Fri05222015

Back You are here: Home PREVENTION INITIATIVES

PREVENTION INITIATIVES

Watumishi wa TASAF Mafia wapandishwa kizimbani

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Wilaya ya Mafia tarehe 18/03/2014 imewapandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Mafia watumishi watatu (03) waliokuwa watekelezaji mradi wa TASAF (Tanzania Social Action Fund ) Halmashauri ya Wilaya ya Mafia. Watumishi hao kwa majina ni Charity Edmore Sichona (36), Cotilde Benedict Gama(48) na Jimmy William Mhina(49).

Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Mh. Hassan Makube (Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Mafia, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na kumbana na Rushwa Wilson Ntiro aliieleza mahakama kwamba, kwa kutumia mamlaka waliyokuwa nayo kama mratibu, mhasibu na muwezeshaji (facilitator) wa mfuko wa TASAF katika Wilaya ya Mafia wote kwa pamoja walikula njama na kutenda kosa la kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu 22, cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11 ya mwaka 2007 pamoja na kifungu 333, 335(a) na 337 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejea ya mwaka 2002.

Kwa mujibu wa mashitaka, makosa waliyotenda washitakiwa hao ni pamoja na kula njama, kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri, kugushi, na wizi wa mali ya umma - kosa kwa mujibu wa kifungu 258 na 270 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejea ya mwaka 2002.

Mahakama ilielezwa kuwa upelelezi wa kesi hii umekamilika, washitakiwa wote wako mahabusu huku utaratibu wa dhamana zao ukiendelea kushughulikiwa. Kila mshitakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini watatu na kwa dhamana ya Shilingi za Tanzania milioni tatu (3,000,000/=) tu kwa kila mshitakiwa. Kesi hii imepangiwa tarehe ya kutajwa.

Imetolewa na

RAMADHANI S.MLANZA

MKUU WA TAKUKURU (W) MAFIA

KIBAHA PWANI.

Wawili wapandishwa kizimbani

Mnamo tarehe 11/03/2014 TAKUKURU Wilaya ya Mvomero iliwafikisha mahakamani Washitakiwa wawili kwa makosa ya Matumizi Mabaya ya Mamlaka chini ya kifungu na. 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 na kuisababishia Serikali hasara chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 1984 (RE: 2002).

Washitakiwa hao ni Bibi. SARAH PHILBERT LINUMA (61) ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mvomero na kustaafu mwaka 2013 pamoja na Bibi ANNA ANDULILE MWAKALYELYE (53) ambaye ni Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya Halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka 2007-2010.

Ilielezwa mahakamani kwamba Washitakiwa hao wakiwa waajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, kwa nafasi zao kama Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Bodi ya zabuni katika kipindi cha kati ya tarehe 5 mwezi Mei  na 28 mwezi Septemba mwaka 2009 walitumia mamlaka yao vibaya kwa  kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004. 

 

Washitakiwa walitenda kosa hilo kwa kumpatia LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED zabuni ya ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Mvomero awamu ya tatu kwa kufanya kazi moja tu ya uwekaji wa paa kwa gharama ya kazi zote zilizopaswa kufanyika katika zabuni iliyotangazwa ambazo ni; kuweka paa, kazi za bomba, plasta na umeme ambapo kwa kufanya hivyo waliisaidia kampuni ya LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED kupata manufaa isiyostahili ya mkataba wa Tsh 365,059,674/= .

Washitakiwa wote kwa pamoja kwa kitendo chao cha kutumia mamlaka yao vibaya kwa kukiuka sheria ya manunuzi ya umma kwa kumpatia zabuni LUCAS CONSTRUCTION COMPANY LIMITED kufanya kazi moja ya kuweka paa pekee kwa gharama ya kazi zote zilizopaswa kufanywa katika zabuni iliyotangazwa wameisababishia Serikali hasara ya TZS 83,455,474/= ikiwa ni gharama ya kazi ambazo hazikufanywa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya  mwaka 1984 (CAP 200)  (RE: 2002).kifungu cha 10(i) Jedwali la kwanza.

