TANZANIA YAELEZA UMUHIMU WA MATAIFA KUSHIRIKIANA KATIKA JITIHADA ZA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA DUNIANI.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 8 wa Mwaka, wa Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani – The 8th Annual General Meeting of International Association of Anti Corruption Authorities (IAACA), wameelezwa juu ya umuhimu wa kukuza mahusiano na ushirikiano katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa katika nchi zao.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Dkt Edward Hoseah, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho hili - Jumamosi tarehe 31/10/2015 wakati wa sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo.

Dkt Hoseah amesema, nchi wanachama wa IAACA, hawana budi kuongeza ushirikiano pale ambapo nchi moja inahitaji taarifa au msaada wa kiuchunguzi kutoka kwa nchi nyingine - kuhusu mali zinazofichwa nje ya nchi, ili kuharakisha na kufanikisha upatikanaji wa mali hizo haramu zilizopatikana kwa njia ya rushwa na kufichwa nje ya nchi husika.

Akitoa uzoefu kwa nchi ya Tanzania, Dkt Hoseah amesema, ni wakati muafaka kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuifanyia marekebisho Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 ili iwe na uwezo wa kufilisi. Amesema hatuna budi kuboresha sheria yetu kwa kuongeza kipengele cha kuwezesha kufilisi mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa au kwa njia nyingine zisizo halali, au kwa kupitia njia ya madai mahakamani, kama nyongeza katika njia ya sasa ambayo ili kufilisi mali tunatumia Sheria ya makosa ya Jinai ambapo inalazimu kuthibitisha kuwa mali hizo ni sehemu ya rushwa pasipokuwa na shaka.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huu umejadili nada zifuatazo:

 1. Uzuiaji Rushwa kama mbinu muhimu katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa

(Prevention as a key tool in the fight against corruption)

 1. Mapambano dhidi ya Rushwa kwa njia ya uelimishaji umma

(Tackling corruption through education)

 1. ‘Public Private Partnerships’ na ushirikiano wa sekta zote katika jamii.

(Public Private Partnership: towards committment, participation and cooperation among all sectors of the society.

IAACA ni shirikisho linalojumuisha pamoja Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani kwa lengo la kuziwezesha kubadlishana uzoefu, kusaidiana katika uchunguzi pamoja na kujadili changamoto na mikakati mipya ya kuzuia na kupambana na rushwa katika nchi zao.

Mkutano huu utafuatiwa na 6th Session of Conference of State Parties unaondaliwa na United Nations Convention Against Corruption (UNCAC), utakaoanza Novemba 2 – 6 hapa hapa jijini St. Petersburg – Russia.

Imetolewa na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU –Doreen Kapwani, St Petersburg- Russia, Tarehe 01/11/2015

RAIS KIKWETE AAGANA NA TAKUKURU

DG na JK

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dkt. Edward Hoseah kwa niaba ya watumishi wa Umma akimkabidhi Tuzo Maalum Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua mchango wake katika kuboresha Utumishi wa Umma nchini wakati wa sherehe ya Watumishi wa Umma kumuaga Rais iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Alhamisi tarehe 22/10/2015.

Dkt. Hoseah azindua jengo la Ofisi TAKUKURU Mbeya, aeleza Serikali ya Rais Kikwete imeimarisha mapambano dhidi ya rushwa

 

 • Awataka wananchi kuchagua kiongozi asiyejihusisha na rushwa

 • RC Mbeya awataka wananchi kuacha kuomba rushwa wanasiasa

 • Jamii yahamasishwa kupigania TAKUKURU kupewa mamlaka ya kushitaki

Na Matai Kirumbi, Mbeya

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dkt. Edward Hoseah leo Oktoba 5, 2015 amezindua jengo jipya la Ofisi ya TAKUKURU Mbeya na kueleza hatua thabiti zilizochukuliwa na Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Dkt. Hoseah alieleza kuwa pamoja na kuwepo changamoto nyingi, uimarishaji huo wa TAKUKURU uliofanyika chini ya Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kati ya mwaka 2005 na 2015, umeiwezesha Taasisi kushughulikia kwa mafanikio kero za rushwa nchini.

