TAKUKURU IRINGA YAKAGUA NA KUTOA ELIMU YA USIMAMIZI WA MIRADI YA FEDHA ZA UVIKO 19
Ndugu Wanahabari,
Kwanza kabisa tumshukuru Mwenyezi Mungu kutukutanisha nanyi leo hii kwa ajili ya kuuhabarisha umma kuhusu kazi zilizotekelezwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Disemba, 2021. Taarifa hii inatokana na kazi zilizotekelezwa na ofisi ya Mkoa pamoja na wilaya za Mufindi na Kilolo. Kazi hizi zimetekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2019 kwa lengo la kuhamasisha na kukuza utawala bora na kuondoa rushwa.
Kazi hizi zimetekelezwa kupitia njia ya Uelimishaji umma ili kushirikisha wadau mbalimbali katika vita dhidi ya rushwa; kwa njia ya Uzuiaji wa vitendo vya rushwa kwa kuziba mianya inayochangia uwepo wake; Pamoja na kupambana na wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na makosa yahusianayo kwa kufanya chunguzi zinazopelekea kufungua mashtaka Mahakamani.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa imetolewa katika makundi mbalimbali ili kuhamasisha umma kushiriki mapambano dhidi ya Rushwa. Ubunifu na mbinu mbalimbali za kuelimisha zimetumika ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Viongozi wa Kata na Kamati za Ujenzi za mkoa wa Iringa zinazosimamia miradi ya fedha zilizoletwa na Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 Kamati za Ujenzi za mitaa na vijiji zilipewa elimu ya umuhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo na kwa kuwahusisha wananchi wa maeneo hayo katika usimamizi wa miradi hiyo. Tija kubwa imepatikana katika kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inapatikana, lakini pia katika udhibiti wa vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika ujenzi huo.
Ubunifu mwingine uliotumika na TAKUKURU mkoa wa Iringa ni kuwashirikisha viongozi wa maeneo ambako miradi hiyo ilitekelezwa kwa kuandaa na kurusha vipindi ya redio ambavyo lengo lake lilikuwa ni kuwahabarisha wananchi kuhusu uwepo wa miradi hiyo katika maeneo yao na kuwataka kutoa taarifa pale wanapogundua kuna ubadhirifu au uzembe wowote unafanyika kwa kupiga simu BURE namba 113 au kupiga namba ya Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na jitihada hizo za makusudi za kudhibti ubora na ukamilifu wa miradi hiyo, pia zimefanyika semina 37; mikutano ya hadhara 42; uimarishaji wa klabu za wapinga Rushwa 46 katika shule za Msingi na Sekondari; Habari 03; vipindi vya redio 03; Mkutano na waandishi wa habari 01; na kugawa machapisho mbalimbali kwa wananchi yenye ujumbe wa kukemea vitendo vya rushwa.
Katika kipindi husika TAKUKURU Mkoa wa Iringa kupitia kwa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, imekabidhi Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji ya Kufundisha Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kwa Skauti Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye pia ni Mlezi wa Skauti wa mkoa, ili aweze kutoa maelekezo ya utekelezaji wa mafunzo hayo muhimu kwa ngazi zote za Skauti walioko mashuleni.
Pia, mlezi huyo amewakabidhi Mwongozo huo Wakuu wa Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi ili uweze kutumika kuwapa mafunzo vijana Skauti katika wilaya hizo.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajenga vijana hao kimaadili ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo katika uwajibikaji na Uzalendo kupitia mkakati wa pamoja wa TAKUKURU NA SKAUTI (TAKUSKA).
Aidha katika kuzuia vitendo vya rushwa katika taasisi za umma, elimu ya Maadili ya Utumishi wa Umma imetolewa kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa ofisi ya mkoa wa Iringa pamoja na Wilaya za Kilolo na Mufindi. Elimu iliyotolewa ilihusu umuhimu wa kusimamia mapato ya Serikali na kuziba mianya ya rushwa inayojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia mada ya maadili na athari za rushwa ya ngono katika elimu zilitolewa kwa watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam – Kampasi ya Mkwawa.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Iringa imefanya kazi ya Uzuiaji wa vitendo vya Rushwa kwa kuziba mianya inayochangia uwepo wake kwa kuendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na udhibiti.
Jumla ya miradi ya maendeleo 12 yenye thamani ya Shilingi 7,135,579,015.93 (BILIONI SABA MILIONI MIA MOJA THELATHINI NA TANO ELFU MIA TANO SABINI NA TISA NA KUMI NA TANO) ilikaguliwa.
