Maafisa Wizara ya Afya Wapandishwa Kizimbani kwa Makosa ya Rushwa.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Mhe. Janeth Kaluyenda, Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza Bw. Arnold Shada kati ya Septemba na Disemba 2008, alitumia madaraka vibaya katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema kuwa, mshtakiwa alishindwa kutoa maelekezo ili jina la Bi. Rhotha Mboyaliondolewe katika orodha ya mishahara kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007.

Bi. Gura alidai katika shitaka la pili kuwa mshtakiwa aliisababishia Serikali hasara ya Shs.1, 091,904.75 iliyotokana na mtumishi huyo mstaafu kulipwa fedha hizo kupitia akaunti ya benki kinyume na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Na 200 ya 2002.

Bi. Gura alidai kuwa mshtakiwa wa pili Bi. Prisca Lwangili kati ya Februari na Juni 2008 alitumia madaraka vibaya kwa kushindwa kutoa maelekezo kwa Mhasibu Mkuu wa Wizara kuondoa jina la Bi. Kaanansia Mmari katika orodha ya malipo ya mshahara baada ya kustaafu.

Mwendesha Mashtaka huyo alisema, shitaka la pili linalomkabili mshtakiwa ni kuisababishia Serikali hasara ya jumla ya Shs. 1,682,653.52 baada ya Bi. Mmari kulipwa mshahara isivyo halali kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU akisoma mashtaka dhidi ya Bi.Agnes Hugo alidai kuwa kati ya Aprili na Oktoba 2008, alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutoa maelekezo ya kuondoa jina la mtumishi Bi. Edith Maimu katika orodha ya malipo ya mshahara baada ya kustaafu utumishi wa umma. Bi. Gura aliieleza mahakama kuwa kutokana na uzembe wa mshtakiwa mtumishi huyo Bi. Maimu alilipwa jumla ya Shs. 942,599.76 isivyo halali.

Kesi hii ilifunguliwa Agosti 8, 2015 na washtakiwa wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali na kila mmoja kusaini dhamana ya Shilingi milioni mbili.