Aliyataja mafanikio hayo kuwa pamoja na TAKUKURU kufungua na kushinda kesi kubwa za rushwa 1,993ikilinganishwa na kesi 384 za kati ya mwaka 1995 na 2004 na kuokoa fedha za umma shilingi bilioni 88. “Hizi ni fedha ambazo, tusingedhibiti na kufanya uchunguzi, zingepotelea kwenye mikono ya walarushwa,” alisisitiza Dkt. Hoseah. Alifafanua kuwa rushwa ina athari kubwa kiuchumi kwa sababu tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza asilimia 30 ya pato la Taifa kwa njia ya rushwa wakati Afrika, kati mwaka 1999-2000, ilipoteza dola za Marekani bilioni 200 kwa njia ya rushwa. Alisema fedha hii ingekuwa na manufaa makubwa iwapo ingerudi katika kugharamia shughuli za maendeleo ya wananchi.

Alieleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Kikwete kati ya mwaka 2005 hadi 2015, Taasisi hii imeimarishwa zaidi kwa kutungwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010. Pia kwa upande wa jukumu ka kuzuia vitendo vya rushwa, TAKUKURU imeelimisha zaidi ya wananchi milioni tano kupitia semina na mikutano na kuwafikia wengine kwa njia ya kurusha vipindi vya redio 666, vipindi vya televisheni 130 na kushiriki katika maonesho 88.

TAKUKURU imefanikiwa pia kuanzisha klabu za wapinga rushwa 7,087zenye wanachama 505,249 nchi nzima. “Tunaamini kwamba kutumia muda wetu kuhamasisha vijana tunafanya kazi nzuri zaidi ya kujenga kizazi chenye mwamko lakini zaidi kizazi kinachochukia rushwa,” aliongeza Dkt. Hoseah.

Aidha, uelimishaji umma unafanyika kupitia luninga inayojazwa upepo (inflatable balloon) na magari ya matangazo, hasa kipindi hiki cha uchaguzi, ambapo wananchi wanaelimishwa kuhusu thamani ya kura. Thamani hiyo inajumuisha wananchi kukataa kushiriki katika vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi. Dkt. Hoseah alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanamchagua kiongozi bora asiyejihusisha na vitendo vya rushwa kwani kiongozi bora ndiye atakayeleta maendeleo ya kweli.

Vilevile, TAKUKURU imefanya tafiti 146 katika sekta mbalimbali kwa madhumuni ya kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza jinsi ya kuiziba. Mathalani utafiti wa kupima joto la rushwa na utawala bora nchini (National Governance and Corruption Survey - NGACS) umesaidia kubainisha mianya ya rushwa iliyopo, sekta inayolalamikiwa zaidi na nini kifanyike ili kudhibiti mianya ya rushwa katika mifumo.

Dkt. Hoseah aliyataja mambo mengine yaliyofanywa na Serikali kuimarisha TAKUKURU kuwa ni kuipatia vitendea kazi vya kisasa, kuiongezea ambapo sasa ina watumishi 2087 ikilinganishwa na watumishi 400 kabla ya mwaka 2005 na kupanua wigo wa ofisi kwa kuwa na ofisi 127.

Awali akieleza kuhusu ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu huyo wa TAKUKURU alisema limegharimu shilingi 1,296,486,673. Alifafanua kwamba chini ya mkakati wa TAKUKURU wa kujenga ofisi tatu kila mwaka kulingana na fedha za maendeleo ambazo Serikali huzitoa, hivi sasa Taasisi ina majengo 18 ambapo ya mikoa ni 12 na ya wilaya yapo sita. Dkt Hoseah alieleza kuwa TAKUKURU imefanikiwa kupunguza sana gharama za ujenzi wa majengo yake kwa kuamua kutumia watumishi wenye taaluma hiyo ambao hufanya usanifu na usimamizi wa ujenzi.

Wito wangu kwa watumishi wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya ni kwamba mlitunze na kulithamini jengo hili ili liweze kutumika na vizazi vijavyo… mimi kama kiongozi wenu nitahakikisha kuwa mnapata samani nzuri pamoja na vitendea kazi vya kisasa kabisa vitakavyoendana na jengo hili,” alisisitiza Dkt. Hoseah.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro katika salaam za mkoa, alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa kuhakikisha watumishi wanapata mahali pazuri pa kazi kwa kujenga jengo zuri na kwa gharama ndogo. “Ni imani yangu sasa tutashuhudia kupanda kwa ufanisi katika utendaji kazi maana nazingira ya kazi kwa sehemu kubwa yatakuwa yameboreshwa,” alisema Mhe. Kandoro.

