• Mwanjelwa ashauri Sheria ihuishwe kuongeza ukali adhabu kwa mafisadi
  • Waziri Mhe. Kairuki akubali Sheria ina mapungufu

 

Na John Kabale, Dodoma,

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoendelea na vikao Dodoma, wamesifia utendajikazi mzuri wa TAKUKURU kwa mwaka wa fedha  wa 2016/2017 wakati wa mjadala wa hotuba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Ofisi hiyo Mhe. Angella Jasmine Kairuki (Mb), Aprili 18, 2017.

Akichangia vifungu vya bajeti ya Wizara hiyo, Mbunge wa Viti Maalum Mbeya Mjini,  ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wanaopambana na Rushwa Tanzania (APNAC- Tanzania Chapter) Mhe. Mary Mwanjelwa, aliipongeza TAKUKURU kwa kuokoa fedha nyingi lakini alionyesha kukerwa na adhabu ndogo zinazotolewa kwa mafisadi. “Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Grand corruption na zile Mahakama za Kifisadi mpaka sasa hivi ni kizungumkuti na adhabu zinazotolewa ni kama tunaleta utani kwa sababu haziendani na uzito wa kosa”, alichangia akitaka ufafanuzi wa Serikali.

Naye Mhe. Abdallah Bulembo, Mbunge wa Kuteuliwa, aliipongeza Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John pombe Magufuli kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na aliipongeza TAKUKURU kwa kufanikisha kuokoa  bilioni 53 ambazo zimeonyeshwa kwenye taarifa iliyowasilishwa kwa Rais hivi karibuni. Mbunge aliliambia Bunge kuwa “Nikupongezeni kwenye eneo la utawala Bora kwenye eneo la TAKUKURU…Juzi Waliwasilisha kwa Mheshimiwa Rais taarifa inayoonyesha wameokoa bilioni 53, siyo kazi ndogo, ni kazi ya kusifia”.

Kwa upande wake mbunge wa viti Maalum (Unguja Kaskazini) Mhe. Angelina Adam Malembeka,  mbali na kuipongeza TAKUKURU kwa kazi nzuri inayofanya na kuokoa fedha nyingi,  aliishauri Serikali kuwa fedha zinazookolewa na TAKUKURU ziijulikane zinaenda kufanya nini na ikiwezekana zitumike kwa kazi nyingine kwa vile sehemu nyingi wananchi wana matatizo mengi.

Wakati akihitimisha hotuba yake Aprili 20, 2017, Waziri Mhe. Kairuki alikubaliana na hoja ya Mhe. Mwanjelwa na alikiri kuwa Serikali inaona umuhimu wa kuifanyia mabadiliko Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 kutokana na kupitwa na wakati takribani miaka 10 tangu itungwe na mambo mengi yamebadilika kiteknolojia. “Kwa hiyo niseme kwamba tunataka tuje na sheria kali, ni imani yangu Waheshimiwa Wabunge tutakapoileta hapa mtaweza kutuunga mkono…maana tumeshaanza mchakato wa kuibadilisha katika ngazi ya Serikali”. Aliwaahidi Wabunge.

Bajeti ya  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mafungu yote  iliidhinishwa na Bunge kiasi cha shilingi 821,322, 347,674 ambapo TAKUKURU ilipangiwa shilingi bilioni 13,309,406,000. Kutokana na majukumu mbalimbali yanayoongezeka kutokana na kuongezeka kwa taarifa za vitendo vya rushwa zinazowasilishwa na wananchi kutokana na uelewa unaongezeka kutokana na kampeni mbalimbali za uelimishaji umma ikiwemo kampeni ya LONGA NASI inayohamasisha matumizi ya simu ya bure ya 113 bajeti ya TAKUKURU bado ni ndogo na Wabunge wengi waljaribu kuishawishi Serikali na Bunge ili TAKUKURU iongezewe bajeti kwa vile imeokoa fedha nyingi.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Jasmine Kairuki (Mb), akiwasilisha hotuba ya ofisi yake bungeni Aprili 18, 2017 kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/2018

Mbunge wa viti Maalum (Mbeya Mjini), Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa akichangia mjadala Bungeni kuhusu Makadirio ya Matumizi ya fedha ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa fedha wa 2017/2018.