JIVUNIE UNAPOSEMA ‘SIRUBUNIKI KWA RUSHWA.’

 

 

Sidebar

TAKUKURU Ngorongoro yaokoa milion 6 mishahara hewa

Robert Rwezaura, Ngorongoro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ngorongoro imeokoa zaidi ya shilingi milioni 6 kutokana na malipo ya mishahara hewa kwa watumishi waliofukuzwa kazi katika hospitali ya Wasso iliyopo Ngorongoro Machi 22, 2017.

Awali katika shauri hilo Hospitali ya Wasso ilipokea Shilingi 2,481,301 kama mishahara ya watumishi wawili ambao tayari walishaachishwa kazi na uongozi wa Hospitali hiyo lakini bado mishahara hiyo iliendelea kupokelewa hospitalini hapo bila kurejeshwa hazina kama mishahara hewa kwa watumishi ambao hawapo kazini.

Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Ngorongoro baada ya kupata taarifa hizo ilianza kufanya uchunguzi na kubaini kuwa Hospitali ya Wasso iliendelea kupokea mishahara kutoka serikalini ya watumishi ambao ilikwisha waachisha kazi bila kuzirejesha hazina.

Aidha, TAKUKURU ilibaini kuwa Bw.Julius Ole Sitoy awali alikuwa mtumishi wa hospitali ya Wasso akiwa kama mlinzi wa hospitali hiyo  na baadae kufukuzwa kazi  Aprili 13, 2015 lakini bado aliendelea kupokea mshahara tangu Mei, 2015 hadi Machi 2016 akilipwa jumla ya kiasi cha Tshs.1,426,812 kinyume taratibu za utumishi wa umma kwa mtu aliyefukuzwa kazi.

Pia TAKUKURU ilibaini kuwa Bw. Daudi Salya Nambololo ambaye nae alikuwa mtumishi wa Hospitali ya Wasso Hospital katika kituo cha Digodigo kama mlinzi, aliachishwa kazi   Septemba 25, 2015 lakini Pamoja na kuachishwa kazi bado ailiendelea kulipwa mshahara  kutoka serikalini kuanzia  Oktoba 2015 hadi Machi 2106 yenye jumla ya Tshs.1,054,489

Baada ya uchunguzi kufanyika na kufanya mahojiano na Hospital ya Wasso walikubali kufanyika kwa makosa hayo na kuanza kurejesha pesa yote iliyokuwa imelipwa kimakosa  kiasi Tshs.2,481,301 walichokuwa wamekipokea kutoka serikalini kama mishahara ya watumishi wawili waliokuwa wameachishwa kazi.

Aidha, pesa hiyo ilirejeshwa kwa katibu Mkuu Hazina kupitia CSP Misc.Deposit,Bank of Tanzania akaunti namba 9921167201 Dar-es-Salaam kwa hundi namba 065023 ya             Januari 11, 2017 kupitia Fund Transfer Request Form namba 0931185.

Wakati huohuo Bw. Nehemia Mshote fundi sanifu maabara katika Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mnamo Julai 15, 2015 kwa ridhaa yake mwenyewe aliamua kuacha kazi kwa kuandika barua ya masaa 28, lakini bado aliendelea kupokea mishahara kupitia katika akaunti yake namba 41110001166 iliyopo benki ya NMB tawi la Loliondo jumla ya kiasi cha        Tshs.4, 925,000.

Aidha, Baada ya ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro kufanya uchunguzi mtuhumiwa na kulifatilia kwa karibu swala hilo Bw.Nehemia Mshote aliamua kurejesha kiasi cha         Tshs.4, 182,000/= kati ya Tshs.4, 925,000/= alizochukua.