 Mkuu wa Mkoa aliwapongeza watumishi wote wa TAKUKURU mkoani Mbeya kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini akaeleza kusikitishwa kwake na tabia iliyojengeka ya baadhi ya wananchi, ambao walitegemewa kuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa kuannza kudai rushwa waziwazi. Alitoa mfano wa rushwa inayodaiwa na wananchi wakati wa mchakato wa uchaguzi wa nafasi za uongozi wa kisiasa nchini.

Swali ambalo unapambana nalo ni ‘unatuachaje?’ maana mwenzako ameishapita, ameisha acha, sasa wewe unatuachaje?” alinukuu Mhe. Kandoro na kueleza kuwa hili ni jambo linalotisha. “Tukitaka kufanikiwa lazima kila mtu aichukie rushwa. Ili aichukie rushwa inabidi ajue madhara yake,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na kuitaka TAKUKURU kupanua wigo wa uelimishaji nchi nzima ili kuwaelimisha wananchi kuachana na tabia hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wa Afrika Wanaopambana na Rushwa-Tawi la Tanzania (Africa Parliamentarians Network Against Corruption-APNAC-Tanzania), Dkt. Mary Mwanjelwa aliipongeza TAKUKURU kwa kazi nzuri ya kupambana na rushwa nchini na kuhamasisha umma kupigania ili ipewe meno zaidi ili iweze kushitaki.

Akieleza historia ya ofisi hii, Mkuu wa TAKUKURU Mbeya, Bw. Bw. Xavery Mhyella alisema ilianzishwa mwaka 1978 ambapo wakati huo ilijulikana kwa jina la Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ya Kikosi cha Kupambana na Rushwa na ilihudumia mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Ruvuma. Alieleza kuwa pamoja na mabadiliko ya sheria, majina na muundo wa Taasisi na hata kukua kwa chombo kwa kuongezeka idadi ya watumishi na vitendea kazi, bado Ofisi iliendelea kutumia jengo la ofisi lililokuwa likitumika tangu mwaka 1978.

Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kutambua hilo na kuamua kutujengea majengo mapya ya kisasa na yenye vitendea kazi vya kisasa…. Kwa mazingira ya ofisi ya jengo jipya pamoja na miundombinu yake kutasababisha watumishi wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya kutekeleza malengo ya taasisi kwa weledi na ufanisi mkubwa. Vilevile, kuwepo kwa maktaba ya kisasa katika jengo hili kutasababisha kuongeza kasi katika kukuza uelewa wa wadau mbalimbali juu ya madhara ya rushwa katika jamii kwa lengo la kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na utunzaji mzuri wa kumbukumbu za ofisi,” alisema Bw. Mhyella.

Moja kati ya matukio yaliyojiri katika uzinduzi huo ni hatua ya wazee wa mila mkoani Mbeya kumsimika uchifu Dkt. Hoseah kwa kumfunga mgolole na kumkabidhi silaha aina ya mkuki na fimbo kwa kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa.

Pia, wanafunzi ambao ni wanachama wa klabu za wapinga rushwa walitumbuiza na kuelimisha umma kuacha kutojihusisha na rushwa katika uchaguzi kwa njia ya igizo, ngonjera, ngoma na nyimbo. Hizi ni Klabu ya Wapinga Rushwa kutoka Shule ya Sekondari Wenda, Shule ya Sekondari Iyunga na Shule ya Sekondari Hayombo.

Hafla hii ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi wengine akiwemo Mkaguzi wa Kanda wa TAKUKURU, Bi Joyce Shundi, Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa, viongozi wa dini, Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali na viongozi wa mila. Wengine ni Wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya zilizoko Mbeya, wanafunzi, waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa Mbeya na watumishi wengine wa TAKUKURU.

DKT HOSEAH – RAIS WA EAAACA KWA MARA NYINGINE TENA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Dkt. Edward G. Hoseah, amechaguliwa kwa mara nyingine tena kuwa Rais wa Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (East African Association of Anti-Corruption Authorities- EAAACA).