Washitakiwa hao wamefunguliwa Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba ECC 4/2014 katika Mahakama ya mkoa wa Morogoro na Kesi hii itakuja tena mahakamani tarehe 25/3/2014 kwa ajili ya maelezo ya awali (Preliminary Hearing).

Imetolewa na Eufrasia Kayombo,

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mvomero

Machi  11,2014

 

 

Mkurugenzi ashikiliwa na TAKUKURU kwa rushwa ya ngono Musoma

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKURUGENZI ASHIKILIWA NA TAKUKURU KWA RUSHWA YA NGONO MUSOMA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mara, inamshikilia Mkurugenzi wa Makoye Education Centre iliyopo eneo la Nyasho Manispaa ya Musoma - Bwana Joseph Makoye kwa tuhuma za kudai rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi aliyekuwa akifanya maandalizi yake ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne katika kituo hicho. Mtihani hiyo Kitaifa ilianza kufanyika tarehe 04/11/2013.

Awali mwanafunzi huyo wa kike ambaye jina lake linahifadhiwa, alifika katika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Mara na kutoa malalamiko yake kwamba alijisajili kufanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2013 kupitia S.L.P 216 linalomilikiwa na Makoye Education Centre, hivyo barua kutoka Baraza la Mitihani Tanzania inayomruhusu binti huyo kuingia kwenye chumba cha mitihani ilitumwa kupitia anuani hiyo. Baada ya barua hiyo kupokelewa katika kituo hicho, ilishikiliwa na mtuhumiwa ambaye kimsingi ndiye mmiliki wa sanduku hilo la barua kwa jina la Makoye Education Centre. Mtuhumiwa huyo badala ya kukabidhi barua hiyo kwa binti huyo, alianza kudai rushwa ya ngono ikiwa ni sharti la kumpatia barua hiyo, akimtahadharisha kuwa, kama binti huyo hatatoa rushwa ya ngono asingeweza kufanya mtihani wake kwa kuwa asingempatia barua hiyo toka Baraza la Mitihani la Tanzania.

TAKUKURU iliandaa mtego ili kumnasa mtuhumiwa katika eneo kilipo kituo cha Makoye Education Centre huko Nyasho tarehe 02/11/2013 majira ya saa moja (1) usiku ambapo mtuhumiwa alikuwa amempigia simu mwanafunzi huyo na kumtaka wakutane katika eneo hilo. Mtuhumiwa alifika kwenye eneo hilo majira ya saa moja na robo (1.15) usiku huo akiwa na gari Toyota Corola lenye namba za usajili T697 BNQ. Hata hivyo Mtuhumiwa hakushuka kwenye gari hilo bali alimwita binti huyo na akamlazimisha aingie kwenye gari na kisha akaondoka naye.

Makachero wa TAKUKURU walianza kufuatilia nyendo za gari hilo kwa tahadhari kuhakikisha kuwa binti huyo hapati madhara kwa namna yeyote ile hadi walipomtia mbaroni mtuhumiwa huyo katika nyumba ya kulala wageni ya Tedasi (Tedasi Lodge) iliyoko Bweri katika Manispaa ya Musoma.

Zoezi la upekuzi lilifanyika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo eneo la Mukendo kati ambapo fomu hiyo kutoka BARAZA LA MITIHANI LA TANZANIA iliweza kupatikana.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na mara utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa. TAKUKURU inawaasa mabinti wote wanaokutana na visa kama hivi vya unyanyasaji wa kijinsia kuwa na uthubutu wa kutoa taarifa TAKUKURU ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Imetolewa na Holle J. Makungu, Mkuu wa TAKUKURU (M) Mara

Tarehe 03.11.2013

 

Taarifa kwa Vyombo vya Habari Tukio la Ujambazi Zanzibar

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dkt. Edward Hoseah amesema tukio la ujambazi lililoripotiwa kutokea mjini Zanzibar Januari 13, 2014 na kumhusisha mtumishi wa TAKUKURU ni tukio lililoichafua sifa ya chombo hiki. Bofya hapa kusoma taarifa kamili

Mkuu wa Kitengo cha PMU Mvomero afikishwa Mahakamani

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mnamo tarehe 10/09/2013 TAKUKURU Wilaya ya Mvomero ilimfikisha mahakamani Bw. DAVID KIRINYA MAYIRA mwenye umri wa miaka 50 ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi (PMU) katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. (Kwa sasa amehamishiwa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kama Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi katika Manispaa hiyo).

