUKURU MKOA WA KILIMANJARO YAMULIKA MIRADI YA UJENZI WA MADARASA
Niawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na pia nawatakia heri ya mwaka mpya wa 2022 wanahabari na wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjaro.
Ndugu wanahabari, leo tumewaita ili kuwapatia habari ya utendaji kazi wetu kwa miezi mitatu yaani Mwezi Oktoba 2021 hadi Desemba 2021.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2021 imetekeleza majukumu yake ya uchunguzi, kuelimisha, pamoja na kuzuia vitendo vya rushwa, kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007.
UCHUNGUZI
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi hicho cha miezi mitatu, TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro tulipokea taarifa Mia moja na ishirini na sita (126) ambapo kati ya hizo, taarifa Sabini na mbili (72) zilikuwa zinahusu makosa ya rushwa na hamsini na nne (54) hazikuwa na uhusiano na makosa ya rushwa hivyo watoa taarifa walielimishwa na kuhamishiwa katika mamlaka nyingine ambazo wana mamlaka ya kushughulikia tuhuma hizo.
Mchanganuo kisekta ya malalamiko yaliyopokelewa ni kama ifuatavyo;
S/N | IDARA HUSIKA | IDADI YA TUHUMA |
1 | ELIMU | 14 |
2 | SERIKALI ZA MITAA | 13 |
3 | POLISI | 05 |
4 | SEKTA BINAFSI | 14 |
5 | MAHAKAMA | 09 |
6 | ARDHI | 12 |
7 | NISHATI NA MADINI | 02 |
8 | AFYA | 05 |
9 | USHIRIKA | 03 |
10 | TAMISEMI | 40 |
11 | MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII | 05 |
12 | UHAMIAJI | 01 |
JUMLA | 126 |
Taarifa zilizohusu rushwa ni – 72.
- Taarifa zinazoendelea na uchunguzi ni – 61
- Taarifa ambazo uchunguzi umekamilika na kupelekea kufungua kesi mahakamani ni – 03
- Taarifa ambazo zimefungwa kwa kukosekana ushahidi ni – 08
Taarifa ambazo hazikuhusu rushwa ni – 54
- Taarifa ambazo wahusika wameelimishwa na kushauriwa ni – 41
- Taarifa ambazo zimehamishiwa Idara nyingine ni – 13
Katika kipindi cha Oktoba – Disemba 2021, kesi mpya zilizofikishwa mahakamani ni nane (8) na kufanya kuwa na jumla ya mashauri (23) yanayoendelea mahakamani. Katika kipindi hicho Jumla ya mashauri mawili (2) yalitolewa hukumu na Jamhuri ilishinda mashauri hayo.
TAARIFA YA UFUATILIAJI WA MATUMIZI, YA FEDHA YA MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19.
Ndugu Wanahabari,
Mkoa wa Kilimanjaro ulipokea kiasi cha shilingi 6,738,843,000 toka Serikali Kuu, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kama ilivyofanywa katika mikoa mingine ya Tanzania, kwa mchanganuo ufuatao kiwilaya.
- Wilaya ya Mwanga ilipokea kiasi cha shilingi 240,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12 katika shule za sekondari na shule ya msingi shikizi na majengo hayo yameonekana kujengwa vizuri.
- Halmashauri ya wilaya ya Rombo ilipokea kiasi cha shilingi milioni 880,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 44 ujenzi huo upo kwenye hali nzuri.
- Wilaya ya Hai ilipatiwa kiasi cha shilingi 860,000,000/=.kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 43 ya shule za sekondari mbalimbali ujenzi huo umekamilika na upo katika hali nzuri
- Wilaya ya Siha ilipatiwa jumla ya shilingi 640,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 32 ujenzi huo ulikamilika na madarasa yameshaanza kutumika.
- Wilaya ya Same ilipatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1,180,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 59 na ujenzi umekamilika na upo katika hali ya kuridhisha.
