Kwa mujibu wa Utangulizi wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007, Sheria hii imetungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili iweze kushughulikia kikamilifu makosa ya rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini. Sheria hii inatumika Tanzania Bara peke yake na inahusu kila mtu atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa awapo nchini Tanzania au anapokuwa nje ya Tanzania au alikuwa nje ya Tanzania na kwa wakati huo anaishi Tanzania .
Lengo kuu la Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007 limeainishwa katika kifungu cha 4 cha Sheria hii ikiwa ni kuhakikisha ustawi wa utawala bora na kuondoa rushwa nchini. Ili kuhakikisha lengo hili linatimia, sheria hii inaweka mazingira bora kisheria, kiutawala, na kiutekelezaji yenye mwelekeo wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini.