TAKUKURU mwaka 2019 ilisaini makubaliano na Shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania – Trust (WFT-Trust) kushirikiana kuelimisha jamii katika mikoa yote Tanzania Bara dhidi ya madhara yatokanayo na rushwa ya ngono nchini kwa kuanzishwa kwa kampeni ijulikanayo kama Vunja Ukimya Kataa Rushwa ya Ngono.
Kampeni hii inatoa fursa kwa wananchi kutoa maoni ya kuimarisha na kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa. Kampeni ya hii inatumika kutangaza Mkakati wa Mawasiliano wa TAKUKURU uliopitishwa na wadau kwa hatua ya utekelezaji. Kuendesha kampeni ya uelimishaji nchi nzima kwa kipindi kirefu kutaifanya TAKUKURU izidi kusikika, kufahamika na kuiweka karibu zaidi na wananchi hatua zitakazokuuza ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Longa Nasi
Mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu letu sote. Hivyo kila mmoja wetu ashiriki kwa kulonga nasi “TAKUKURU” kwa kuwa tumepewa dhamana ya kuongoza mapambano haya.
Utatu
Kampeni imejengengeka kwenye dhana ya ushirikiano wa makundi muhimu katika kupambana na ajali za barabarani Makundi hayo ni TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau; Neno “Wadau” linajumuisha makundi mbalimbali; Hatuhitaji kumnyooshea kidole mtu au taasisi yoyote bali kukaa pamoja kutatua kero za ajali za barabarani. Tatizo la ajali za barabarani linasababishwa na mambo mengi ikiwemo RUSHWA, SHERIA MBOVU, UBOVU WA MIUNDOMBINU n.k. Tunahitaji kuweka mikakati ya pamoja na endelevu inayotibu tatizo.
Klabu za wapinga Rushwa
TAKUKURU imekuwa ikiwatumia wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwa mapambano yanategemea juhudi za wadau mbali mbali. Moja ya wadau ambao wanatumiwa na TAKUKURU ni wanafunzi kupitia klabu za wapinga rushwa. Mnamo mwezi Mei, 2007 TAKUKURU ilianzisha kampeni ya kufungua klabu za wapinga rushwa katika shule za sekondari Tanzania Bara ambapo Mkurugenzi Mkuu Dkt. Edward Hoseah alizindua klabu ya wapinga rushwa katika shule ya Sekondari Makongo ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kampeni hii. Zoezi hili liliendelea hata katika vyuo vya elimu ya juu na shule za msingi. Lengo la kuanzisha klabu hizi ni kuwajenga wanafunzi kimaadili kwa kuwafanya watambue madhara ya rushwa ili waichukie katika maisha yao na kuchukua hatua za kuzuia na kupambana nayo hatimaye kujenga jamii ya watu waadilifu.
Miongoni mwa kazi zinazofanywa na klabu ni
- kuwaelimisha wafunzi wenzao kuhusu rushwa na madhara yake
- kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU
- kutoa elimu ya rushwa kwa njia ya maigizo, uandishi wa makala, insha, uchoraji wa katuni, midahalo, kuimba nyimbo, kushiriki katika matamasha yanayoandaliwa na TAKUKURU, kushiriki katika shughuli za kijamii kama kutembelea wagonjwa, wazee ama wahitaji mbali mbali, kupanda miti na mengineyo.
Vijana wa Skauti
Lengo Kuu ni kuelimisha vijana wa Skauti ili waichukie rushwa na kushiriki kuzuia na kupambana nayo wakingali wadogo. Mkakati huu utawezesha wawezeshaji kuwa na uelewa wa pamoja wa maudhui ya elimu na kuongeza ufahamu wa masuala kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na itachangia kuwafanya wanafunzi shuleni na vyuoni kuwa wazalendo, waadilifu na wawajibikaji zaidi katika jamii na Taifa kwa ujumla. Aidha, tunaamini kuwa, Mwongozo huu utawanufaisha pia walimu, wanafunzi na wadau wengine watakaousoma kwa madhumuni ya kujifunza kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.