SAKATA LA ESCROW: VIGOGO WA BOT, TRA, TANESCO, REA NA ARDHI WAPANDISHWA KIZIMBANI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, imewafikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, watumishi watano waaandamizi wa umma kwa tuhuma za kuhusika na rushwa katika sakata la Escrow.

Watuhumiwa hao ambao walifikishwa mahakamani katika siku mbili tofauti ni Bw. Teophil John, ambaye ni Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini - REA, anayetuhumiwa kupokea fedha za Tanzania shilingi milioni 161.4 kutoka kwa mfanyabiashara Bw. James Rugemarila, fedha zinazodaiwa kuwa zilitolewa katika mazingira ya rushwa.

Mtuhumiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Rugonzibwa Teophil ambaye kwa mujibu wa hati ya mashtaka, yeye anatuhumiwa kupokea fedha shilingi milioni 323, kutoka kwa Bw. Rugemarila pia katika mazingira yanayodhaniwa kuwa ni ya rushwa.

Katika kesi inayomkabili Bw. John, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bw. Leonard Swai ameeleza kuwa mtuhumiwa akiwa kama mtumishi wa umma, alipokea fedha hizo kupitia akaunti aliyoifungua kwenye benki ya Mkombozi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam. Hakimu anayesimamia kesi hiyo, Frank Moshi, amemwachia mtuhumiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanye fedha za Tanzania shilingi milioni 25 kila mmoja.

Katika shtaka linamkabili Bw. Rugonzibwa, Hakimu Mfawidhi Bw. Emilius Mchauru amemtaka mtuhumiwa huyo kuwa na mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha pesa alichokipokea, pamoja na wadhamini wawili ambao kila mmoja atawasilisha mahakamani hapo fedha za Tanzania shilingi milioni kumi.

WAKATI HUO HUO:

MKURUGENZI wa Fedha wa Benki Kuu, Julius Angello, Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Mutabingwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea rushwa ya zaidi ya Sh bilioni mbili kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Washtakiwa hao walipandishwa jana kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mahakimu wawili tofauti na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Leonard Swai.

MUTABINGWA
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda, mshtakiwa Mutabingwa anayekabiliwa na mashtaka manne, alidaiwa kutenda makosa hayo Januari 27, 2014 maeneo ya Benki ya Mkombozi iliyopo Manispaa ya Ilala.
 
Inadaiwa mshtakiwa akiwa katika wadhifa wake wa Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, alipokea rushwa ya Sh 1, 617,000,000 kupitia akaunti namba 00110202613801, fedha hizo ni miongoni mwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow, alipokea kutoka kwa Mshauri wa Kimataifa ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira.
 
Mshtakiwa anadaiwa kupokea tuzo hiyo kwa kuiwakilisha TRA na wakati huo huo Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits inayomilikiwa na Rugemalira katika moja ya kesi zake zilizoko Mahakamani.
 
Swai alidai katika shtaka la pili kuwa, Julai 15 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00110202613801, fedha za Escrow kutoka kwa Rugemalira.
 
“Mheshimiwa shtaka la tatu, inadaiwa Agosti 26 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi, mshtakiwa alipokea rushwa tena ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti hiyo hiyo kutoka kwa Rugemalira na fedha hizo zilikuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.


“Shtaka la nne anadaiwa Novemba 14 mwaka jana kwa kutumia akaunti yake hiyo alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kutoka kwa Rugemalira, fedha ambazo zilikuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alidai Swai.
 
Swai alidai upelelezi wa kesi umekamilika na aliomba tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
 
Pamoja na hilo, Swai alisema mshtakiwa hakuwa na pingamizi la dhamana isipokuwa aliomba Mahakama ifunge akaunti yake mpaka kesi itakapomalizika.
 
Hakimu Kaluyenda alisema mshtakiwa atadhaminiwa baada ya kutimiza masharti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh bilioni moja ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, wadhamini watatu watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 340 kila mmoja, wadhamini wawili wawe na kazi ya kuaminika, wawasilishe kitambulisho na mshtakiwa hatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali.
 
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hati za nyumba hazikuwa na ripoti ya mthamini kuonyesha thamani yake hivyo alirudishwa rumande hadi atakapotimiza masharti, kesi itasikilizwa Januari 29 mwaka huu na tayari akaunti yake imefungwa.
 
URASSA
Swai akisoma mashtaka dhidi ya Urassa mbele ya Hakimu Kaluyenda alidai, Februari 14 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, mshtakiwa akiwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00120102658101 kutoka kwa Rugemalira, fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia tuzo hiyo baada ya kuiwakilisha Tanesco na IPTL katika kesi ya Standard Charter nchini Hong Kong.
 
Urassa alikana mashtaka, upelelezi wa kesi umekamilika, upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi la dhamana isipokuwa aliomba akaunti ya mshtakiwa ifungwe kutumika mpaka kesi itakapomalizika.
 
Hakimu Kaluyenda alikubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti ya kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni 81 ama hati ya mali isiyohamishika, wadhamini wawili wafanyakazi, barua kutoka ofisini na kitambulisho.
 
Mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana lakini hakuweza kuwasilisha ripoti ya mthamini kujua thamani ya mali yake.
 
Hakimu Kaluyenda alisema mshtakiwa alishakuwa mfanyakazi wa Tanesco ni wakili hivyo mahakama inakubali kumpa dhamana na upande wa mashtaka waendelee kuhakiki hati. Kesi itasikilizwa Februari 2 mwaka huu.
 
ANGELLO
Mshtakiwa Angello alipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai.
 
Swai alidai mshtakiwa Februari 6 mwaka jana maeneo ya Benki ya Mkombozi, akiwa Mkurugenzi wa Fedha wa BoT alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00120102646201 kutoka kwa James Rugemalira.
 
Fedha hizo zinadaiwa zilikuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, alipokea kama tuzo kutokana na malipo yaliyotolewa katika akaunti hiyo kwenda kwa Pan Africa Solutions Limited (PAP).
 
Mshtakiwa alikana mashtaka, upelelezi umekamilika, waliomba tarehe nyingine ya kuanza kusikiliza kesi na waliomba mahakama iamuru kufungwa kwa akaunti ya mshtakiwa.
 
Hakimu Kisoka alikubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh 80,800,000 au hati ya mali yenye thamani hiyo, wadhamini wawili, kila mmoja asaini dhamana ya maneno ya Sh milioni 50, mdhamini mmoja kutoka serikalini na mwingine anayeishi Dar es Salaam.
 


Alisema hati ya nyumba lazima iwe na ripoti ya mthamini kuonyesha thamani yake halisi bila hivyo hawezi kutoa dhamana.
 
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti, alirudishwa rumande na kesi itaendelea kusikilizwa maelezo ya awali Januari 27 mwaka huu.
 
Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amewasilisha ilani ya kuzuia fedha zilizomo katika akaunti ya Rugonzibwa Mujunangoma anayedaiwa kupokea rushwa ya zaidi ya Sh milioni 300, aliyefikishwa mahakamani Jumatano ya wiki hii mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru.
 
Hadi sasa washtakiwa watano tayari wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kupokea rushwa kwa Rugemalira kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

MAWAZIRI WAWILI WA ZAMANI WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA TISA

 

Mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona (Nishati na Madini), wamehukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Tsh 5,000,000/-, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.5 bilioni.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu - Sam Rumanyika alisema, baada ya jopo la mahakimu watatu kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 13 wa upande wa mashtaka na wengine sita wa utetezi wakiwamo washtakiwa wenyewe, wameamua kumwachia huru mshtakiwa wa tatu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Hakimu Rumanyika alisema wanamuachia huru Mgonja kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yote 11 yaliyokuwa yakimkabili.

Hakimu Rumanyika alisema wanamtia hatiani Mramba katika mashtaka yote 11 yaliyokuwa yakimkabili ambapo katika shtaka la kwanza hadi la 10 ambayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka, atakwenda jela kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila shtaka na vifungo hivyo vitakwenda sambamba, hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Katika shtaka la 11 ambalo ni la kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni pia alitiwa hatiani na kuhukumiwa ama kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa fidia ya Sh5 milioni na kuwa vifungo hivyo vyote vitakwenda sambamba hivyo Mramba atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Kuhusu Yona, Hakimu Rumanyika alisema, naye wanamtia hatiani katika shtaka la kwanza, la pili, la tatu na la tano ambayo ni ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na shitaka la 11 la kuisababishia hasara Serikali ya Sh11.7 bilioni.

“Yona katika kila kosa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na adhabu zote zinakwenda sambamba hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Alisema Rumanyika. “Katika shtaka la kusababisha hasara atalipa fidia ya Sh5 milioni na iwapo atashindwa atakwenda jela miaka mitatu,” alimaliza Hakimu Rumanyika.

