TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI TAKUKURU ARUSHA YAFUATILIA MIRADI YA SHILINGI BILIONI 12.6
Ndugu Wanahabari,
Awali wa yote nitumie fursa hii kuwatakia wote KHERI YA MWAKA MPYA 2022! Tumekutana leo hapa kama ilivyo ada ili kuuhabarisha Umma juu ya Utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba 2021. Taarifa hii tutakayoitoa kwa Umma, inahusisha utendaji kazi wa Ofisi ya TAKUKURU Mkoa na Ofisi zake za Wilaya ya Arumeru, Monduli, Longido, Karatu na Ngorongoro.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2019, TAKUKURU inayo majukumu makuu matatu ambayo ni; Kuelimisha Jamii juu ya rushwa na madhara yake; Kutekeleza shughuli za Uzuiaji Rushwa katika Taasisi za Umma na sekta binafsi na kufanya uchunguzi na kufikisha watuhumiwa Mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) baada ya chunguzi hizo kukamilika.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, katika kipindi cha miezi mitatu iliendelea kutekeleza majukumu yake ya kufanya uchunguzi wa makosa ya rushwa na kuwafikisha Mahakamani wale waliobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa; Kuelimisha Umma kwa kuhakikisha kuwa jamii inafahamu madhara ya rushwa ili kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya rushwa na Kuzuia Rushwa kwa kufanya Tafiti katika Sekta za Umma na Binafsi kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika sekta hizo na kushauri njia sahihi za kuziba mianya hiyo.
1.0 UZUIAJI RUSHWA
1.1 Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma – PETS
Ndugu Wanahabari,
Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni jukumu mojawapo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Ufuatiliaji huu unalenga kubainisha mianya ya rushwa, ucheleweshaji wa utekelezaji, uvujaji wa fedha za umma na ushirikishwaji wa wananchi au wadau katika miradi husika. Pia mtiririko wa fedha hufuatiliwa kutoka chanzo ambacho kinaweza kuwa; Hazina, Wafadhili au Vyanzo vya ndani, mpaka kwenye mradi husika.
Baada ya ufuatiliaji, TAKUKURU huchukua hatua zifaazo kulingana na kinachobainika katika ufuatiliaji huo ikiwemo; kushauri au kujadiliana na wadau kuhusu namna ya kuondoa upungufu uliobainika ili thamani ya fedha ifikiwe; kuelimisha wananchi au wadau; kufanya uchambuzi wa mifumo na kuanzisha uchunguzi kwa miradi inayobainika kuwa na mapungufu makubwa.
Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2021, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha imefanya ufuatiliaji wa Shilingi za Kitanzania Bilioni Kumi na mbili, milioni mia tano hamsini na tano, laki sita themanini na tano elfu, mia moja thelathini na nane nukta mbili saba ( Sh. 12,555,685,138.27 ). Ufuatiliaji huo ulifanyika katika fedha zilizotolewa kwa ajili utekelezaji wa shughuli zifuatazo;
- Utoaji wa chanjo ya UVIKO 19,
- Ujenzi wa miundo mbinu kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19, kwa vyumba vya madarasa na mabweni, sekta ya afya na ujenzi wa barabara.
Kati ya fedha hizo kiasi cha;
- Shilingi Bilioni kumi, Milioni mia saba thelathini (Sh. 10,730,000,000/-) zililenga kujenga vyumba vya madarasa (516),
- Shilingi milioni mia mbili arobaini na nne, laki sita ishirini na tatu elfu, mia tisa thelathini na nne nukta mbili tano (Sh. 244,623,934.25) zililenga kutekeleza shughuli mbalimbali za utoaji wa chanjo ya UVIKO 19,
- Shilingi Milioni mia nane tisini na moja, na tisini na moja elfu, mia mbili na nne (Sh. 891,091,204) zililenga kujenga barabara,
- Shilingi Milioni mia mbili arobaini (Sh. 240,000,000/-) zililenga kujenga mabweni matatu (03),
- Shilingi milioni thelathini (Sh. 30,000,000) zililenga kujenga maabara moja (01) na
- Shilingi milioni mia mbili (Sh. 250,000,000) zililenga kujenga kituo cha afya.