Uchaguzi huo umefanyika leo Jumanne tarehe 29/09/2015 jijini Entebe – Uganda, katika Mkutano Mkuu wa 8 wa shirikisho hilo ulioanza leo.

Hii ni mara ya pili kwa Dkt Hoseah kuchaguliwa kushika wadhifa huo kwani yeye ndiye aliyekuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo lililoanzishwa mwaka 2007.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwake, Dkt Hoseah amesema katika kipindi cha uongozi wake kama Rais wa EAAACA (2015 -2017) atatoa kipaumbele katika kutekeleza yafuatayo:

 1. Kuweka mikakati michache inayotekelezeka ikiwemo kufanya tafiti za kuziba mianya ya rushwa katika mifumo mbalimbali ya Taasisi katika za nchi za Afrika Mashariki.
 1. Kuimarisha uhusiano kati ya Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki na kuongeza jitihada za kuhakikisha EAAACA inajumuishwa katika Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (East African Community).

Shirikisho hilo linalojumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, liliundwa rasmi Septemba 28, 2007, ambapo viongozi wa TAKUKURU (Tanzania), IG (Uganda) na KACC (Kenya) - ambao ndio waanzilishi, walisaini azimio la kuwa na Ushirikiano wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki.

Azimio hilo lilipewa jina la ‘AZIMIO LA KAMPALA’ na lilitamka kwamba:

 • Taasisi hizi zinarejea dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na kufanya kazi pamoja katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.
 • Taasisi hizi zinatambua kuwa rushwa inaweza kuharibu ufanisi wa kiutendaji wa jamii yoyote, inahatarisha demokrasia, ukuaji wa uchumi na utawala wa sheria. Kwa msingi huu, Taasisi hizi zinaendelea kutilia mkazo kuundwa kwa EAAACA kama jukwaa la kubadilishana taarifa, uzoefu na kukuza ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kuzuia na kupambana na rushwa katika sura zake zote.
 • Taasisi hizi zinatambua kuwa jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mtu katika kila jamii na kwamba mapambano haya yanahusisha ulinzi na uimarishaji wa maadili katika jamii zote.
 • Uamuzi wa kuingia katika makubaliano haya na kuundwa kwa Ushirikiano huu ni ishara ya kweli ya dhamira ya kila moja ya Taasisi hizi katika kutokomeza rushwa.

Kuundwa kwa EAACA ni ishara ya wazi ya dhamira ya viongozi wakuu wa taasisi hizi katika kutekeleza kwa mafanikio jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa katika nchi zao. Hatua hii pia, kama inavyojieleza katika tamko hilo, inazidi kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kila mwanajamii na mataifa katika kukabiliana na tatizo la rushwa duniani.

Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 8 wa EAAACA inasema ‘Uimarishaji wa jitihada za kuzuia na kupambana na Rushwa katika nchi za Afrika Mashariki' na mkutano ujao wa mwaka, umepangwa kufanyika Tanzania mwaka 2016.

Imetolewa na Doreen J. Kapwani, Afisa Uhusiano wa TAKUKURU, Jumanne tarehe 29/10/2015

DR. HOSEAH - THE NEW CHAIRMAN OF AAACA

The 5th Commonwealth Regional Conference for Heads of Anti- Corruption Agencies in Africa, which was held in Dar es Salaam – Tanzania from 25th to 29th May,2015 at Ledger Plaza- Bahari Beach Hotel, elected Dr. Edward G. Hoseah - Director General of PCCB – Tanzania, to be the Chairman of AAACA for the year 2015/ 2016.

Association of Anti-Corruption Agencies in Commonwealth Africa (AAACA) was formed in Gaborone - Botswana in the year 2011 for the purpose of promoting collaboration and peer learning among the member countries.

Heads of Anti Corruption Agencies from the member countries has a custom of meeting annually aiming at sharing country experiences through strengthened network and also provides a unique platform for sharing emerging practices and country innovations in the fight against corruption. By doing so they become in a better position to advice their respective governments on how best to curb the challenges of corruption and therefore promote good governance in Commonwealth Africa. The Chairman for the year 2014/2015 was from Ghana.