Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imempandisha kizimbani aliyekuwa Mkuerugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani Oktoba 13, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Sofia Masati, ambapo alisomewa shtaka na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, John Sang’wa.

Kati ya Septemba 6 na 8, 2016 mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kama Mkurugenzi Mtendaji alitumia vibaya madaraka yake wakati akitekeleza majukumu yake.
Mshtakiwa aliipa kazi kampuni ya CMJT LTD kutoa ushauri katika mradi wa kuandaa mpango mkakati wa KEC huku akijua CMJT LTD inaamilikiwa na yeye, mke wake na watoto wake kwa gharama ya sh. 19,050,000/= na hivyo kuiwezesha CMJT kujipatia manufaa ya kiasi hiki cha fedha pasipo kustahili.
Pia, utaratibu wa kuipatia kazi kampuni hiyo ulikiuka sheria ya Manunuzi ya umma kwa kuwa haikushindanishwa wala kuangaliwa vigezo vyake iwapo ilikidhi mahtaji ya Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Fedha za kufanyia kazi ya ushauri zilitolewa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) na mshtakiwa aliidhinisha kampuni yake kulipwa kupitia kwenye akaunti yake binafsi ya benki.

Pamoja na kulipwa kiasi hiki cha fedha, CMJT LTD haikufanya kazi ya kutoa ushauri kwa KECna na badala yake ilifanywa na watumishi wa shirika la Elimu Kibaha (KEC).
Mshtakiwa alisomewa mashtaka akiwa amelala kitandani katika wodi namba 116 VIP katika hospitali ya Tumbi Kibaha, Pwani ambako amelazwa kwa ugonjwa na alikana shtaka linalomkabili.
Baada ya kusomewa shtaka, hakimu Masati alisema dhamana ilikuwa wazi na mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja waliotakiwa kusaini bondi ya sh.milioni 20 kila mmoja.
Hata hivyo, wadhamini walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na mshtakiwa alibaki chini ya ulinzi wa polisi akiwa hospitali hadi oktoba,25, mwaka huu kesi itakapotajwa tena.