Tandahimba imewafikisha mahakamani watuhumiwa watatu

TAKUKURU YAFUNGUA KESI YA JINAI (CC. NO.50/2014).

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (W) ya Tandahimba imewafikisha mahakamani watuhumiwa watatu tarehe 27/05/2014. Watuhumiwa hao ni ndugu Athumani Juma Mwihumbo ambaye ni Mweyekiti wa Kuchele Amcos, Said Hamis Chivanga ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kuchele Amcos na Hassan Chinanda, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkonjowano. Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tandahimba na kufunguliwa Kesi ya Jinai (CC. NO.50/2014) mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, Mh. Paulo Ntumo.

Watuhumiwa wote watatu walisomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, bwana Sospeter Teah ya kwamba wameshtakiwa kwa kukiuka kifungu cha 28 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 na vifungu vya 258 na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (cap 16 R.E 2002). Washtakiwa wote walikana mashtaka na walipewa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Aidha shauri hili limepangwa kusikilizwa tena tarehe 12/06/2014 katika mahakama hiyo ya Wilaya ya Tandahimba.

TAKUKURU Mkoa wa Mtwara tunaendelea kutoa wito kwa wananchi wa mkoa huu kwamba waendelee kutoa ushirikiano kwa chombo hiki ili tuweze kuhakikisha kuwa tunamaliza kero ya rushwa katika mkoa wetu.

Imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara – Edson Makallo,

Juni 05, 2014.

Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Songea anaswa kwa Rushwa

Mnamo tarehe 03/03/2015 TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea akishirikiana na baadhi ya wanakijiji wa Kijiji cha Makwaya kata ya Muhukulu, wamepanga kutoa rushwa kwa Hakimu anayeendesha kesi ya Maliasili ambayo ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Songea kwa lengo la kutaka kufuta kesi hiyo.

Baada ya kupokea malalamiko, TAKUKURU walifanya uchunguzi wa awali ambao ulihusisha kufika hadi Mahakama ya Wilaya ambako nako uchunguzi ulibaini kuwa kuna mazingira ambayo yalionesha kuwa watuhumiwa walipanga kutoa rushwa kwa hakimu anayeendesha kesi hiyo bila hakimu kujua mipango hiyo.

Ili kuthibitisha kuwepo mazingira ya kutaka kutoa rushwa TAKUKURU iliweka mtego ambao baadaye ulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wafuatao ;

  1. HOTAY TLUWAY (43), MWANASHERIA WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA
  2. SIRAVIANI MBARARE (MAISHA) (37), MKAZI WA KIJIJI CHA MAKWAYA NA NI MMOJA WA WASHITAKIWA WA KESI YA MALIASILI AMBAYO IKO MAHAKAMANI.

Walikamatwa wakitoa fedha Tshs. 330,000/= kwa hakimu ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sasa.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

TAKUKURU yakamata magogo – Mkuranga - Pwani.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, imekamata malori matano(5) yaliyokuwa yamesheheni magogo yaliyozidisha kiwango cha tani zilizokubaliwa lakini pia yaliweza kupitishwa bila kutozwa faini katika kituo cha mizani – MIKINDU kilichopo barabara ya Kilwa, kinyume na utaratibu, baada ya kuwa wametoa hongo kwa  wasimamizi wa mizani hiyo.

Malori hayo yalikamatwa Alhamis tarehe 16/09/2010 alfajiri ambapo TAKUKURU kwa kushirikiana na wataalamu wa TANROADS Mkoani Pwani walipima upya mizigo hiyo baada ya kuwa imeshavushwa na wahusika walitozwa faini ya Tsh 17,515,850/= (Milioni kumi na saba, laki tano na kumi na tano elfu, mia nane na hamsini tu), fedha ambayo serikali tayari ilishaipoteza.

Uchunguzi dhidi ya tuhuma hiyo bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini iwapo magogo yaliyokamatwa yalikuwa na kibali cha kuvunwa na iwapo yaligongwa mihuri husika baada ya kukaguliwa.

Tunapenda kuujulisha umma kuwa TAKUKURU inatekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Sheria ambayo ni Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007.

Sheria hii ndiyo inayotoa mamlaka ya kuchunguza, kuhoji na hata kukamata mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa bila kujali cheo, dini, chama wala wadhifa alionao.  

Vilevile TAKUKURU inaendelea na uchunguzi dhidi ya watuhumiwa ikiwa ni pamoja na waliotuhumiwa katika kipindi cha kura za maoni za CCM na yeyote atakayethibitika kuwa alitenda vitendo vya rushwa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.