Muuguzi ahukumiwa jela miaka mitatu kwa kosa la kujipatia ajira kwa cheti cha kufoji

Akitoa hukumu hiyo, hakimu Mushi alisema mahakama inamuona na hatia kama alivyoshtakiwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi  wanne wa upande wa jamhuri bila kuacha shaka yoyote.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Eric Kiwia aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa kwake mwenyewe na watu wengine wenye tabia hiyo.

Kwa upande wake, mshtakiwa aliiomba mahakama imwonee huruma kwa kuwa ni mja mzito na ana ugonjwa wa homoni ambao haumruhusu kukaa kwenye eneo lenye joto kali.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani na Jamhuri kwa mara ya kwanza 15Novemba, 2015na kufunguliwa mashtaka mawili ya kufoji cheti cha elimu ya sekondari na kutumia cheti hicho kujipatia ajira ya uuguzi Hospitali ya Mkoa Mara.

Awali ilidaiwa mahakamani na  upande wa mashtaka kuwa kati ya Mei na Septemba, 2009 katika tarehe na maeneo yasiyofahamika mshtakiwa alitenda kosa la kufoji cheti cha kuhitimu elimu ya sekondari Forodhani mwaka 1995.

Aidha ilidaiwa kuwa Septemba 3, 2009 mshtakiwa aliwasilisha cheti cha kufoji kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na hivyo kuweza kuajiriwa kama muuguzi katika hospitali ya Mkoa wa Mara.

Akitoa adhabu hakimu Mushi alisema amezingatia utetezi wa mshtakiwa, hivyo akamhukumu kulipa faini ya Sh.500,000/= au jela miaka mitatu kwa kosa la kwanza na kosa la pili faini Sh.100,000/= au kwenda jela miaka mitatu.

Hakimu Mushi alimhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini Sh.600, 000/= kwa kuwa adhabu zinaenda pamoja.

Mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Ostac Mligo alilipa faini ya Sh.600, 000/= na hivyo kukwepa kwenda jela kutumikia kifungo miaka mitatu.