DIWANI NA MTENDAJI WA KATA WALIOJIMILIKISHA TREKTA LA MRADI WA VIJANA WAPANDISHWA KIZIMBANI

Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Eric Kiwia ameiambia mahakama kuwa kati ya tarehe 9Machi, 2015 na 24 Julai, 2015 washtakiwa kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kununua trekta aina ya Masey Ferguson toka kampuni ya Kilasa kinyume na kanuni 163(1) na 164(1) za Kanuni za Manunuzi ya Umma za 2003 kitendo ambacho kiliinufaisha kampuni ya Kilasa kiasi cha Tsh.57,000,000/=.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa uchunguzi wa kesi hiyo umekamilika na uko tayari kwa usikilizwaji wa awali (ph) kwa tarehe itakayopangwa na mahakama na haukuwa na pingamizi kwa dhamana ya washtakiwa.

Mshtakiwa  wa kwanza ambaye ni Ekwabi Dennis Michael yuko nje kwa  dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo walitakiwa kulipa pesa taslimu Sh.14,250,000/= au kuwa na mali isiyo nhamishika yenye thamani ya Sh. 14,250,000/=  pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alitakiwa kusaini bondi ya Sh. 14,250,000/=.

Kesi imeahirishwa hadi tarehe25 Aprili mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali.

Tarehe 29.06.2013 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ilihamisha fedha kiasi cha shilingi million hamsini  kwenda katika akaunti ya mfuko wa maendeleo ya kata ya Suguti kwa ajili ya ununuzi wa trekta la kikundi cha vijana kata ya Suguti. Uhamishaji wa fedha hizo ulitokana na maombi yaliyowasilishwa kwenye baraza la madiwani na mshitakiwa Ekwabi Dennis Michael kama kipaumbele cha kata ya Suguti.

Diwani Ekwabi Dennis Michael (ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Maendeleo ya Kata) na  Jackson Mgendi Marwa (Katibu wa kamati hiyo), wote wakiwa watia sahihi wa akauti ya mfuko wa maendeleo ya kata, tarehe 02/12/2013 walichukua fedha hizo Tshs. 50,000,000/= kutoka akaunti namba 3032301513 iliyoko NMB Musoma kwa maelezo ya kwenda kununua trekta la kikundi cha vijana Suguti.

 Baada ya kutoa fedha hizo toka benki, kwa nia ovu na bila maelezo yoyote, walikaa na fedha hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu hadi tulipopata taarifa hizo. Baada ya uchunguzi kuanzishwa, mshitakiwa wa kwanza ambaye ni Ekwabi Dennis Michael alienda Mwanza kwenye kampuni ya Kilasa

na kununua trekta aina  ya Massey Furguson kwa Tshs.57,000,000/=.

Trekta hilo alilinunua kwa jina lake na kwa kukiuka kanuni za 163(1) na 164 (1),  za Kanuni za Manunuzi ya Umma za  mwaka 2013 na manunuzi hayo yasiyozingatia sheria yaliiwezesha Kampuni ya Uuzaji Matrekta ya Kilasa kujipatia Manufaa isiyostahili ya Tshs.57,000,000/=.

Pamoja na ukiukwaji wa sheria ya manunuzi, Edwabi Dennis Michael hakukabidhi trekta wala kuujulisha uongozi  na wanachama wa kikundi cha vijana kata ya Suguti kuhusiana na kuwepo kwa fedha zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa ajili ya ununuzi wa trekta la kikundi hicho.  Kwa msingi huo Ekwabi Dennis Michael ameendelea kulimiliki trekta na kujinufaisha nalo badala ya kikundi cha maendeleo ya vijana Suguti kinyume na Sera ya Taifa ya kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.