WAHUJUMU PEMBEJEO ZA KILIMO WAHUKUMIWA KWENDA JELA

Hukumu hii  imetolewa alhamisi iliyopita  na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Gabriel Kurwijila  baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka ulioongozwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Kelvin Murusuri akisaidiana na Bi. Husna kiboko.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza 27Julai,2016 na kusomewa mashtaka ya makosa 74 yanayohusiana na kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Mbali na wakala wa pembejeo kushtakiwa kwa kosa moja la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu washtakiwa kwa pamoja walishtakiwa kwa makosa 73 ya kughushi,moja la kusaidia kutenda kosa ambayo ni kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Katika hukumu hii John sitta kalabo na Bakar Iddi Muktar walihukumiwa kifungo cha miaka 2 jela au kulipa faini ya Shilingi 2,000,000/= kwa makosa ya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu Na. 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.

Aidha John sitta kalabo na Bakar iddi muktar  walihukumiwa na mahakama kifungo cha miaka 3 jela bila kulipa faini, kwa makosa 73 ya kughushi nyaraka kinyume na vifungu vya 333,335,337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (CAP 16 ya mwaka 2002).

Wakala wa pembejeo za kilimo Bakar Iddi Muktar amehukumiwa miaka mitatu jela kwa kosa la la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (CAP 16 ya mwaka 2002).

Pia Afisa Ugani wa Kata ya Ikobe wilaya ya Mbogwe  Idrisa Mohamed amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja au kwenda jela miezi kumi na mbili kwa kosa la kumsaidia wakala wa pembejeo za kilimo Bakar Iddi, kutumia nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya Mkurugenzi wa halmashaur ya wilaya ya Mbogwe kuwa wakala huyo amesambaza pembejeo hizo jambo ambalo si kweli.

Aidha mahakama iliwaachia huru washtakiwa Kulwa Rashid na Samwel Nalumbikya Makala ambao ni Maafisa kilimo wa Wilaya baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashtaka  dhidi yao ya kumsaidia wakala wa pembejeo Bakar iddi kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wake ambaye ni halmshauri ya wilaya ya mbogwe kuwa pembejeo za kilimo zilisambazwa katika kijiji cha Ishigamva kata ya ikobe jambo ambalo lilikuwa si kweli.

 Washtakiwa wote walikuwa wanatetewa na wakili wa kujitegemea Makanjero Ishengomana  na hukumu ilitolewa bila Mtendaji wa Kijiji cha Ishigamva John sitta kalabo kuwepo mahakamani baada ya kutoroka wakati inaendelea.

Kwa kuwa adhabu zinaenda pamoja kwa makosa ya kutumia hati za uongo na kughushi nyaraka mahakama iliamuru John Sitta Kalabo na Bakar Idd Muktarambaye waende jela kutumikia kifungo cha miaka 3 na kulipa faini ya Sh.2,560,000/= baada ya kumaliza kutumikia kifungo.

Pamoja na hayo Mahakama iliamuru kwa kuwa mshitakiwa bwana John Sitta Kalabo (Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ishigamva ) hakuwepo mahakamani wakati hukumu inatolewa mara tu atakapopatikana ataanza kutumikia adhabu yake.

Afisa Ugani wa Kata ya Ikobe wilaya ya Mbogwe  Idrisa Mohamed alipelekwa jela kutumikia kifungo cha cha miezi kumi na mbili baada ya kushindwa kulipa  faini ya Sh.1,000,000/=.