Mshitakiwa huyo ameshitakiwa kwa makosa ya kutumia nyaraka zenye maelezo ya uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri na kutumia mamlaka yake vibaya chini ya vifungu vya 22 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kwamba akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, kwa nafasi yake kama Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, mnamo tarehe 20/05/2010 aliandaa taarifa ya kumpendekeza Mkandarasi M/S Tengo Contruction kufanya kazi ya ujenzi wa barabara ya Makao Makuu yenye urefu wa mita 700 (Kilomita 0.7) kwa gharama ya Tsh. 218,000,000/= (Milioni mia mbili kumi na nane tu), kwa njia ya ‘Direct contracting’ ambayo ilifanyika bila ushindani.

Bw. DAVID MAYIRA huku akijua kuwa mapendekezo hayo aliyafanya mwenyewe pasipo wajumbe wengine kushirikishwa, aliyawasilisha katika kikao cha Bodi ya Zabuni na kupelekea Mkandarasi kupewa zabuni hiyo kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004. Hivyo, kwa nafasi yake kama Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi anakabiliwa na kosa chini ya vifungu vya 22 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Mshitakiwa huyo amefunguliwa Kesi ya Jinai Namba 138/2013 katika Mahakama ya Wilaya ya Morogoro na kesi hii itakuja tena mahakamani tarehe 24/09/2013 kwa ajili ya maelezo ya awali (Preliminary Hearing).

Imetolewa na Eufrasia Kayombo,

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mvomero

Septemba 12,2013

Askari Polisi akamatwa kwa Rushwa - Musoma

TAKUKURU yafikisha Mahakamani vigogo wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kwa tuhuma za rushwa 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Mara inamshikilia ASKARI POLISI mwenye namba F.1863 MARIDAD DAVID KAPINGA wa Kituo Kikuu cha Polisi hapa Musoma.

Askari huyo alikamatwa na TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA Mnamo tarehe 10 September 2013 kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu ishirini (Tsh 20,000). Awali TAKUKURU ilipokea taarifa toka kwa Raia mwema akimlalamikia askari huyo kwamba anamdai rushwa ya shilingi elfu ishirini (Tsh 20,000/=) ili aweze kumrejeshea kitambulisho cha makazi kilichokuwa kinashikiliwa na askari huyo kama moja ya masharti ya dhamana ya kumdhamini ndugu yake aliyekuwa na tuhuma zilizofunguliwa katika kituo cha Polisi Kati - kwa kumbukumbu namba RB/2818/2013.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, mtego wa kumnasa uliandaliwa na maafisa wa TAKUKURU ambapo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa amekwisha kupokea fedha hizo katika eneo zilizopo ofisi za TANESCO MKOA WA MARA. Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na mara utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Askari huyo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara ndugu HOLLE MAKUNGU anawaasa ASKARI na watumishi wa umma kwa ujumla wao kuzingatia maadili ya kazi zao katika utekelezaji wa nyadhifa walizokabidhiwa.

Imetolewa na  Holle J. Makungu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara,

Septemba 11, 2013

Waliotaka kumhonga DC Kilindi Kizimbani

Mnamo tarehe 13/11/2013 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Kilindi iliwafikisha Mahakamani SHARIFF LEMANDA LEMTEKA Mkazi wa Lesoit KITETO na   EMMANUEL OLE KILELI mkazi wa Elerai kata ya KIBIRASHIWilayani Kilindi mkoa wa Tanga na kufunguliwawaa kesi ya jinai Na. CC. 228/2013. Washitakiwawanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na Kifungu cha 15 (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/20007.

