ILALA, OKT – DES 2021

ILALA – JANUARI 24, 2022   TAARIFA KWA UMMA   TAKUKURU (M) ILALA YAFANYA UFUATILIAJI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI  TANO ZA FEDHA  ZA MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19

Ndugu Wanahabari,

Ninapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wetu na kuja kushiriki kwenye mkutano huu. Karibuni sana ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ilala.

Ndugu Wanahabari,

Ni utaratibu wetu TAKUKURU kutoa taarifa ya utendaji kazi kwa umma katika kipindi cha kila robo mwaka kupitia kwenu wanahabari. Leo TAKUKURU Mkoa wa Ilala tunatoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2021, kama inavyofafanuliwa hapa: –

  1. MAHAKAMA

Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ilala ina mashauri yanayoendelea mahakamani 27. Pia katika kipindi tajwa kesi 02 zilitolewa maamuzi mahakamani ambapo kesi zote zilishinda.

  • UCHUNGUZI

Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Ilala tumepokea taarifa 173. Kati ya taarifa hizo malalamiko yaliyohusu rushwa ni 116, ambapo idara zinazolalamikiwa ni: –  Idara za Utawala katika ofisi mbalimbali 26, Sekta binafsi 18, Serikali za Mitaa 13, Fedha 8, elimu 7, usafiri 5, biashara 5,  ujenzi 4, Idara zenye malalamiko matatu kila moja ni Saccos, Polisi na Ardhi. Idara zenye malalamiko mawili kwa kila moja ni Viwanda, Umeme, Ulinzi na Michezo. Aidha idara zenye lalamiko moja moja ni Afya, Mahakama, Maji , Mafuta na gesi, Madini, Mawasiliano na Huduma za jamii. Uchunguzi wa taarifa zote 116 unaendelea na upo kwenye hatua mbalimbali.

Aidha kati ya taarifa 173 zilizopokelewa, taarifa 57 zilikuwa sio za vitendo vya rushwa. Kati ya taarifa hizo 57, watoa taarifa 53 walielimishwa na kushauriwa na taarifa 04 watoa taarifa walielimishwa na kuelekezwa mamlaka husika ya kuwasilisha taarifa zao ili ziweze kufanyiwa kazi.

UELIMISHAJI UMMA

TAKUKURU (M) wa Ilala tunalo jukumu la Uelimishaji Umma. Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021 Dawati la Elimu kwa umma Mkoa wa Ilala tumeweza kuelimisha makundi mbalimbali kwa njia ya vipindi vya redio na TV 2, semina 04, mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi 02, taarifa kwa vyombo vya habari 01, kuimarisha klabu katika shule za Msingi, Sekondari na vyuo 04.

TAKUKURU INAYOTEMBEA

TAKUKURU inaendelea kutoa huduma kupitia kampeni ya TAKUKURUINAYOTEMBEAambao ni ubunifu wa kuwafuata wananchi sehemu mbalimbali ili kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021, TAKUKURU (M) Ilala imefika katika Mtaa wa Zavala, Kata ya Chanika kwa ajili ya kusikiliza kero za rushwa ,ambapo baadhi zilipatiwa ufumbuzi nyingine zinaendelea  kufanyiwa kazi.

TAKUSKA

Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Ilala iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu ambao umeandaliwa chini ya mpango wa ushirikiano kati ya TAKUKURU na Chama cha Skauti nchini – TAKUSKA, tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika. Lengo la mwongozo na ushirikiano huu ni kuwajenga vijana hasa wanachama wa skauti katika misingi ya Uzalendo, Uwajibikaji na Uadilifu ikiwa ni pamoja na kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.

4.0 UZUIAJI RUSHWA

Katika kuhakikisha kuwa kero mbalimbali zinapatiwa ufumbuzi, na wakati mwingine kubaini mianya ya rushwa na hatimaye kupata njia sahihi ya kuishauri serikali kuhusiana na masuala ya rushwa katika mkoa wetu tumefanikiwa kufanya chambuzi tatu za mifumo kama ifuatavyo:

  1. Uchambuzi wa mfumo wa uendeshaji wa vyama vya ushirika vya soko la Mchikichini iliandaliwa na kukamilika.Uchambuzi huu ulitokana na malalamiko yalliyopokelewa na ofisi ikaona umuhimu wa kufanya uchambuzi wa mfumo wa kubaini mianya ya rushwa katika usimamizi wa chama cha Ushirika KAVIMCO kilichopo katika soko la Mchikichini.
  1. Kupitia mwongozo kukusanya takwimu na kuandaa taarifa ya udhibiti wa rushwa ya ngono. Hii inafanyika kwa kufanya mahojiano na walimu wa shule za Msingina Sekondari na viongozi wa ngazi za Halmashauri.
  1. Taarifa ya tathmini ya utendaji kazi ya wakala wa ununuzi serikalini (GPSA)imeandaliwa na kukamilika. Aidha tathmini ya taarifa hiyo  ilifanyika na kubainisha changamoto na mianya ya rushwa iliyobainika  na kuainisha mapendekezo ya namna ya kuidhibiti.