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Arusha kupitia Ofisi zote za Wilaya, ilifuatilia miradi hii kuanzia hatua ya awali ya utekelezaji wake ambapo baadhi ya miradi hiyo ilibainika kutekelezwa kwa kufuata taratibu na pia ipo iliyobainika kuwa na mapungufu kama vile kutokufuatwa kwa ramani za ujenzi hasa za madarasa, kukosewa kwa vipimo vya milango, madirisha na veranda, kutokuwa na utaratibu mzuri katika upokezi wa vifaa, udanganyifu katika makato ya kodi ya zuio (withholding tax), watoa huduma kutotoa stakabadhi za EFD na mwisho ucheleweshaji wa vibali vya ujenzi. Baada ya kubaini mapungufu haya, Ofisi ya TAKUKURU ilitoa ushauri na maelekezo kwa mamlaka husika na hatua za marekebisho zilifanyika. Aidha kwa miradi iliyobainika kuwa na kasoro kubwa uchunguzi umeanzishwa na unakamilishwa kwa sasa.
Lengo la ufuatiliaji huu, ni kuhakikisha na kujiridhisha miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha (Value for money) inapatikana kwenye utekelezaji wake na kuangalia iwapo kuna uvujaji, ucheleweshaji wa makusudi wa mradi, uchepuzi wa rasilimali za mradi na pia iwapo jamii inashirikishwa ipasavyo katika utekelezaji wa miradi hiyo. Katika kipindi tajwa, miradi ifuatayo ilifuatiliwa kwa kila Wilaya;
Wilaya ya Arusha
Thamani ya Miradi Shilingi 2,207,121, 083.90/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 107,121,083.90/- za kutekeleza shughuli mbalimbali za Utoaji Chanjo ya Uviko 19 katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Arusha.
- Ufuatiliaji wa shilingi 2,100,000,000/= za ujenzi wa Madarasa 105 Katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
Wilaya ya Arumeru
Thamani ya Miradi Shilingi 3,883,192,296.07/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 62,101,092.07/- za kutekeleza shughuli mbalimbali za Utoaji Chanjo ya Uviko 19 katika Wilaya ya Arumeru.
- Ufuatiliaji wa shilingi 3,400,000,000/- za Miradi ya Ujenzi wa Madarasa 170 Katika Wilaya ya Arumeru kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
- Ufuatiliaji wa shilingi 30,000,000/- za ukamilishaji wa Maabara ya shule ya sekondari Majengo katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru.
- Ufuatiliaji wa shilingi 391,091,204/- za ujenzi wa barabara ya Kivulini – Maternity Afrika katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Wilaya ya Monduli
Thamani ya Miradi Shilingi 1,237,428,121.58/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 27,428,121.58/- za kutekeleza shughuli mbalimbali za Utoaji Chanjo ya Uviko 19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.
- Ufuatiliaji wa shilingi 250,000,000/- za ujenzi wa Kituo cha Afya Tarafa ya Kisongo.
- Ufuatiliaji wa shilingi 960,000,000/= za miradi ya ujenzi wa Madarasa 48 Katika Halmashauri ya wilaya ya Monduli kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
Wilaya ya Longido
Thamani ya Miradi Shilingi 1,513,443,454.68/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 23,443,454.68/- za kutekeleza shughuli mbalimbali za Utoaji Chanjo ya Uviko 19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
- Ujenzi wa majengo ya upasuaji na kichomea taka katika kituo cha afya Ketumbeine kwa shilingi 250,000,000/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 1,240,000,000/= za ujenzi wa vyumba 62 vya Madarasa katika halmashauri ya wilaya ya Longido kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
Wilaya ya Karatu
Thamani ya Miradi Shilingi 2,090,000,000/-
- Ujenzi wa barabara ya lami kilometa 1 Karatu mjini kwa shilingi 500,000,000/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 1,590,000,000/- za ujenzi wa vyumba 62 vya Madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
Wilaya ya Ngorongoro
Thamani ya Miradi Shilingi 1,624,500,182.04/-
- Ufuatiliaji wa shilingi 24,500,182.04/- za kutekeleza shughuli mbalimbali za Utoaji Chanjo ya Uviko 19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
- Ufuatiliaji wa shilingi 240,000,000/- za Ujenzi wa mabweni matatu katika shule ya msingi Enduleni.