- Katika Halmashauri ya Moshi vijijini jumla ya shilingi 1,700,000,000zilipelekwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 85 vya shule za katika shule za sekondari 24, ujenzi huo umekamilika na majengo yapo kwenye hali nzuri.
- Manispaa ya Moshi ilipokea kiasi cha shilingi 438,843,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 22 , ujenzi huo umekamilika na vyumba vimeanza kutumika.
Kupitia ufuatiliaji huu, TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro ilibaini kuwa yapo madarasa yaliyojengwa na kuwa na dosari mbali mbali za kiujenzi ambazo ni pamoja na ufungaji wa milango iliyo chini ya kiwango kilichopitishwa, na pia sehemu ya kupitia walemavu kwa mlalo, kuwa parefu sana kuliko urefu unaotakiwa. Dosari hizi zilijadiliwa kati ya TAKUKURU na wataalam husika katika warsha za majadiliano na marekebisho yalifanyika kulingana na dosari hizo zilizokuwa zimeainishwa
Ndugu Wanahabari,
Tuliendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro ili kuhakikisha kuwa thamani ya fedha (Value for Money) inapatikana na fedha zinatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa. Ufuatiliaji wa miradi yenye thamani ya shilingi 8,227,258,724.46 ulifanyika na miradi iliyokuwa na changamoto au mapungufu ilijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na mamlaka husika. Miradi hiyo ni kama ifuatavyo;
- 7,082500/– na mradi haujakamilika ipasavyo na ufuatiliaji wa karibu unaendelea.
- jenzi wa maji ya bomba katika ziwa Chala sehemu ya Njiro shilingi 200,000,000. Na pia walifuatilia fedha zilizotumwa na serikali kwa ajili ya kuhamasisha chanjo ya UVIKO 19 kiasi cha shilingi 25,254,666.91 katika Wilaya ya Rombo na ofisi ya TAKUKURU imechukua hatua ya kuendelea kufuatilia walipwaji wa fedha hizo. Ili kubaini uhalali wa waliolipwa.
- fedha za kutekeleza shughuli mbalimbali za utoaji chanjo ya uviko19, kiasi cha shilingi 29,601,576.25/= malipo yameridhisha. Na mradi wa Ujenzi wa zahanati ya Lang’ata bora kiasi cha shilingi 69,803,000 zilitumika na mradi upo kwenye hali nzuri.
- fuatiliaji wa utekelezaji wa mradi wa chanjo ya Uviko-19, zilitumwa na serikali kiasi cha shilingi 28, 788,000.36.na TAKUKURU Hai wanaendelea kufuatilia.
Mapungufu yaliyobainika katika Ukaguzi wa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kituo cha mabasi kuchukua muda mrefu kukamilishwa tofauti na muda uliokuwa umepangwa.
Hata hivyo, mamlaka husika ilijulisha kuwa uchelewaji huo, ulitokana na fungu dogo linaloletwa kwa ajili ya ujenzi huo kwa awamu. Changamoto hii imejadiliwa katika kikao na wadau husika na kuweka mikakati ya kuitatua.
UCHAMBUZI WA MIFUMO
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU mkoa wa Kilimanjaro ilifanya chambuzi za mifumo katika idara ya Elimu ili kuweza kubaini mianya ya rushwa katika sekta ya elimu ambapo tulibaini yafuatayo;-
- vitendo vya rushwa ya ngono vinavyotokana na matumizi mabaya ya madaraka hususani pale kiongozi anapotumia mbinu za upendeleo au kunyanyasa baadhi ya waliochini yake
- Ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma kuweza kuchochea vitendo vya rushwa hususani katika suala la ulevi na utoro kazini vitu vinavyopelekea mtumishi kuhitaji kupendelewa ili asichukuliwe hatua za kinidhamu
- Upangaji wa vituo vya kazi na uhamisho ndani ya halmashauri
- Utoaji wa fursa za mafunzo ya muda mfupi, semina na mafunzo ya muda mrefu kwa upendeleo.