Baadhi ya mapungufu tuliyoyabaini katika uchambuzi huo wa mifumo ambao ungeweza kusababisha mianya ya rushwa, tumewafahamisha mamlaka husika na tayari marekebisho yameanza kufanyika.

Pamoja na kuchambua mifumo, katika kipindi husika ofisi imefuatilia matumizi ya fedha za umma kwenye miradi ya maendeleo, ambapo miradi miwili (2) yenye thamani yashilingi milioni mia sita ishirini na mbiliilifuatiliwa kama ifuatavyo:

  1. Ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Gulukwalala wenye thamani ya shilingi milioni mia tano (Tsh.500,000,000/=)  umefanyika. Aidha ufuatiliaji huo umebaini kuwa ujenzi umefanyika kwa kiwango kizuri ingawa umechukua muda mrefu kukamilika.
  1. Ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Luhanga na nyumba ya mtumishi  wenye thamani ya shilingi milioni mia moja ishirini na mbili (Tsh.122,000,000/=) umefanyika. Aidha ufuatiliaji huo umebaini kuwa ujenzi umefanyika kwa kiwango kizuri ingawa umechukua muda mrefu kukamilika.

UFUATILIAJI WA MATUMIZI YA FEDHA MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19

Jumla ya shilingi bilioni tano na milioni mia moja ( Tsh.5,100,000,000/=) zimepokelewa katika Jiji la Dar es salaam kwa ajili ujenzi wa madarasa mia mbili hamsini na tano(255) ya shule za sekondari kwa lengo la kuondoa msongamano ili kupunguza maambukizi ya Uviko 19.

Fedha hizo zilielekezwa katika majimbo yote kwa mchanganuo ufuatao: Ilala  madarasa 89, Segerea madarasa 41 na Ukonga madarasa 125. Shule zipatazo 39 zilizokuwa na upungufu zaidi kati ya 62 ndizo zilinufaika na mradi huo. Aidha ujenzi huo wa madarasa ulifanyika pamoja na utengenezaji wa madawati hamsini (50) kwa kila chumba cha darasa kilichojengwa.

Ofisi ya TAKUKURU (M) Ilala ilifanikiwa kupitia miradi hiyo ambayo imekamilika na hakukuwa na mapungufu yoyote yaliyobainika. Aidha utengenezaji wa madawati bado unaendelea.

MIPANGO YA MIEZI MITATU IJAYO

TAKUKURU (M) Ilala katika kipindi cha miezi mitatu (3) cha Januari hadi Machi, 2022, itaendelea na majukumu yake ya kuelimisha umma, kuchunguza, kufanya utafiti na udhibiti pamoja na kufuatilia miradi ya maendeleo.

Katika kutekeleza majukumu haya, TAKUKURU (M) Ilala imeweka mikakati maalum ya kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi na mkazo utaelekezwa kwenye kudhibiti vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na inakamilika kwa wakati na thamani ya fedha (Value for money) inaonekana.

Elimu itatolewa kwa vijana wa skauti kuhusu kuzuia nakupambana na rushwa, kwa lengo la kuandaa kizazi ambacho kitachukia rushwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Kwa upande wa utafiti na udhibiti mkazo utaelekezwa katika kudhibiti mianya ya rushwa katika Sekta ya Elimu, Maji, Ujenzi wa Miundombinu, Uwekezaji, Viwanda, Manunuzi ya Umma na ukusanyaji mapato ya Serikali.

Kufanikisha hilo, tutahakikisha miradi yote katika sekta hizi inayotekelezwa ndani ya Jiji la Ilala inafuatiliwa kikamilifu katika hatua zote kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kuiziba mapema kabla ya upotevu wa fedha za Serikali haujajitokeza.

MWISHO

Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa kukubali kuja kunisikiliza na hasa tukizingatia umuhimu wa shughuli yenu ya habari.

Ninapenda kutoa wito kwenu kuendelea kutoa elimu juu ya adui rushwa kwa jamii na TAKUKURU inawaomba mkaendelee kuwa mabalozi madhubuti wa mapambano dhidi ya rushwa.

KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LANGU

IMETOLEWA NA

Pilly Mwakasege

KAMANDA WA TAKUKURU (M) ILALA

0738 150234

Taarifa kwa Umma