Washitakiwa hao walinaswa tarehe 12/11/2013 kwenye mtego uliowekwa na TAKUKURU katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilindi.  Watuhumiwa walitenda kosa la kujihusiha na vitendo vya kushawishi na kutoa hongo ya Tsh 1,100,000/= kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Selemani Liwowa ili atamke kuwa eneo la Elerai lililopo wilayani Kilindi ni kijiji halali na kimeundwa baada ya kupitia taratibu zote za kisheria, jambo amabalo halikuwa la kweli.

Washtakiwa wote wawili walisomewa mashtaka na mwendesha mashataka wa TAKUKURU ndugu George Magoti mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. MALIGANA . Aidha, washitakiwa wote wawili walipata dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani hapo tarehe 28/11/2013.

TAKUKURU inatoa wito kwa wananchi wote kuzingatia maadili na kutokujihusisha na vitendo vya Rushwa. Imetolewa na;

EDSON MAKALLO

MKUU WA TAKUKURU (M),

TANGA

14/11/2013

Taarifa kwa vyombo vya habari 2

Mnamo tarehe 05/09/2013 Mahakama ya Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga ilimtia hatiani Bwana YOHANA KILUWASHA (65) kwa kosa la kushawishi kutoa Rushwa chini ya kifungu cha 15(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana Na Rushwa Na.11/2007.

Mshitakiwa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha ZEGE katika Kata ya Dindira Wilaya ya Korogwe alifikishwa Mahakamani hapo mnamo tarehe 27/09/2012 katika shauri la Jinai Na.99/2012 akikabiliwa na jumla ya makosa mawili ambapo alikutwa hana kesi ya kujibu katika shitaka la pili. Mshitakiwa alikuwa akiwashawishi kuwapa hongo ya shilingi 20,000/= vijana watatu waliokamata mbao zilizokuwa zimevunwa kinyume na agizo la Serikali kuzuia uvunaji katika msitu wa Sakare ili wasiseme ukweli kuhusiana na idadi kamili ya mbao walizokuwa wamezikamata na kumkabidhi mshitakiwa kwa Afisa Misitu Wilaya ya Korogwe.

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Mh. ARNOLD KIREKIANO. Mshitakiwa alihukumiwa kulipa faini ya shilingi 500,000/= au kutumikia kifungo cha miezi tisa (9) jela ambapo mshitakiwa alishindwa kulipa faini husika.

TAKUKURU inaendelea kutoa wito kwa watumishi wa umma, wanasiasa na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia maadili na kutokujihusisha na vitendo vya Rushwa.

Imetolewa na;

EDSON A. MAKALLO

MKUU WA TAKUKURU (M),

TANGA

06/09/2013

Subcategories

  • Download Centre

    Feugiat convallis turpis massa ligula sagittis enim aliquet fringilla orci pretium. Ut Aenean Vestibulum suscipit eros pede et nibh laoreet Pellentesque mus. Aliquet ultrices dictumst justo justo tortor vitae nisl nec sem.

  • Research Papers

    Lorem ipsum dolor sit amet consectetuer pede cursus Pellentesque eros nulla. Pretium nibh feugiat Fusce nibh Curabitur consectetuer In arcu est eros. Phasellus Aliquam vitae hendrerit cursus nec elit Nam Quisque volutpat Phasellus. Id nibh interdum vitae nec enim cursus pretium pellentesque Aenean laoreet. Quisque gravida metus natoque ridiculus ac vitae mollis In Quisque suscipit. In et Fusce lorem gravida Morbi.

  • Press Releases
  • Publications

    Auctor pellentesque lobortis enim urna gravida nunc sit ligula sit eget. Suscipit sociis elit felis sed tincidunt feugiat urna orci Nam Integer. Curabitur metus pulvinar condimentum Pellentesque quam massa sed vel velit Morbi. Vestibulum dictum purus dolor Curabitur Donec malesuada faucibus congue augue et. Pellentesque pretium eu consectetuer id Proin Curabitur risus Vestibulum lorem Lorem. Turpis ullamcorper in condimentum Donec Sed Phasellus.