TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imeendelea na utekelezaji wa lengo la kukuza na kuimarisha utawala bora na kuzuia na kupambana na rushwa kwa mujibu wa sheria.
Sehemu ya utendaji wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma kwa robo ya Oktoba hadi Disemba, 2021 ni kama ifuatavyo:
Kwanza, waswahili wanasema ’samaki mkunje angali mbichi’ na mwenendo mwema wa watendaji wa umma unapaswa ujengwe kama tabia katika makuzi ya wanajamii tangu katika umri mdogo.
TAKUKURU kwa kushirikiana na Chama cha SKAUTI inazingatia umuhimu wa makuzi mema kwa vijana ili kuwajenga katika uadilifu, uzalendo na uwajibikaji, silaha ambazo zitawafanya wawe wananchi na watendaji makini wasio na hulka za ubinafsi ambao huzalisha matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za umma. Hivyo tumeanza kutekeleza mkakati wa kuwaelimisha vijana wanachama wa SKAUTI na wale wa klabu za wapinga rushwa kuhusu nafasi zao katika kuzuia vitendo vya rushwa katika jamii wanamoishi. Lengo ni kuwa na watumishi wa sekta za umma na binafsi na wananchi kwa ujumla ambao uzalendo wao utawafanya waichukie rushwa na kuwa mstari wa mbele katika kuipinga kwa maneno na matendo yao.
Aidha, katika eneo la uelimishaji umma ili kuhamasisha ushiriki wa jamii kwa ujumla katika mapambano dhidi ya rushwa, tumefanya mikutano 47 ya hadhara; semina 90; Onesho moja; na tulitembelea kwa lengo la kuimarisha klabu 121 za wapinga rushwa zilizopo kwenye shule za Msingi, Sekondari na Vyuo na tulishiriki katika vipindi 12 vya redio. Baadhi ya mikutano ya hadhara ilifanyika kwa utaratibu wa TAKUKURU INAYOTEMBEA ambapo kwa kutumia gari la matangazo tuliwahamasisha wafanyabiashara kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji wa biashara; kutambua umuhimu na wajibu wa kulipa kodi; kutotoa wala kushawishi kutoa rushwa na kutoa taarifa TAKUKURU pindi wanapokutana na watumishi wa umma wanaowataka kujihusisha na rushwa.
Pili, Miradi ya maendeleo ni mali ya wananchi. Hivyo, TAKUKURU inawaelimisha wananchi kutambua hilo na kuwa mstari wa mbele kuifuatilia ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika vizuri. Kwa kushirikiana na wadau wengine, tuliweka nguvu nyingi kufuatilia madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, ambapo pamoja na madarasa, jumla ya miradi 596 ya ujenzi yenye thamani ya shilingi 20,660,907,935/= ilikaguliwa ambapo ushauri ulitolewa kwa wahusika kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto.
Pia tumekamilisha ufuatiliaji wa miradi minne iliyokuwa imekataliwa kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021. Kati ya miradi hiyo mine, miradi mitatu kati yake ilikutwa na dosari ndogo ndogo, ambazo zilijadiliwa na kurekebeshwa, lakini kwenye mradi mmoja inaonekana kuna malipo yaliyofanyika kabla ya kazi husika kutekelezwa, hivyo tunashirikiana na halmashauri husika kufuatilia marekebisho ya dosari hiyo.
Tunawakumbusha watendaji na wananchi kwa ujumla kuzingatia kwamba vifaa vya ujenzi katika miradi inayotekelezwa kwa njia ya ‘force account’ vinapaswa kununuliwa kwa bei ya soko ili thamani ya fedha ifikiwe.
Aidha, katika kuzuia vitendo vya rushwa, tulifanya chambuzi za mifumo 9 ya utendaji na utoaji huduma katika mkoa wetu wa Dodoma na kushiriki warsha 11 za kujadili matokeo ya uchambuzi wa mifumo hiyo.
Kufuatia uchambuzi huo, taarifa nne za utekelezaji wa maazimio tuliyokubaliana na wadau husika katika warsha, tayari zimeshapokelewa. Uchambuzi hufanyika katika maeneo yanayolalamikiwa kwa vitendo vya rushwa kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kushirikiana na wadau wa eneo husika ili kuweka mikakati ya kuiziba.
Tatu, Katika dawati la uchunguzi, tumepokea jumla ya taarifa 106 ambapo taarifa za rushwa zilikuwa 58 tu na zisizohusu rushwa zilikuwa 48. Taarifa 58 zinazohusu rushwa zimeshughulikiwa kwa njia za uzuiaji rushwa; uelimishaji pamoja na uchunguzi ambapo uchunguzi wa majalada 19 umekamilika na mashauri matano yamefunguliwa kesi mahakamani na hivyo kufanya jumla ya mashauri 53 yanayoendelea mahakamani katika mkoa wa Dodoma mpaka sasa. Aidha, katika kipindi husika, Jamhuri imeshinda kesi mbili mahakamani.
Kati ya taarifa 48 ambazo hazikuhusu rushwa, 8 zilihamishiwa idara nyingine na zilizosalia (taarifa 40), watoa taarifa walielimishwa na kushauriwa ni wapi mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko yao.
Taarifa 106 zilizopokelewa zilihusu Sekta zifuatazo: Serikali za Mitaa, Vijiji, Kata na Halmashauri malalamiko 36; Ardhi 19; Elimu 11; Mahakama 9; Afya 7; Fedha 5; na Sekta nyinginezo 19.
Nne, Pamoja na kujikita katika kuelimisha vijana wanachama wa SKAUTI mbinu mbalimbali ili wawe vinara wa mapambano dhidi ya rushwa katika jamii kwa kuzingatia misingi ya uskauti, pia katika robo ya Januari hadi Machi mwaka huu tutatumia gari la matangazo la ’Longa nasi’ na mbinu zingine, kuelimisha wananchi walio katika mikusanyiko kwenye Mitaa, Vijiji na Vitongoji mbalimbali mkoani Dodoma.
Mkazo ni kuwakumbusha wajibu wao wa kushiriki katika kuikataa, kuikemea na kuitokomeza rushwa. Pia tutaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine kufuatilia miradi ya maendeleo inayoendelea katika Mkoa wetu, kwani miradi ni mali ya wananchi.
Mwisho, Vitendo vya rushwa ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili ambapo ubinafsi unatawala na uzalendo unafifishwa.
Hivyo, tunawaomba wananchi wa Mkoa wa Dodoma kushiriki kukuza maadili ya kitanzania yanayozingatia misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. RUSHWA HAILIPI.
Imetolewa na:
Sosthenes Kibwengo
Mkuu wa TAKUKURU (M) Dodoma
Simu: 0738150070