- Ufuatiliaji wa shilingi 1,360,000,000/- za ujenzi wa vyumba 68 vya Madarasa katika halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
1.2 Uimarishaji wa Mifumo
Ndugu Wanahabari,
Uimarishaji wa mifumo hufanyika kwa kufanya uchambuzi wa mifumo kwenye sekta za Umma na Binafsi, kuweka mikakati ya kudhibiti mianya ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa mikakati iliyoazimiwa. Katika kipindi tajwa, TAKUKURU Mkoa wa Arusha imefanya chambuzi nane (08) za mifumo katika utendaji kazi wa wakala wa huduma ya ununuzi Serikalini (GPSA) na kufanya tathmini ya vihatarishi vya rushwa ya ngono katika ajira na upandishwaji wa vyeo katika sekta ya elimu (Umma na Binafsi). Baadhi ya mianya ya rushwa ilibainishwa na kwa kupitia warsha tulikaa na wadau husika kujadili matokeo ya chambuzi hizo na kuwekeana maazimio ya namna bora ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.
2.0 UELIMISHAJI UMMA
Ndugu Wanahabari,
TAKUKURU Mkoa wa Arusha katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, imefanikiwa kufikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa makundi mbalimbali ya wananchi kupitia njia ya Semina kumi na tano (15), Mikutano ya hadhara Sitini na moja (61), Uimarishaji wa klabu za wapinga rushwa katika Shule za Msingi na Sekondari sitini na nne (64), kuandika Makala nne (04), Kushiriki Maonesho sita (06), kuendesha vipindi vya radio vitano (05) na kutoa taarifa moja (01) kwa umma kupitia vyombo vya habari. Uelimishaji huu umeenda sanjari na ugawaji wa machapisho mbalimbali yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa yanayowawezesha wananchi kuendelea kujielimisha zaidi juu ya rushwa na madhara yake.
Vilevile, katika kipindi husika, TAKUKURU Mkoa wa Arusha iliweza kuutambulisha kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji wa Kufundishia Vijana wa Skauti Kuhusu Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mwongozo huu tayari umetambulishwa hadi ngazi za Wilaya tayari kwa kuanza kutumika – lengo likiwa ni kuwajenga vijana katika misingi ya Uzalendo, Uwajibikaji na Kutojihusisha na Vitendo vya Rushwa.
3.0 UCHUNGUZI NA MASHTAKA
Ndugu Wanahabari,
Katika jukumu letu la kupambana na rushwa, tunapokea taarifa za vitendo vya rushwa, tunazifanyia uchunguzi na zile zinazobainika kuwa na ushahidi wa kutosha, wahusika wanafikishwa Mahakamani kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kujibu tuhuma husika. Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilipokea jumla ya taarifa mia moja tisini na nane (198) ambapo kati ya taarifa hizo; Mia ishirini na nane (128) zilihusu rushwa na Sabini (70) zilihusu makosa mengine tofauti tofauti.
Kati ya taarifa 128 zilizohusu Rushwa na kuanzishiwa uchunguzi, majalada 115 uchunguzi wake bado unaendelea, taarifa mbili (02) zilifungwa kwa kukosa ushahidi, na uchunguzi wa majalada kumi na moja (11) ulikamilika. Aidha, kati ya taarifa 70 ambazo hazikuhusu rushwa, taarifa Hamsinina tisa (59) zilitolewa ushauri na taarifa Kumi na moja (11) zilihamishiwa Idara nyingine kama vile Ardhi, Mahakama, Polisi, Halmashauri na Sekta binafsi.
Aidha katika kipindi tajwa, Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilifungua mashauri mapya manne (04) Mahakamani. Katika kipindi tajwa mashauri ishirini na saba (27) yanaendelea Mahakamani, ambapo mashauri tisa (09) yalitolewa uamuzi kwa Jamhuri kushinda yote na watuhumiwa kukutwa na hatia.
4.0 USHIRIKIANO WA WADAU
Ndugu Wanahabari,
Ili kufanikisha jukumu la Mapambano dhidi ya rushwa, TAKUKURU inawajibika kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kufikisha ujumbe wa mapambano dhidiya rushwa katika jamii.
Kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, Ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Arusha ilishirikiana na wadau na kufanikiwa kufanya shughuli za maonesho makubwa ya Kitaifa na Kimataifa kama vile;
- Maonesho ya Utalii ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Mwezi Oktoba 2021,
- Maonesho ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji yaliyofanyika mwezi Novemba 2021 na
- Maonesho ya wiki ya Nenda kwa usalama Barabarani yaliyofanyika kitaifa Jijijini Arusha Mwezi Novemba 2021.
Katika maonesho hayo TAKUKURU mkoa wa Arusha ilipata fursa ya kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi waliohudhuria maonesho hayo kwa njia ya maelezo na kugawa machapisho na vipeperushi mbalimbali vyenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa.
Aidha katika kipindi tajwa, TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilishirikiana na Chama cha SKAUTI Mkoa wa Arusha kutoa elimu kwa vijana wa skauti katika kambi ya skauti iliyohusisha vijana zaidi ya 200 kutoka Wilaya zote Mkoani Arusha na kuweka mikakati ya kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa.
5.0 MIKAKATI YA KIPINDI CHA JANUARI HADI MACHI 2022
Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2022 tumejipanga kufanya mambo yafuatayo: –
- Kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwaelimisha na kuwashirikisha wadau katika shughuli za mapambano dhidi ya rushwa. Mojawapo wa wadau muhimu ambao tunaendelea kushirikiana nao ni Chama cha Skauti Mkoa wa Arusha ambapo viongozi na vijana wa Skauti wataendelea kuelimishwa na baadae kutumika kuelimisha makundi mengine kuhusiana na rushwa.
- Kuendelea na utaratibu wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao kupitia TAKUKURU INAYOTEMBEA na kusikiliza kero zinazohusu vitendo vya rushwa kwa lengo la kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati, utaratibu huu utawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali kama masoko,magulio na mikutano mbalimbali ya Kiserikali.
- Tutaendelea kufanya kazi za uzuiaji rushwa kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika maeneo mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi na kushauri namna bora ya kuiziba mianya hiyo. Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kufuatilia Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na wafadhali hususani fedha za mkopo wa IMF ambayo bado haijakamilika ili iweze kukamilika kama ilivyokusudiwa.
- Kuendelea kupokea na kufanyia uchunguzi malalamiko ya vitendo vya rushwa kwa mujibu wa sheria na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.Chunguzi zilizolengwa ni pamoja na Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, Ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika Halmashauri na Vyama vya Ushirika ambapo taarifa mbalimbali zinaonyesha kuna vitendo vya Rushwa na ufujaji.
6.0 WITO
Ndugu Wanahabari,
Wito wetu kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha, waendelee kuipa ushirikiano TAKUKURU na Serikali kwa ujumla hasa katika kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa ukamilifu na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika. Aidha tunawaasa kutoa taarifa mara moja pale wanapobaini ukiukwaji wowote wa taratibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Pia nitumie fursa hii kuwatahadharisha wananchi juu ya uwepo wa wimbi kubwa la matapeli ambao wamekuwa wakiwapigia wananchi simu na kujitambulisha kuwa ni maafisa wa TAKUKURU na baadae kuwataka kufika Ofisi za TAKUKURU kwa kuwatishia kuwa wana tuhuma za rushwa.
Wananchi wanapopata wito kama huu, kwanza wasitishike na kuanza kuingia makubaliano ya kutoa fedha ili kumaliza suala lao, badala yake wapige simu au kufika Ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu nao ili kupata uhakika wa wito huo. Ofisi yoyote ya TAKUKURU atakayoenda itamwezesha kufahamu iwapo wito huo ni wa kweli au la.
Tunawaasa pia wananchi kuendelea kutumia njia zetu za mawasiliano kutoa taarifa za vitendo vya rushwa au wanapohitaji kujielimisha zaidi juu ya rushwa. Njia hizo za mawasiliano ni simu ya BURE 113, *113# ambayo unaweza kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maneno, TAKUKURU APP, You Tube – (TAKUKURU TV), facebook– (Takukuru Tz), Twitter (TAKUKURU.TZ) na Instagram – (takukuru.tz).
‘KUPAMBANA NA RUSHWA NI JUKUMU LANGU’
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA,
Imetolewa na:
James Ruge
Mkuu wa TAKUKURU (M) Arusha
Simu: 0738 150 063