Miradi hii ni ya sekta za elimu, ujenzi (barabara) na afya. Miradi hii ilikaguliwa kwa lengo la kujiridhisha iwapo thamani halisi ya fedha imezingatiwa kwa kuangalia iwapo kuna ufujaji; ucheleweshaji wa makusudi wa mradi; uchepuzi wa rasilimali za mradi; na namna jamii inavyoshirikishwa. Miradi yote iliyokaguliwa inaendelea vizuri.
Vilevile zimefanyika chambuzi 5 za mifumo ya utoaji wa huduma katika Sekta za elimu na manunuzi, ambapo baada ya uchambuzi tulikutana na wadau kujadili matokeo ya chambuzi zetu na kuwekeana maazimio ya namna bora ya kuondokana na mianya ya rushwa.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2021 tumeendelea kupokea malalamiko na kishakufanya uchunguzi. Katika kipindi husika tumepokea taarifa na malalamiko 48 ambapo taarifa zilizohusu rushwa ni 26 na 22 hazihusiani na rushwa. Taarifa 22 ambazo hazihusiani na rushwa, watoa taarifa walielimishwa na kushauriwa namna bora ya kupata haki zao ikiwa ni pamoja na walalamikaji kuelekezwa mahali sahihi pa kwenda kuwasilisha malalamiko. Taarifa 26 zilizohusu rushwa zimefunguliwa majalada na uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbali mbali.
Mchanganuo wa taarifa hizo 48 kisekta ni kama ifuatavyo: Tamisemi 19, Mahakama 7, Afya 6, Elimu 2, Ardhi 2, Kilimo 2, Mnada 2, TAnesco 1, Viwanda 1, Elimu ya Juu 1, Benki 1, Usafirishaji 1, Idara ya maji 1, Nishati 1, na Polisi 1.
Jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kwa sasa ni 10 ambapo kesi mpya 1 ilifunguliwa katika kipindi cha Oktoba – Desemba 2021.
Ndugu Wanahabari,
Kazi zote hizi zimeweza kutekelezwa ikiwa ni mafanikio ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa, ikiwa ni pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa wilaya zote, Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama, Waandishi wa habari pamoja na Wananchi wote kwa ujumla.
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2021 ofisi iliendelea na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao kwa utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA na kuzipatia majibu, ambapo katika kipindi hicho mikutano ya hadhara ilifanyika katika maeneo mbalimbali.
Katika mikutano hiyo wananchi walionesha mwamko mkubwa na ari ya kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa na kuomba utaratibu huu uendelee ili kutatua kero mbalimbali za rushwa zinazowakabili wananchi.
TAKUKURU iliwapa elimu juu ya dhana ya rushwa, umuhimu wa kusimamia miradi ya maendeleo, umuhimu na jinsi ya kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kuelezwa dhumuni la kuwafikia mahali walipo ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi ya kusikilizwa ili kujua changamoto za rushwa zinazowakabili kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
MKAKATI WA JANUARI HADI MACHI, 2022
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2022 TAKUKURU mkoa wa Iringa imejipanga kuendelea kutatua kero za wananchi zinazohusiana na vitendo vya Rushwa na kuendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi kama vile kutenga siku moja kila mwezi kuwafuata wananchi walipo kupitia utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA ili kusikiliza na kutatua kero zao zinazohusu rushwa. Pia tutaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ile ya kimkakati.
Pia mafunzo kwa vijana wa Skauti mkoa wa Iringa yataanza kutolewa ili kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa. Vilevile tumejipanga kuendelea kuwaelimisha watumishi wa Sekta za Umma na Binafsi kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kujiepusha na ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya ofisi za umma.
Aidha, tutafuatilia utekelezaji wa maazimio tuliyokubaliana na wadau katika warsha za kujadili mianya ya rushwa iliyobainishwa katika chambuzi mbalimbali zilizokwishafanyika.
Wito kwa wananchi wa mkoa wa Iringa ni kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya rushwa kwa kupiga namba 113, kutuma ujumbe mfupi kwa kutumia namba *113#. Pia tunawasihi wananchi kujihadhari na watu wanaojifanya maafisa wa TAKUKURU na kwamba mtoe taarifa pale mnapowabaini.
Vilevile, tunawaasa watumishi wa Sekta za Umma na Binafsi mkoani Iringa, kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kujiepusha na ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya ofisi za umma ili kuwaondolea kero ya rushwa wananchi pindi wanapohitaji huduma kutoka kwao.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
“KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LANGU”
Imetolewa na:
Domina J. Mukama,
Mkuu wa TAKUKURU (M) Iringa,
Simu: 0738150054