- Uteuzi wa kusimamia mitihani, sensa au kazi nyingine maalum kwa upendeleo
Kupitia chambuzi hizi, mapungufu tajwa hapo juu ambayo baadhi yake yanapelekea mianya ya rushwa ya ngono, kwa kupitia warsha, wadau husika watashirikishwa kujadili matokeo ya chambuzi zetu na kuwekeana maazimio ya namna bora ya kuondokana na mianya ya rushwa ya ngono.
ELIMU KWA UMMA
Ndugu Wanahabari
TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro imeendelea kufanya juhudi za uelimishaji umma kwa lengo la kuwashirikisha wananchi kwenye mapambano dhidi ya rushwa ambapo kwa kipindi tajwa tumefanya Semina (49) katika Idara mbalimbali, mikutano ya hadhara (45), tumeimarisha klabu za wapinga rushwa (64),Maonesho (8) na pia tumeendesha vipindi vya Radio (12).
Vile vile, tulitayarisha makala (08) kwa ajili ya machapisho ya uelimishaji umma yanayoandaliwa na TAKUKURU. Ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa unaendelea kuimarika kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyojitokeza katika mkoa huu na mahali pengine nchini.
Aidha, katika kipindi Oktoba hadi Disemba 2021, TAKUKURU INAYOTEMBEA ilifanikiwa kukutana na wananchi wa Mabogini katika Halmashauri ya Moshi na kusikiliza kero zao mbali mbali na katika wilaya ya Rombo walifanikiwa kuwafikiwa wananchi wa soko la Mamsera na wananchi wa kata ya Useri na kusikiliza kero zao mbali mbali.
USHIRIKIANO NA SKAUTI
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi husika, TAKUKURU kwa kushirikiana na SKAUTI waliweza kwenda kuutambulisha mwongozo wa namna bora ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika kupambana na rushwa kati ya TAKUKURU na SKAUTI kwa walezi wa Skauti katika ngazi ya Mkoa na wilaya, hivyo Basi Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, akiambatana na Afisa Elimu Mkoa na Kamishna wa Skauti Mkoa, waliweza kwenda Kuutambulisha Mwongozo huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye kimsingi ndiye Mlezi wa Skauti katika mkoa huu, na kwa wakuu wa Wilaya zote za Same, Mwanga, Rombo, Siha, Hai na Moshi.
Hata hivyo tayari ushirikiano huo umeanza kwa kuwanoa waelimishaji yaani Wanachama wa Skauti na bado mafunzo yanaendelea ili waweze kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya Rushwa.
MWELEKEO WETU JANUARI-MACHI 2022
Ndugu Wanahabari,
Mwelekeo wetu katika kipindi cha mwezi wa Januari – Machi 2022, tutaelekeza nguvu zaidi katika KUZUIA RUSHWA kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kupitia vijana wa skauti na kupitia klabu za wapinga rushwa. Elimu hii itatolewa pia kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU na SKAUTI yaani – TAKUSKA.
Vileile, tutafuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha kuna thamani ya fedha (value for money) katika miradi hiyo ya Serikali na ya umma na kwamba fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Aidha tumejipanga kufanya chambuzi za mifumo katika Sekta za Afya, Maji, Ujenzi, Ukusanyaji wa Mapato, Ununuzi wa Umma, Nishati na Madini, Viwanda na Biashara pamoja na Uwekezaji.
WITO
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU mkoa wa Kilimanjaro inatoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wetu wa Kilimanjaro, kuendelea kutoa ushirikiano ili kuondoa kero za Rushwa katika jamii, kwani rushwa ni adui wa haki na adui mkubwa wa maendeleo ya mkoa wetu. Kazi iendelee!
Imetolewa na,
FRIDA WIKESI,
MKUU WA TAKUKURU
KILIMANJARO
0738150110